Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-04-24 15:37:38    
Majaribio mapya ya mageuzi ya mambo ya fedha vijijini nchini China

cri

Mageuzi ya mambo ya fedha vijijini ni sehemu muhimu ya mageuzi ya mambo ya fedha nchini China. Katika miaka ya hivi karibuni, idara ya usimamizi wa fedha ya China imekuwa inarekebisha sera ya kuingia kwa idara za fedha za benki vijijini, na kuhimiza mitaji mbalimbali kuingia katika idara za fedha vijijini, ili kuwasaidia wakulima milioni 800 kuongeza mapato yao haraka. Wakati huohuo idara za aina mpya za fedha zinazofaa vijiji pia zinatokea vijijini.

Baada ya katikati ya miaka ya 90 ya karne iliyopita, kutokana na kuwepo kwa wasiwasi wa hatari ya mikopo, benki mbalimbali kubwa za biashara za China ziliondoka kutoka sehemu za vijijini. Hii ilisababisha hali fulani ya kutokuwepo kwa huduma za mkopo katika sehemu za vijijini, isipokuwa mikopo isiyo ya kiserikali, na ilikuwa ni vigumu kwa wakulima kupanua uzalishaji au kushughulikia shughuli za kiuchumi kwa mikopo ya idara rasmi za fedha. Lakini hivi sasa hali hiyo inabadilika.

Tarehe 1 Machi mwaka huu, mikoa ya Sichuan na Jilin ilianzisha idara tatu za aina mpya za fedha, yaani benki za tarafa. Kutokana na sheria husika, benki hizo zinazotoa huduma mahsusi kwa sehemu za vijijini, huduma zinazotolewa na benki hizo kwanza zinatakiwa kukidhi mahitaji ya maendeleo ya uchumi wa vijiji. Mkuu wa benki ya tarafa ya Chengxin iliyoko wilayani Dongfeng mkoani Jinlin Bw. Ding Xiaobo alimwambia mwandishi wa habari kuwa, wateja wengi wa benki hiyo ni wakulima wa huko.

"Benki ya tarafa ya Chengxin ya Dongfeng imeanzishwa kwa wakulima, na miradi yetu ni kutoa mikopo kwa ajili ya kilimo na ufugaji kwa wakulima wakati wa uzalishaji, ili kuwasaidia wakulima waongeze mapato haraka, na kutoa huduma kwa kujenga vijiji vipya vya ujamaa."

Imefahamika kuwa benki ya tarafa inaidhinisha na kutoa mikopo kwa haraka, na riba ya mikopo ni ndogo kuliko ile ya mikopo isiyo ya kiserikali, pia inaweza kuvumbua shughuli mbalimbali za fedha kutokana na hali halisi ya maendeleo ya kilimo na uchumi wa vijiji, na kufanya uendelezaji kutokana na kanuni ya soko.

Pamoja na benki za tarafa, makampuni yanayotoa mikopo midogo pia yanatokea katika sehemu mbalimbali nchini China, na wanaopewa huduma ni wakazi na viwanda vya sehemu za vijijini. Makampuni hayo yanasajiliwa katika idara ya viwanda na biashara, na yamepata hadhi ya kisheria, ambayo fedha za mitaji iliyosajiliwa zinatumika kama ni mtaji wa kuanzisha shughuli zao, na yanatoa mikopo kwa kikomo cha riba kubwa ya mara nne ya ile ya serikali . Mwandishi wetu wa habari alipofanya mahojiano wilayani Pingyao, mkoani Shanxi, kaskazini mwa China alifahamishwa kuwa, hivi sasa wanavijiji wengi wanachagua kukopa kutoka makampuni yanayotoa mikopo midogo. Katika makampuni mawili maarufu yanayotoa mikopo midogo huko Rishengrong na Jinyuantai, mwandishi wa habari aliona wakulima waliokuwa wanakuja kukopa kila mara. Wakulima wanaweka dhamana ya vitu au walikuwa wanadhaminiwa na watu wengine, na kwa kawaida wanaweza kupewa fedha ndani ya siku tatu hivi. Mwanakijiji Wang Zhongqing alimwambia mwandishi wa habari kuwa, aliwahi kukopa Yuan za RMB elfu 50 kutoka kwenye shirika linalotoa mikopo midogo, na hivyo kutatua tatitzo la kukwama kwa mzunguko wa fedha. Anaona kuwa kukopa kutoka kwenye makampuni yanayotoa mikopo midogo ni rahisi sana kuliko kukopa kutoka kwenye chama cha ushirika cha fedha vijijini.

