Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-04-23 18:42:05    
Bw. Maliki yuko ziarani nchini Misri kufanya maandalizi ya kufanyika kwa mkutano wa kimataifa kuhusu usalama wa Iraq

cri

Waziri mkuu wa Iraq Bwana Nuri al-Maliki tarehe 22 aliwasili Cairo kufanya ziara yake ya kwanza nchini Misri tangu ashike madaraka. Lengo la ziara ya Bw. Maliki nchini Misri ni kufanya maandalizi ya kufanyika kwa mkutano wa kimataifa kuhusu usalama wa Iraq mwanzoni mwa mwezi ujao huko Sharm el-Sheikh nchini Misri. Baadaye Bw. Maliki pia atafanya ziara katika nchi za Ghuba zikiwemo Saudi Arabia, Kuwait, umoja wa falme za kiarabu na Oman.

Mkutano wa mawaziri utakaowashirikisha wajumbe wa nchi tano wajumbe wa kudumu wa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa, kundi la nchi nane na nchi jirani za Iraq unatazamiwa kufanyika huko Sharm el-Sheikh tarehe 3 hadi 4 mwezi Mei kwa ajili ya kutafuta ufumbuzi wa mgogoro wa kumwaga damu nchini Iraq. Siku hiyo Bw. Maliki kwa nyakati tofauti alifanya mazungumzo na rais Hosni Mubarak wa Misri na waziri mkuu Bwana Ahmed Nazif wakijadiliana kuhusu hali ya usalama ya nchini Iraq. Kwenye mkutano na waandishi wa habari uliofanywa pamoja na Bw. Maliki na Bwana Nazif, Bw. Maliki alisema, migogoro ya kimabavu iliyotokea hivi karibuni nchini Iraq yote ilifanywa na magaidi wa kundi la al Qaeda na wafuasi wake. Migogoro ya kimabavu kati ya madhehebu ya Suni na madhehebu ya Shia imedhibitiwa kwa kiasi kikubwa. Naye Bw. Nazif alisema serikali ya Misri inaunga mkono juhudi za serikali ya Iraq za kufikia maafikiano kati ya madhehebu mbalimbali ya kidini na makundi mbalimbali ya kijamii nchini humo, na kulaani shughuli za kigaidi dhidi ya raia.

Mada nyingine muhimu iliyojadiliwa kati ya Bw. Maliki na viongozi wa Misri ni kuboresha uhusiano kati ya nchi hizo mbili. Tangu serikali ya madhehebu ya Shia iliyoongozwa na Bw. Maliki iundwe, migogoro ya kimabavu kati ya madhehebu ya Suni na Shia ilitokea mara kwa mara, nchi jirani za Iraq na Misri zina wasiwasi kuwa, hali ya usalama inayozidi kuwa mbaya nchini Iraq kutahatarisha usalama na utulivu wa sehemu ya mashariki ya kati. Bw. Nazif alisema ziara hii ya Bw. Maliki nchini Misri itahimiza maendeleo ya uhusiano wa pande mbili kati ya Misri na Iraq, na kueleza msimamo imara wa Misri wa kuunga mkono kwa nguvu zote jitihada za Iraq za kuleta amani na utulivu. Na Bw. Maliki na Bw. Nazif wameeleza kwa kauli moja kuyahimiza makampuni ya Misri kurudi nchini Iraq na kushiriki katika ukarabati wa Iraq.

Wachambuzi wameona kuwa hali ya usalama inayozidi kuwa mbaya, kutokea mara kwa mara kwa migogoro kati ya madhehebu ya kidini na shughuli za kigaidi nchini Iraq kunatishia vibaya amani, usalama na utulivu wa nchi jirani zake na sehemu ya mashariki ya kati, namna ya kuisaidia Iraq kukomesha migogoro ya kumwaga damu haraka iwezekanavyo, na kurejesha amani na utulivu wa Iraq kumekuwa jambo linalokubaliwa pamoja na jumuiya ya kimataifa. Kabla ya kufanyika kwa mkutano wa kimataifa kuhusu usalama wa Iraq, Bw. Maliki anafanya ziara nchini Misri na nchi nyingine za kiarabu kwa lengo la kuziarifu kuhusu hali ya usalama ilivyo nchini Iraq na kuboresha uhusiano kati ya nchi hiyo na nchi jirani, ili kushirikiana na nchi husika kukabiliana kwa pamoja changamoto za kigaidi, na kutafuta njia mwafaka ya kutuliza hali ya usalama ya Iraq, hatua hii itachangia sana kuboresha hatua kwa hatua hali ya usalama ya nchini Iraq.