Mkutano wa Baraza la ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara kati ya China na Kenya ulifunguliwa tarehe 24 Aprili huko Nairobi Kenya, Mkutano huo unalenga kuimarisha ushirikiano kati ya China na Kenya na bara la Afrika katika sekta za uchumi na biashara. Mwenyekiti wa Baraza la mashauriano ya kisiasa la China Bwana Jia Qinglin alitoa hotuba kwenye ufunguzi wa Mkutano huo.
Katika hotuba yake Bwana Jia Qinglin alisisitiza kuwa China na Afrika zinapaswa kushikilia ushirikiano wa kunufaishana ili kupata maendeleo ya pamoja, kupanua maeneo ya ushirikiano, kutilia maanani ufanisi wake wa kijamii ili kuleta manufaa halisi kwa wananchi wa Afrika. Alisema:
China itajadiliana na nchi zinazohusika za Afrika kuhusu kujenga sehemu ya biashara huria na mipango ya biashara yenye sera nafuu kati ya pande mbili mbili, na kuongeza uagizaji bidhaa kutoka nchi za Afrika. Tunapaswa kuweka mkazo katika ushirikiano kuhusu miradi inayohusiana na maisha ya wananchi, kutoa kipaumbele kuzisaidia nchi za Afrika ziendeleze shughuli za utengenezaji wa mazao na utengenezaji wa bidhaa, kuongeza nafasi za ajira na mapato ya kodi, kusukuma mbele maendeleo ya uchumi na jamii, na kuboresha maisha ya wananchi. Serikali ya China itatoa misaada na mikopo yenye riba nafuu kwa nchi za Afrika kutokana na mahitaji yao, kupunguza au kusamehe madeni, kuongeza nguvu ya kutoa mafunzo kwa kuandaa watu wenye ujuzi, kusaidia kujenga shule vijijini, vituo vya vielelezo vya ufundi wa kilimo na vituo vya kinga na tiba ya malaria, ili kuwawezesha wananchi wa Afrika wapate manufaa mapema zaidi.
Aidha, Bwana Jia Qinglin aliahidi pia kuwa serikali ya China itaendelea kuvitaka viwanda na kampuni za China zishikilie maadili ya kazi, kuweka mkazo zaidi kudumisha sifa za bidhaa na kufanya shughuli kwa kufuata sheria, hasa kubeba kwa hiari majukumu ya jamii, kutilia maanani kuhifadhi mazingira ya hifadhi katika nchi wanazofanya kazi barani Afrika, na kujitahidi kuzisaidia jamii za nchi za Afrika, ili wananchi wa Afrika waweze kupata manufaa mengi zaidi kutokana na matokeo ya ushirikiano kati ya China na Afrika.
Maneno hayo yanathibitishwa na takwimu zifuatazo ambazo zinaonesha kuwa, katika miaka hiyo 30, China kwa ujumla imewekeza mitaji ya aina mbalimbali barani Afrika yenye thamani ya dola za kimarekani bilioni 11.7, na kulisaidia bara la Afrika kujenga miradi karibu 900. Na kwa mujibu wa hesabu hivi sasa biashara kati ya Afrika na China inachangia ongezeko la uchumi wa Afrika kwa asilimia 20.
Ushirikiano kati ya Afrika na China unawaletea waafrika manufaa na kustawisha uchumi na jamii ya pande hizo mbili, hii ndiyo sababu ushirikiano huo unakaribishwa na serikali za nchi za Afrika na watu wake. Katika hotuba aliyotoa kwenye ufunguzi wa Mkutano huo, makamu wa rais wa Kenya Bw. Moody Awori alionesha matumaini yake juu ya kukuza ushirikiano huo. Alisema ?
Tunasifu sana maendeleo ya kasi ya uchumi wa China, na kutaka makampuni ya China yaje barani Afrika hasa Kenya kutafuta fursa za uwekezaji. Naona kuwa Mkutano huo utasukuma mbele zaidi maendeleo ya kina ya ushirikiano kati ya China na Afrika katika sekta za uchumi na biashara.
Wanakampuni wa China na Kenya waliohudhuria mkutano huo wameona kuwa hotuba ya Bwana Jia Qinglin imewatia moyo sana, na wameongeza imani yao kuhusu ushirikiano kati ya China na Afrika. Mtendaji mkuu wa Shirikisho la wazalishaji la Kenya, Bi. Betty Maina alisema:
Serikali ya China imeahidi kuimarisha ushirikiano kati ya China na Afrika katika sekta mbalimbali, kuanzia sasa pande mbili zitaimarisha zaidi ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara, na ushirikiano huo utafanyika kwenye msingi mzuri wa kisiasa, uaminifu na sifa nzuri.
Meneja wa kampuni mojawapo ya China iliyowekeza nchini Kenya Bw. Li Jincheng vile vile alimwelezea mwandishi wetu wa habari furaha yake kuhusu Mkutano huo, akisema wameongeza imani kuanzisha shughuli zao barani Afrika, na watajitahidi kutoa mchango kwa ajili ya maendeleo ya nchi za Afrika na kuwanufaisha wananchi wa nchi za Afrika.
Idhaa ya kiswahili 2007-04-25
|