Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-04-27 15:05:34    
Pande husika za mgogoro wa Palestina na Israel zajizuia kutokana na hali ya wasiwasi ya hivi sasa

cri

Kundi lenye silaha la Palestina tarehe 26 liliishambulia Israel kwa makombora mawili kutoka sehemu ya Gaza, hii ni siku ya tatu mfululizo kwa kundi lenye silaha la Palestina kurusha makombora kwa Israel baada ya tarehe 24. Wakati huo huo kundi la Jihad lilisema, halitatekeleza ahadi za kundi la Hamas kuhusu kurudi katika makubaliano ya kusimamisha vita usiku wa tarehe 25, na itaendelea kuishambulia Israel, lakini pande nyingine husika bado zimejizuia.

Tarehe 24 mwezi huu, kundi la Ezzedine al-Qassam Brigades lililo chini ya kundi la Hamas lilitoa taarifa likisema, siku hiyo lilirusha makombora zaidi ya 20 ya maroketi na makombora zaidi ya 70 kwa sehemu ya kusini ya Israel. Lilisema kuwa hatua hii ni kwa ajili ya kulipia kisasi kitendo cha kijeshi cha jeshi la Israel cha wiki iliyopita kilichosababisha vifo vya Wapalestina 10. Hii ni mara ya kwanza kwa kundi la Hamas kutangaza kuishambulia Israel baada ya Palestina na Israel kufikia makubaliano ya kusimamisha vita kisehemu mwezi Novemba mwaka jana huko Gaza. Baadaye jeshi la ulinzi la Israel lilithibitisha kuwa, hakukuwa na vifo wala majeruhi katika mashambulizi ya siku hiyo. Lakini Israel inaona kuwa tukio hilo lililotokea katika siku ya uhuru ya Israel ni "uchokozi dhidi ya Israel". Waziri mkuu wa Israel Bw. Ehud Olmert aliitisha mkutano wa dharura wa idara za usalama ili kujadili kujibu mashambulizi hayo. Wakati huohuo jeshi la Israel lilitoa matakwa ya kutekeleza vitendo mara moja kwa mamlaka ya utawala. Hivyo hali ya sehemu ya Gaza ilianza kuwa ya wasiwasi ghafla. Lakini kutokana na kujizuia kwa viongozi wa Palestina na Israel na usuluhishi wa Misri, hali haiendelei kuwa mbaya.

Habari zinasema baada ya kutokea kwa tukio hilo, mwenyekiti wa mamlaka ya utawala wa Palestina Bw. Mahmoud Abbas aliyefanya ziara nchini Italia alisema, anatumai kuwa Israel itajizuia, na kutochukua hatua zitakazofanya hali izidi kuwa mbaya. Na mwishoni Bw. Olmert pia alitoa uamuzi wa kujizuia kuhusu tukio hilo. Aidha, Misri pia kupitia mjumbe wake wa mambo ya usalama huko Gaza Bw. Burhan Hammad ilifanya mazungumzo na wajumbe wa makundi mbalimbali yenye silaha ya Gaza, ili kulinda hali ya utulivu. Tarehe 26 asubuhi, Misri iliiambia Israel kuwa makundi yenye silaha ya Palestina yatatekeleza tena makubaliano ya kusimamisha vita katika sehemu ya Gaza.

Maoni ya raia yanaonesha kuwa, hivi sasa pande husika za Palestina na Israel zinaweza kujizuia kutokana na sababu zifuatazo: kwanza Umoja wa Nchi za Kiarabu ulifikia maoni ya pamoja kuhusu kuanzisha tena Pendekezo la Amani la Nchi za Kiarabu la mwaka 2002, na kuhimiza mazungumzo ya amani kati ya Palestina na Israel kwa msingi wa pendekezo hilo, ili kutimiza amani ya kikanda, na umeunda kikundi cha kazi cha kufanya mazungumzo na Israel; viongozi wa Palestina na Israel wameanzisha utaratibu wa kufanya mazungumzo kila baada ya muda fulani, na kumaliza mazungumzo ya kwanza. Yaani hali inaendelea kuwa nzuri, hivyo pande zote husika zinatumai hali hiyo itaendelea.

Pili kuchukua hatua zinazosababisha mgogoro kupamba moto ni hatari kwa pande hizo mbili. Kwa upande wa Hamas, ikiwa sehemu ya serikali ya muungano wa taifa ya Palestina, Hamas siku zote inafanya juhudi ili kutambuliwa na jumuiya ya kimataifa na mwishoni kuondolewa vikwazo vya uchumi kwa serikali ya Palestina. Kama itafanya mashambulizi makubwa dhidi ya Israel, huenda itafanya nchi zinazojenga uhusiano na serikali mpya ya Palestina zisiiamini serikali ya Palestina.

Kwa upande wa Israel, kwa kuwa haikufanya vizuri katika vita dhidi ya chama cha Hezbollah cha Lebanon mwaka jana, hivyo serikali ya Olmert inakabiliwa na shinikizo kubwa la kisiasa, licha ya hayo ripoti ya kipindi cha katikati ya uchunguzi wa vita itatolewa wiki ijayo, hivyo sasa Bw. Olmert hathubutu kuanzisha vita kirahisi.

Idhaa ya kiswahili 2007-04-27