Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-04-26 17:57:31    
Luoping, peponi kwa ndege

cri

Luoping ni wilaya moja iliyopo katika mkoa unaojiendesha wa Ningxia Wahui, kaskazini magharibi mwa China. Ardhi ya huko ina chumvi na magadi nyingi na ipo kwenye mteremko, pia kuna maziwa mbalimbali na eneo kubwa la ardhi oevu. Baada ya juhudi za kuboresha mazingira katika miaka zaidi ya 10 iliyopita, uvuvi umeendelezwa sana huko Luoping, jambo ambalo limefanya mazingira ya huko yaboreshwe sana na kuvutia ndege wengi wanabaki huko kupitisha siku za baridi. Hivi sasa wilaya ya Luoping inajulikana kama peponi kwa ndege.

"Zamani hapa lilikuwa ni eneo kubwa la ardhi ya chumvi na magadi, upepo ukivuma ulileta dhoruba ya mchanga na udongo. Baada ya kuendeleza maziwa, hivi sasa naona hali ya hewa ya huko imeboreshwa." Aliyesema hayo ni Bw. Zhang Yubiao, ambaye ni mkulima anayeishi huko Luoping.

Bwana huyo alianza kujishughulisha na ufugaji wa samaki mwaka 1990, hivi sasa ana mkataba wa kuendeleza shamba lenye hekta zaidi ya 30. Kutokana na familia yake kuchapa kazi kwa miaka zaidi ya 10, ardhi hiyo ya chumvi na magadi na yenye mashimo madogo madogo ikabadilika kuwa na maziwa ya kufugia samaki, na pato la familia hiyo pia limeongezeka. Katika miaka ya hivi karibuni wakulima wengi walianza kujishughulisha na ufugaji wa samaki kama anavyofanya Bw. Zhang Yubiao, jambo ambalo lilileta uhai katika maziwa madogo mbalimbali.

Sambamba na upanuzi wa maziwa ya kufugia samaki na ustawi wa nyasi na miti iliyopo karibu na maziwa hayo, mazingira ya huko yaliboreshwa siku hadi siku na ndege wengi walianza kuishi huko. Hata katika majira ya siku za baridi, ndege wa rangi ya kijivu na ndege weupe wanajitokeza wakiruka angani juu ya maziwa ya kufugia samaki, na hali ya uhai inaonekana popote pale katika mwaka mzima.

Hapo mwanzoni wakulima hawakufurahia samaki, walikuwa na wasiwasi kwamba, ndege wangekula samaki wengi na kuleta hasara kubwa. Lakini serikali ya wilaya ya Luoping ilizingatia uhifadhi wa ndege, ilifanya harakati mbalimbali za kuwaelimisha wakulima umuhimu wa kuwepo kwa ndege, na hatua kwa hatua wakulima walitambua na kukubali umuhimu wa kuhifadhi ndege. Bw. Zhang Yubiao alieleza kuwa, hivi sasa wakulima wanawachukulia ndege kama ni marafiki, wameacha tabia ya kuwafukuza ndege.

Alisema  "Ndege wakija usiwachokoze, waache watue kwenye visiwa vidogo maziwani, ambapo wanaangua mayai visiwani. Hivi sasa ndege wanalindwa kwa sheria ya China, hata kama wakitutia hasara fulani hatutaki kuwasumbua."

Mkulima mwingine Bw. Ma Yun anayejishugulisha na ufugaji wa samaki aliwahi kumwokoa ndege mmoja aina ya korongo wa kijivu aliyeumia. Siku moja bwana huyo alikuwa njiani kurudi nyumbani, aliona ndege mmoja mdogo aliyejeruhiwa akiwa kando ya ziwa. Alimchukua na kwenda nayo nyumbani na kufunga majeraha yake. Pamoja na hayo alivua samaki kutoka kwenye ziwa lake na kumlisha ndege huyo. Kutokana na kutunzwa vizuri na Bw. Ma Yun, ndege alipona kabisa kwa haraka. Katika siku ya kuagana na ndege, majirani walishirikiana na Bw. Ma Yun kumsindikiza ndege huyo.

Kutokana na mazingira mazuri na kuwepo kwa chakula kingi, wilaya ya Luoping sasa ni peponi kwa ndege. Katika majira ya siku za baridi ya mwaka 2006 ndege zaidi ya elfu 20 wanaohamahama walibaki huko bila kuhamia kwenye sehemu ya kusini, hali ambayo ilimfurahisha sana Bw. Ma Yun. Alisema  "Wakati majira ya kuchipua yanaporudi, nitaingiza maji zaidi ziwani, ambapo ndege wa aina mbalimbali watakuja. Wakija watakula samaki ziwani. Nasikia vizuri kuona ndege wengi sana."

Luoping ina raslimali nyingi, kwa mfano kuna hekta zaidi ya 8,600 za ardhi oevu ambayo sasa imeendelezwa. Awali mashimo madogo mbalimbali yalionekana katika sehemu mbalimbali wilayani humo, hivi sasa yamebadilika kuwa maziwa, na ardhi ya chumvi na magadi iliyoachwa na watu sasa pia imepandwa miti.

Naibu mkurugenzi wa kituo cha mazao ya maji cha wilaya ya Luoping Bw. Ren Yongbin alisema  "Serikali ya wilaya yetu inaendeleza uvuvi katika mazingira mazuri ya viumbe. Tulibadilisha mabwawa madogo kuwa maziwa, kupanda mianzi kando ya maziwa na kupanda mayungiyungi ndani ya maziwa, mimea hiyo ni yenye thamani kubwa ya kiuchumi. Hatua hizo zimeboresha mazingira, pia zimeongeza faida za uvuvi na kuinua maisha ya wakulima."

Bw. Tian Xinjiang mwenye umri wa miaka 48 alipata mkataba wa kuendeleza hekta 17 za ardhi iliyoachwa na watu ili kufuga samaki na ndege, pato lake limeongezeka sana. Hivi sasa anataka kujishugulisha na utalii, ana mpango wa kujenga kituo cha kuvua samaki na jukwaa la kutizama ndege kando ya ziwa lake la kufugia samaki. Bw. Tian alisema  "Mazingira yetu yamebadilika kuwa mazuri, ndani ya ziwa kuna maji, kwa hiyo ndege wengi wanakuja. Sisi na ndege tunaishi kwa utulivu, ndege wakija hatuwafukuzi na wala hatuwapigi. Tunatumai kuwa mazingira yatakuwa mazuri zaidi."

Huko wilayani Luoping kuna uhusiano mzuri wenye masikilizano kati ya binadamu na ndege. Ni kawaida kuona kundi kubwa la ndege wakitua mahali fulani, baadhi ya ndege wanapumzika huku wengine wanasafisha manyoya yao, ambapo wapita njia wanapita njia nyingine bila kuwasumbua ndege hao.

Idhaa ya kiswahili 2007-04-25