Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-04-24 18:35:54    
Barua0422

cri

Msikilizaji wetu Bw. Mbaraka Mohammed Abucheri wa P.O. Box 792, Kakamega Kenya ametuletea barua akianza kwa salamu kwa wasikilizaji wa Radio China Kimataifa, na kutoa pongezi kutokana na kuongeza muda wa matangazo katika mawimbi ya FM. Lengo la barua ya msikilizaji wetu huyu ni kutoa mkono wa pongezi kwa uongozi na wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya Radio China Kimataifa, kuongeza muda wa Matangazo kwenye mawimbi ya FM, matangazo ambayo yanasikika huko Nairobi, Kenya.

Anasema matangazo hayo yanasikika kuanzia saa mbili hadi saa tatu asubuhi, na kuanzia Saa sita hadi saa saba mchana. Matangazo mengine yanasikika kuanzia saa mbili hadi saa nne usiku. Anaona kuwa hii ni hatua kubwa iliyofikiwa na Idhaa ya Kiswahili ya Radio China Kimataifa katika mambo ya utangazaji na hasa tukizingatia wakati huu, ambao ni wa ushindani mkubwa kote duniani. Pia anasema ni matumaini yake kuona uongozi wa Radio China Kimataifa unaweka mikakati ya kuendeleza ubora wa matangazo yake, kwani kuongeza muda wa matangazo kumezidisha kujenga uhusiano wa karibu kwa wasikilizaji wake, kote Afrika mashariki na kudumisha mawasiliano mazuri yenye kuendeleza manufaa ya pande zote zinazohusika.

Anasema anatupa changamoto ya kuendeleza juhudi zetu bila kuhofu wala kuchoka, na wao wasikilizaji wanaendelea kutuunga mkono kwa kutoa maoni na mapendekezo ili tuweze kuboresha matangazo na vipindi vya Idhaa ya Kiswahili ya Radio China Kimataifa.

Tunamshukuru sana msikilizaji wetu Mbaraka Mohamed Abucheri kwa barua yake, tunakubaliana na changamoto aliyotupa ya kuendelea kuchapa kazi. Pia tunafurahi sana kusikia kuwa wasikilizaji wetu mnafurahia kuongezwa kwa muda wa matangazo yetu. Hata hivyo hiyo inatokana na maoni na mapendekezo yenu, kwa hiyo tunatumai kuwa mtaendelea kutoa maoni na mapendekezo yenu, ili tuweze kuboresha zaidi matangazo yetu.

Msikilizaji wetu Bw. Caleb wa Kenya yeye pia ametuandikia barua akianza kwa salamu kwa wasikilizaji wenzake na wafanyakazi wa Radio China kimataifa. Yeye ana mapendekezo mbalimbali, kwanza anasema anaona ingekuwa ni vizuri sana kama kipindi cha Jifunze kichina kingesikika saa kumi kwa saa za Afrika mashariki, ili watu wengi zaidi waweze kupata nafasi ya kukisikiliza. Pendekezo lake lingine anasema, pamoja na kuwa matangazo yetu yanasikika kwenye mawimbi ya FM Nairobi na kupitia KBC, anaona itakuwa ni vyema kama matangazo ya masafa mafupi yataendelea kuboreshwa. Mbali na mapendekezo hayo, anasema anashukuru sana kwa Radio China kimataifa kuweza kumuunganisha na wasikilizaji wengine na kuweza kuwasiliana nao kwa salamu, na anashukuru kwa kuongeza muda wa kipindi hicho.

Tunamshukuru sana msikilizaji wetu huyu Caleb kutoka huko Kenya. Tunapenda afahamu kuwa, pamoja na kwamba matangazo yetu yanasikika kwenye mawimbi ya FM huko Nairobi, na kupitia shirika la utangazaji Kenya KBC, hii haina maana kuwa tumesahau matangazo yetu yanayosikika kwenye masafa mafupi, juhudi pia zinaendelea kufanyika ili kuhakikisha kuwa wasikilizaji wetu wanapata usikivu mzuri.

Msikilizaji wetu Gulam Haji Karim wa P.0.Box 504 Lindi, Tanzania ametuletea barua akitoa Pongezi kwa Serikali ya Watu China. Msikilizaji wetu huyu anaipongeza ziara aliyoifanya rais wa China katika Nchi za Afrika. Lakini pia kwa rais wa China kuwaalika viongozi wan chi za Afrika nchini China, na kuwaeleza kuwa watu wa China wako pamoja na Watu wa Afrika katika kujikomboa kiuchumi na maendeleo ya watu wa Afrika. Kama hiyo haitoshi rais wa China alitoa ahadi ya kuzisaidia nchi za Afrika kwa kuzipatia mikopo mikubwa yenye masharti nafuu, na kufuta madeni ya zamani. Anasema katika ziara katika baadhi ya nchi za Afrika, rais wa China, aliweza kujionea matatizo mbalimbali yanayozikabili nchi nyingi za Afrika. Kwa mfano matatizo barabara, ukosefu wa maji safi na salama, elimu duni na maendeleo ya mtu mmoja mmoja. Ziara hiyo imezidi kufungua mlango kati ya China na Afrika kwa kubadilishana, kuuza na kununua bidhaa mbalimbali. Anamaliza barua yake kwa kusema udumu urafiki kati ya China na Tanzania na udumu urafiki kati ya China na Afrika.

