Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-04-25 18:31:51    
Jumuiya ya mtandao wa vijana wa China inayojitahidi kueneza elimu kuhusu afya ya uzazi

cri

Kutokana na mila na desturi za jadi, wakazi wengi wa China hujizuia kuzungumzia mambo yanayohusu afya ya uzazi. Kwa hiyo vijana wengi wa China, hasa wale wanaoishi kwenye sehemu zilizo nyuma kiuchumi, hawawezi kupata ujuzi wa lazima wa mambo yanayohusu afya ya uzazi, hali hiyo imekuwa ni moja ya sababu za kuongezeka kwa idadi ya vijana wanaoambukizwa ugonjwa wa Ukimwi.

Ili kueneza ujuzi na ufahamu kuhusu afya ya uzazi kwa vijana wa China, hivi sasa jumuiya ya mtandao wa vijana wa China inayowashirikisha na kuwahudumia vijana inajitahidi kufanya kazi hiyo kwenye sehemu mbalimbali kote nchini China. Jumuiya hiyo ya mtandao wa vijana wa China ilianzishwa mwaka 2004 kutokana na uungaji mkono wa shirikisho la mpango wa uzazi la China na shirika la idadi ya watu la Umoja wa Mataifa, wanachama wake wote ni vijana kutoka sehemu mbalimbali nchini China. Bw. Li Haimin kutoka mji wa Yangquan mkoani Shanxi ni mwanachama wa mwanzo wa jumuiya hiyo. Alimwambia mwandishi wetu wa habari kuwa, jumuiya hiyo ina malengo dhahiri, yaani kujitahidi kueneza ujuzi na ufahamu kuhusu afya ya uzazi kwa vijana wa China hasa wale wanaoishi kwenye sehemu zilizo nyuma kimaendeleo na kuwasaidia kutatua matatizo yanayowakabili katika maisha yao. Lakini baada ya kazi halisi zilipoanza, wanachama wa jumuiya hiyo wamegundua kuwa kazi hiyo ni ngumu sana. Bw. Li Haimin alisema, mwanzoni alipokuwa akifanya kazi ya kueneza ufahamu wa afya ya uzazi kwenye maskani yake, alikumbwa na kizuizi kikubwa. Bw. Li Haimin alisema:

"kwenye maskani yangu, watu wanajizuia sana kuzungumzia mambo yanayohusu afya ya uzazi. Tuliwahi kujaribu kuanza kazi ya jumuiya hiyo kwenye kiwanda kimoja, kwani vijana wengi wako huko. Lakini tulipozumgumza na maneja wa kiwanda hicho, maneja huyo alikataa mara moja, alipinga kithabiti vijana kuzungumzia afya ya uzazi na mambo yanayohusu afya ya uzazi. Hatimaye kutokana na juhudi zetu za kumshawishi, alikubali kwa shingo upande kuwatuma wawakilishi wawili kushiriki kwenye shughuli zetu na kupewa mafunzo."

Bw. Li Haimin alisema hali kama hiyo zinatokea mara kwa mara. Lakini kutokana na juhudi za pamoja za wanachama wa jumuiya ya mtandao wa vijana wa China, katika muda wa miaka miwili tu, jumuiya hiyo imekuwa inajulikana kwa watu wengi. Vijana wengi wameweza kupewa ujuzi wa afya ya uzazi na kuondoa kiasi matatizo waliyokuwa wakikumbana nao kuhusu afya ya uzazi kwa kushiriki kwenye shughuli zilizoandaliwa na jumuiya hiyo. Bw. Li Haimin alisema, anataka kufanya juhudi kueneza ujuzi kuhusu afya ya uzazi kwa vijana wengi zaidi ili kuwasaidia wapitie kipindi cha ujana bila matatizo hayo.

Msichana Wu Liping anayeishi katika wilaya ya Deqing mkoani Zhejiang pia ni mwanachama wa jumuiya ya mtandao wa vijana ya China, anasoma katika shule ya mafunzo ya kazi ya wilaya hiyo. Alianzisha jumuiya ya "Elimu ya wenzi" inayotoa elimu ya uzazi ya afya katika shule yake, jumuiya hiyo inaeneza ujuzi sahihi kuhusu afya ya uzazi kwa kupitia mawasiliano kati ya vijana wenye rika moja. Wu Liping alimwambia mwandishi wetu wa habari kuwa, utafiti wa kisaikolojia umeonesha kuwa watu hasa vijana, hupenda kupokea ushauri au mapendekezo kutoka kwa marafiki au wenzi wenye rika sawa na kiwango sawa cha elimu. "elimu ya wenzi" ni njia moja ya kueneza elimu kwa vijana kwa kufuata kanuni hiyo.

Wu Liping alipoanza kuandaa jumuiya hiyo, alikumbwa na matatizo mengi. Alisema alipoandaa shughuli ya kwanza ya jumuiya hiyo katika shule yake, watu wachache tu walishiriki kwenye shughuli hiyo. Wakati huo, alikuwa na nia ya kuacha shughuli hizo, lakini hatimaye aliendelea na kazi hiyo kwa juhudi na uvumilivu mkubwa.

Katika miaka miwili iliyopita, Bw Wu Liping aliwaandikisha wanafunzi kumi kadhaa kujiunga na jumuiya hiyo katika shule yake, pia alieneza shughuli hizo katika shule nyingine za huko. Mwenzake Bw Pang Can alikuwa anaendelea kushiriki kwenye shughuli za jumuiya ya "Elimu ya wenzi", alisema amepata manufaa makubwa kutoka kwa shughuli hizo. Pang Can alisema,

"nimefahamu kuwa kipindi cha ujana ni kipindi muhimu katika maisha, hasa kuhusu mambo ya afya ya uzazi."

Kutokana na shughuli na mafunzo mbalimbali, jumuiya ya mtandao wa vijana wa China imekamilika zaidi, mpaka sasa imeanzisha vituo kwenye wilaya zaidi ya 30 kote nchini China na kutoa fursa kwa vijana wengi zaidi kupata elimu kuhusu afya ya uzazi.

Aidha jumuiya hiyo pia imejenga uhusiano mzuri wa ushirikiano na idara husika za serikali na jumuiya mbalimbali za jamii na imepata uungaji mkono kutoka kwa jamii. Miradi ya misaada kwa China ya shirika la mfuko wa idadi ya watu la Umoja wa Mataifa inahusu mpango wa kuunga mkono maendeleo ya jumuiya ya mtandao wa vijana wa China. Naibu mjumbe wa shirika hilo nchini China Bi. Mariam Khan alisema:

"vijana wana akili na wachangamfu, wana uwezo wa kusaidiana, hasa katika mambo ya afya ya uzazi."

Shirikisho la mpango wa uzazi la China ambalo ni jumuiya kubwa kabisa ya kiraia inayoshughulikia mambo ya mpango wa uzazi na afya ya uzazi lilikuwa limeendelea kuunga mkono na kuelekeza kazi za jumuiya ya mtandao wa vijana wa China, katibu mkuu wa shirikisho hilo Bi. Li Yanqu alisema:

"ndiyo kutokana na kushiriki shughuil hizo kwa vijana, miradi yetu itaweza tu kukidhi vizuri zaidi mahitaji ya vijana."