Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-04-27 15:37:44    
Watoto wote wa China watapata fursa sawa ya elimu

cri

Katika miaka ya hivi karibuni serikali ya China imechukua hatua mbalimbali kutatua suala la kuwawezesha watoto wa wakulima wanaofanya kazi za vibarua mijini wapate fursa ya kusoma kwenye shule za mijini, na kazi hiyo imepata maendeleo.

Bwana Wang Jianwei na mke wake kutoka kijiji cha mkoa wa Shangdong, mashariki mwa China wanafanya kazi za vibarua mjini Beijing. Hivi sasa jambo linalowafurahisha ni kwamba tatizo lililowasumbua kwa muda mrefu limetatuliwa, yaani mtoto wao mwenye umri wa miaka 8 hatimaye ameruhusiwa kusoma kwenye shule ya msingi ya sehemu ya Haiting ya Beijing. Bwana Wang Jianwei alisema:

"Tulikuwa na wasiwasi mkubwa. Mtoto wetu tunayeishi naye mjini Beijing amefika umri wa kusoma shuleni, kama angeshindwa kupata nafasi ya kwenda shule, ingekuwa haina maana kwa sisi kufanya kazi za vibarua hapa Beijing. Tunafanya kazi kwa bidii mjini Beijing ili mtoto wetu apate elimu bora zaidi kuliko sisi, ili awe na mustakabali mzuri wa maisha."

Tatizo la watoto wa wakulima wanaofanya kazi za vibarua kupata elimu mijini lilianza kutokea katika miaka ya 80 kutokana na wakulima wengi wa vijijini kumiminikia mijini kutafuta kazi za vibarua. Matokeo ya sensa ya idadi ya watu iliyomalizika mwishoni mwa mwaka 2000 yalionesha kuwa, idadi ya watu wanaohamahama nchini China ilifikia milioni 120, miongoni mwao milioni 20 ni watoto walioishi mijini wanaofuatana na wazazi wao wanaofanya kazi za vibarua mijini, asilimia 9.3 ya watoto hao yaani watoto milioni moja walikosa nafasi za kwenda shule. Watoto hao wakikosa nafasi za kwenda shule wanakuwa watoto wanaorandaranda mitaani, hali hii haisaidii utulivu na maendeleo endelevu ya jamii. Suala hilo limekuwa linafuatiliwa sana na serikali na jumuiya mbalimbali katika jamii, mjumbe wa baraza la mashauriano ya kisiasa la China Bw. Huang Hong alisema:

"Watoto wote wana haki sawa, hivyo watoto wa vijijjini wanaoishi mijini wakifuatana na wazazi wao wangeruhusiwa kwenda shule za mijini."

Ili kutatua suala la elimu ya watoto wa wakulima vibarua, serikali ya China na idara husika zimetunga sera husika ili kuhakikisha haki zao za kusoma shuleni. Watoto wanaofuatana na wazazi wao kuishi mijini watapewa nafasi za kusoma kwenye shule za mijini, na wale wanaobaki vijijini watahakikishwa kupata elimu ipasavyo.

Kutokana na uungaji mkono wa serikali na ufuatiliaji wa jamii, tatizo la elimu kwa watoto wa wakulima vibarua limetatuliwa hatua kwa hatua. Kwenye shule kadhaa za msingi za miji mikubwa, idadi ya wanafunzi ambao ni watoto wa wakulima wanaofanya kazi za vibarua mijini hata imezidi ile ya wanafunzi wakazi wa mijini. Kuhusu suala la watoto wanaobaki vijijini kukosa utunzaji wa wazazi wao, serikali za sehemu mbalimbali zimechukua hatua mbalimbali kutokana na hali halisi za huko. Mjumbe kutoka mkoa wa Shangxi, kaskazini magharibi mwa China Bwana Shi Xinmin alifahamisha:

"Kutokana na kupungua kwa idadi ya watu vijijini, idadi ya wanafunzi shuleni pia inapungua, hivyo zilianzishwa shughuli za kuunganishwa kwa shule. Shule zenye wanafunzi wachache na hali duni ziliondolewa, ambapo mazingira ya shule zilizobaki yameboreshwa, na shule za bweni kwa ajili ya watoto wanaobaki vijijini zimeanzishwa, hivyo wanafunzi wengi wanaweza kusoma shuleni bila wasi wasi."

Bw. Shi Xinmin alisema watoto wa wakulima wanaofanya kazi za vibarua mijini wakipata elimu sawa na wale wa mijini, sifa zao bila shaka zitainuka, na watakuwa na mustakabali mzuri zaidi. Hali hiyo pia itasaidia kupunguza tofauti kati ya wakazi wa mijini na vijijini.

Idhaa ya kiswahili 2007-04-27