Baada ya waziri mkuu wa Iraq Bw. Nuri al-Maliki kuonesha upinzani dhidi ya jeshi la Marekani kujenga ukuta nchini Iraq, balozi wa Marekani nchini Iraq Bw. Ryan Crocker tarehe 23 alisema ataheshimu maoni ya serikali ya Iraq, lakini hakusema wazi kusimamisha ujenzi wa ukuta huo.
Tokea tarehe 10 mwezi huu, jeshi la Marekani nchini Iraq lilianza kujenga ukuta wa utenganishaji usiku na mchana katika sehemu ya Azamiyah kwenye ukingo wa mashariki wa mto Tigris nchini Iraq, ili kutenganisha sehemu ya Wasuni na sehemu ya Washia. Kwa mujibu wa mpango, ukuta huo wa saruji una urefu wa kilomita tano, kimo cha juu kabisa kwenye sehemu fulani kinafikia mita 3.5, na utakamilishwa mwishoni mwa mwezi huu. Baada ya ukuta huo kukamilishwa, sehemu ya Azamiyah itafungwa, wakazi wataweza tu kupita kwenye mlango, na askari wa Iraq watawajibika kulinda mlango huo na kukagua watu wote wanaopita. Ofisa wa jeshi la Marekani anayeshughulikia ujenzi wa ukuta huo alisema, baada ya ukuta huo kukamilika, itakuwa ni vigumu kwa watu wenye silaha wa madhehebu ya Shia na magaidi kuingia kwenye sehemu ya Azamiyah, usalama wa sehemu hiyo utaboreshwa, na vitendo vya mauaji kwenye makazi ya Washia vitapungua. Mbali na sehemu ya Azamiyah, jeshi la Marekani litajenga sehemu kadhaa zinazozingirwa ndani ya mji wa Baghdad. Kadhalika jeshi hilo litajenga vituo kadhaa vya ukaguzi wa usalama mjini Baghdad na kuimarisha doria. Gazeti la Uingereza, The Independent, tarehe 11 lilitangaza kuwa jeshi la Marekani limekuwa likijiandaa kuchukua hatua kali dhidi ya vita vya msituni katika mji wa Baghdad, na kutenganisha mitaa 30 kati ya mitaa 89 ya mji huo ili kuhakikisha usalama.
Inasemekana kwamba, mbinu ya kujenga "sehemu zinazofungwa" kwa kujenga ukuta wa utenganishaji ilitolewa na amirijeshi mkuu wa jeshi la Marekani nchini Iraq Bw. David Howell Petraeus. Watu wanaona kuwa mbinu hiyo inahusiana na mpango wa usalama ulioandaliwa na majeshi la Marekani na Iraq na kuanza kutekelezwa mwezi Februari. Lakini mpango huo haukuleta matokeo dhahiri katika muda zaidi ya miezi miwili tangu ulipoanza kutekelezwa.
Zaidi ya hayo, kabla ya ukuta wa Azamiyah kukamilishwa kelele za upinzani zimesikika nchini Iraq. Tarehe 23 wakazi mia kadhaa wa Baghdad walifanya maandamano kupinga ujenzi wa ukuta huo. Ingawa balozi wa Marekani nchini Iraq Bw. Ryan Crocker aliwaelezea waandamanaji kuwa ujenzi wa ukuta wa utenganishaji ni kwa ajili ya kulinda usalama wa sehemu ya makazi, bali sio kwa ajili ya kutenganisha sehemu ya makazi. Lakini vyombo vya habari vya Iraq vinaona fikra za kujenga ukuta ni "upuuzi", kwani kufanya hivyo licha ya kutoweza kuondoa vitendo vya mauaji, kutaitenganisha sehemu ya Azamiyah na sehemu nyingine, na kuleta matatizo ya usafiri wa wakazi na maendeleo ya makazi. Baadhi ya watu wanasema ukuta huo utazidisha mgawayo kati ya Washia na Wasuni.
Aidha, vyombo vya habari pia vinasema mbinu ya kuleta usalama kwa kujenga ukuta wa utenganishaji sio mbinu mpya. Mwezi Agosti mwaka jana jeshi la Marekani nchini Iraq lilijenga ukuta wa saruji kusini mwa mji wa Baghdad ili kuzuia migogoro kati ya madhehebu ya kidini, na sehemu ya katikati ya mji huo yaani "sehemu ya kijani" pia ilifungwa kwa ukuta. Lakini yote hayo hayakusaidia kuboresha mazingira ya usalama. Tarehe 12 mwezi huu jengo la bunge kwenye sehemu hiyo ya kijani lilikumbwa na mlipuko wa bomu la kujiua. Wachambuzi wanaona ukuta wa utenganishaji sio ukuta wa usalama, sio dawa zuri ya kutuliza vurugu na kuleta usalama nchini Iraq, na baadhi ya maofisa wa jeshi la Marekani pia walisema, mbinu ya kujenga ukuta wa utenganishaji iliwahi kutumika katika miaka ya vita dhidi ya Vietnam, lakini haikusaidia.
Idhaa ya kiswahili 2007-04-24
|