Msikilizaji wetu Gabriel Simiyu Wekesa wa S.L.P.292 Kimilili, Kenya ametuletea barua akitoa Pongezi kwa Radio China Kimataifa. Kwanza ni pongezi kwa kazi za kila siku za kuwapasha habari za ulimwengu kupitia Radio China Kimataifa, na pili ni kwa vipindi mbalimbali vikiwemo vya Safari nchini China, Sanduku la Barua na Jifunze kichina, na ameelimishwa kuhusu mambo mengi sana. Anasema katika kipindi cha Safari nchini China, amejua kuwa nchi ya China ina mandhari nzuri, mkoani Sichuan ambapo kuna bonde la Jiuzhaigou, na ambayo ni maskani ya wanyama Panda. Mwisho anamshukuru sana msikilizaji wetu mwingine anayeitwa Ayub Mutanda kwa kumpatia anuani ya Radio China Kimataifa, na anasema ataendelea kuwasiliana nasi.

Msikilizaji wetu Kennedy Nyongesa Barasa wa S.L.P.172 Siaka Kijijini, Bungoma, Kenya, ametuletea barua kuhusu Sherehe ya Sikukuu ya Mwaka Mpya wa Jadi wa China. Anasema kwa mara ya kwanza tarehe 18/02/2007 klabu yao ilijumuika na kusheherekea sikukuu ya mwaka Mpya wa Jadi wa China. Walikuwa watu 34 na wageni wao waliofika walikuwa sita. Anasema ingawa hawakuwa na vyakula vya kichina, lakini walitumia chai ya kichina na vyakula vingine vya wenyeji. Wageni wetu walikaribishwa kwa kushangiliwa kutokana na wao kuvaa mavazi ya kichina na yaliyokuwa na maandishi ya Radio China Kimataifa. Wageni wao walionekana kufurahishwa na mapambo ya picha na maandishi ya kichina waliyotumiwa katika kupamba jengo lao kwa ajili ya sherehe. Baadaye mmoja wa wageni wao aliwaeleza maana na matumizi ya maandishi waliyopamba. Pia aliwasimulia jinsi Bw Mutanda alivyotembelea nchini China. Kuhusu chai alisema twende Hangzhou kuonja chai ya Longjing. Aliwaeleza kuwa chai ya Longjing imekuwa na historia ya zaidi ya miaka 1,200. Ilianzia huko katika kijiji cha Longjing, kusini magharibi ya ziwa la Xihu la Hangzhou. Wanachama wengi kweli walionekana kuifurahia Radio China Kimataifa. Sherehe ilimalizika kwa watu kupewa kalenda na kadi za salamu na pia kuwataka wasikilize Radio China Kimataifa kwani ni daraja la urafiki. Anasema anaamini kuwa sherehe hiyo iliwasaidia watu kujua kuwa tarehe 18/02/2007 wamesheherekea na watu wa China, Sikukuu ya mwaka mpya wa Jadi wa China.

Tunamshukuru sana msikilizaji wetu Kennedy Nyongesa kwa maelezo yake marefu kuhusu jinsi walivyosherekea mwaka mpya wa jadi wa China. Maelezo yake yanatuonesha kuwa wasikilizaji wetu mbali na kufuatilia matangazo yetu, pia wanajaribu kujifunza utamaduni wa China, kama vile kuvaa mavazi ya kichina na hata kujaribu kupika chakula cha kichina na kunywa chai ya kichina. Tunafurahi kusikia kuwa klabu yenu ilisherekea vizuri mwaka mpya wa jadi wa China, tunatumai kuwa mtaendelea kujifunza mengi kutokana na matangazo yetu.

Msikilizaji wetu Yaaqub Saidi Idambira wa P.O. Box 2519 Kakamega Fans Club, Kenya ametuletea barua akitoa Pongezi kwa kuongeza muda wa matangazo yetu kwenye mawimbi ya FM na kwenye masafa mafupi. Pia anapenda pia kuwapongeza wasikilizaji wenzake waliopata nafasi ya kwanza, ya pili na ya tatu na hasa wale waliopata nafasi maalumu na kualikwa kutembelea mji wa Beijing katika shindano la kuadhimisha miaka 65 ya Radio China Kimataifa. Ombi lake kwa Radio China Kimataifa, ni kutaja orodha ya majina ya watu waliopata nafasi ya nne hadi ya kumi ili kuwapa motisha na hamasa ya kufanya bidii katika mashindano ya chemsha bongo. Ni matarajio yake kuwa tutafanya kama alivyopendekeza. Pia anatushukuru kwa kuongeza muda wa matangazo kwenye mawimbi ya FM jiji la Nairobi, hasa wakati wa asubuhi.

Anasema kwa kweli mabadiliko haya ya kuongeza muda ni ufanisi mkubwa kwa Radio China Kimataifa. Ni matumaini yake uongozi utaendelea na mikakati ya kuboresha na kukifanya kituo cha FM, Jijini Nairobi kuwa kituo rasmi na cha kujitegemea kwa kurusha matangazo na vipindi vyenye mafunzo. Pia ninaomba juhudi zifanyike ili kuhakikisha matangazo ya kituo hiki cha FM yanasikika kote nchini Kenya, hasa mkoa wa magharibi na mikoa mingine ili isikilizwe na wasikilizaji ambao idadi yao inazidi kuongezeka kila kukicha. Pia anatoa pongezi kwa kufanya mabadiliko pia katika matangazo na vipindi ambapo kipindi cha salamu kilikuwa kinaendeshwa na mtangazaji mmoja, lakini sasa hivi kuna watangazaji wawili, anasema hilo ni jambo zuri.