Kabla ya kuanzishwa kwa benki za tarafa na makampuni yanayotoa mikopo midogo, watu wengi walieleza wasiwasi kwa hatari ya mikopo ya vijiji. Waliona kuwa wakulima hawakuwa na mwamko wa kutumia mikopo, hii ilileta hatari kubwa kwa kurudisha mikopo ya makampuni ya fedha. Lakini hivi sasa makampuni yanayotoa mikopo midogo ya Shanxi hayakukumbwa na hali ngumu ya kutolipwa kwa mikopo. Naibu meneja mkuu wa kampuni inayotoa mikopo midogo ya Rishengrong Bw. Guo Tongliang alisema,

"Hadi sasa tumerudisha asilimia 100 ya mikopo kwa wakati; na tumerudisha asilimia 100 ya riba kwa wakati."

Wataalam wanaona kuwa, benki za tarafa, makampuni yanayotoa mikopo midogo, pamoja na vyama vya ushirika vijijini vitakuwa watoaji wakuu wa mikopo kwa sehemu za vijijini katika siku za baadaye, ambayo yatahimiza mfumo wa fedha vijijini.

Kama tukisema kuwa benki za tarafa na makampuni yanayotoa mikopo midogo kwa kiwango fulani zinatatua tatizo la ukosefu wa vyanzo vya fedha za mikopo vijijini, basi benki ya posta ya China iliyoanzishwa muda mfupi uliopita inatazamiwa kuboresha kiwango cha utoaji huduma wa fedha kwa wakulima. Benki ya posta ya China inaundwa kwa msingi wa mtandao wa mfumo wa posta wa China, hivi sasa benki hiyo ina matawi elfu 36, miongoni mwake asilimia 70 yako katika sehemu za vijijini. Meneja mkuu wa benki ya posta ya China Bw. Liu Andong alisema, benki hiyo itaunda idara zinazotoa huduma mahsusi za fedha vijijini, ili kupanua shughuli zake vijijini, na kutoa huduma bora za fedha kwa wateja wa vijiji. Alisema

"Benki ya posta ya China itakapoundwa itafanya juhudi zaidi kujenga mtandao wa utoaji huduma wa fedha, ambao matawi yake yataenea kote nchini."

Lakini benki za tarafa, makampuni yanayotoa mikopo midogo na benki ya posta zote zinakabiliwa na matatizo mengi ya maendeleo. Kwa mfano makampuni yanayotoa mikopo midogo, kutokana na sera ya hivi sasa, makampuni hayo yanaweza tu kutumia fedha za mitaji zinazosajiliwa kama fedha za kuanzisha shughuli za kutoa mikopo, hayawezi kuchukua akiba kama benki za biashara kuongeza fedha, hali hii inayazuia kupanua shughuli zao. Mtaji uliosajiliwa wa kampuni inayotoa mikopo midogo ya Rishengrong mkoani Shanxi wakati ilipoanzishwa ni Yuan za RMB milioni 17, lakini baada ya miezi 6 tu, kwa ujumla lilitoa mikopo zaidi ya Yuan za RMB milioni 16. Meneja mkuu wa kampuni hiyo Bw. Liu Weihui alisema, wenye hisa wa kampuni hiyo waliongeza Yuan milioni kadhaa, lakini fedha hizo bado haziwezi kukidhi mahitaji ya maendeleo ya shughuli zao. Alisema anatumai kuwa serikali itafanya utafiti na kurekebisha sera husika, ili kupanua vyanzo vya fedha vya makampuni yanayotoa mikopo midogo.

Wataalam wamesema ili kuinua kihalisi kiwango cha utoaji huduma wa fedha vijijini, ni lazima kutunga sera zenye unafuu, kuhimiza mabenki mengi zaidi kwenda kwenye sehemu za vijijini kuanzisha matawi yao, na kuyasaidia kuongeza fedha za mitaji. Kuhusu hayo, mwenyekiti wa kamati ya usimamizi wa sekta ya benki ya China Bw. Liu Mingkang alisema, China itarekebisha sera husika za usimamizi ili kuunga mkono maendeleo ya fedha vijijini.

Idhaa ya kiswahili 2007-04-24