Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-04-26 19:25:34    
Umoja wa Ulaya wajaribu kuangalia uwezekano wa kuendelea na mazungumzo kuhusu suala la nyuklia la Iran

cri

Tarehe 25 mjumbe wa Umoja wa Ulaya anayeshughulikia mambo ya nje na sera za usalama Bw. Javier Solana na mjumbe wa kwanza wa mazungumzo wa Iran Bw. Ali Larijani kwa mara ya kwanza walifanya mazungumzo tokea mwezi Februari. Kutokana na hali ya hivi karibuni, pande zote mbili hazikuwa na matumaini yoyote kama mazungumzo hayo yangeweza kuondoa vikwazo vya mazungumzo kuhusu suala la nyuklia la Iran.

Siku hiyo baada ya mazungumzo ya faragha ya muda wa saa sita Bw. Solana aliwaambia waandishi wa habari kwamba walifanya "mazungumzo yenye maana", na Bw Larijani alisema, "mazungumzo ni ya furaha", na pande zote mbili zilieleza kuwa zitaendelea na juhudi za kutatua suala la nyuklia la Iran, na kudokeza kuwa watafanya mazungumzo tena hivi karibuni. Hali ilivyo ni kwamba, kutokana na suala la nyuklia kuzidi kuwa na utatanishi na msimamo wa Iran haubadiliki, Umoja wa Ulaya unakabiliwa na kuchagua sera mpya kutatua suala la nyuklia la Iran kwa njia ya mazungumzo.

Suala la nyuklia la Iran lililodumu kwa miaka mingi limeonesha kuwa Iran imenuia kuendeleza mpango wake wa nyuklia na haitaacha mpango wake kutokana na shinikizo la nje. Kinyume na hali hiyo kila Baraza la Usalama linapoingilia suala hilo, Iran imekuwa ikiharakisha mpango wake, Umoja wa Ulaya unaifahamu sana hali hiyo. Lakini kwa kuwa upande muhimu katika utatuzi wa suala la nyuklia la Iran, Umoja wa Ulaya unaelewa kwamba ni lazima ufuate sera tofauti, ambayo ni tofauti na sera ya nguvu ya Marekani. Kwa hiyo katika miezi kadhaa iliyopita Iran ilipokuwa inazidi kwenda kinyume na matumaini ya jumuiya ya kimataifa, na ilipowateka nyara askari wa jeshi la majini la Uingereza, na Marekani kuongeza tishio katika Ghuba ya Uajemi, Bw. Solana alikuwa anaendelea kuwa na mawasiliano ya simu na Iran, ili awe na mazingira ya kuweza kurudisha tena mazungumo ya uso kwa uso.

Kwa upande mwingine Umoja wa Ulaya unapoonesha sera ya upole pia inaonesha sera ngumu. Kabla ya mazungumzo hayo kati ya Bw Solana na Bw Larijani, tarehe 23 mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya walifanya mkutano mjini Luxembourg waliamua kuichukulia Iran hatua ambazo ni kali zaidi "kuliko azimio la Baraza la Usalama" ikiwa ni pamoja na kuwawekea vikwazo watu na idara zote za Iran zinazojihusisha na mpango wa nyuklia. Vyombo vya habari vinaona kuwa uamuzi huo wa Umoja wa Ulaya unataka kuionya Iran "isifanye itakavyo", na kutaka kuirudisha Iran kwenye meza ya mazungumzo.

Kuhusu suala la nyuklia la Iran, Umoja wa Ulaya na Iran zina msimamo wa namna moja, yaani mazungumzo ni njia bora ya kutatua suala hilo. Na maazimio ya Baraza la Usalama yanapoiwekea vikwazo Iran, pia yanasisitiza juhudi za kidiplomasia. Marekani pia inaonesha kukaribisha mazungumzo hayo kati ya Bw Solana na Bw Larijani. Yote hayo yameonesha kuwa kuna uwezekano wa kuanzisha tena mazungumzo kuhusu suala la nyuklia la Iran.

Kutokana na utatanishi wa suala la nyuklia la Iran, Bw. Solana alionesha tahadhari katika mazungumzo yake na Bw Larijani, na kusema kwamba "hakika mazungumzo yatafanikiwa, au hakika yatashindwa." Watu wanasema, utatuzi wa suala la nyuklia la Iran lina mchakato mrefu, ingawa mazungumzo kati ya Bw Solana na Bw Larijani yalikuwa ni kama majaribio tu, lakini yatasaidia Umoja wa Ulaya kurekebisha sera zake kuhusu utatuzi wa suala la nyuklia la Iran.