Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-04-29 18:59:26    
Ziara ya waziri mkuu wa Japan Mashariki ya Kati inalenga kuhakikisha usalama wa nishati wa Japan

cri

Waziri mkuu wa Japan Bw. Shinzo Abe tarehe 28 alifika Riyadh na kuanza ziara nchini Saudi Arabia. Na baadaye pia atazizuru Misri, Kuwait, Qatar na umoja wa falme za kiarabu. Wachambuzi wanasema ziara hiyo ya Bw. Abe katika nchi za Mashariki ya Kati inalenga kuimarisha uhusiano kati ya Japan na nchi zinazozalisha mafuta, kuongeza nguvu ya ushawishi wa Japan katika kanda hiyo, ili kuhakikisha Japan inapata uhakika wa nishati kutoka kwa nchi za Mashariki ya Kati.

Miongoni mwa nchi tano atakazotembelea, nchi nne za Saudi Arabia, Kuwait, Qatar na Falme za kiarabu ni nchi za Ghuba zinazozalisha mafuta na gesi kwa wingi, ambapo asilimia 70 ya nishati inayoingizwa na Japan inatoka kwenye nchi hizo nne. Kwa hiyo lengo la ziara hiyo ya waziri mkuu wa Japan ni kuhakikisha usalama wa nishati.

Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Saudi Arabia, usalama wa nishati na akiba ya nishati ni masuala yaliyojadiliwa sana kwenye mazungumzo kati ya Bw. Abe na mfalme Abdullah wa Saudi Arabia. Katika mwezi Julai mwaka jana, waziri mkuu wa Japan wa wakati huo Bw. Junichiro Koizumi aliwahi kutembelea Mashariki ya Kati. Hivi sasa Bw. Abe anaizuru sehemu hiyo kwa mara nyingine tena ndani ya muda wa mwaka mmoja. Hii inaonesha ni jinsi gani viongozi wa Japan wanavyozingatia suala la usalama wa nishati.

Mbali na hayo lengo lingine muhimu la ziara hiyo ya Bw. Abe ni kuimarisha mawasiliano ya kisiasa, kiuchumi na kibiashara pamoja na kiutamaduni kati ya Japan na nchi zinazozalisha mafuta za kanda ya Mashariki ya Kati, ili kuongeza nguvu ya ushawishi ya Japan katika kanda hiyo. Katika safari hiyo Bw. Abe ameambatana na ujumbe mkubwa unaoundwa na wawakilishi 180 kutoka sekta ya viwanda na biashara ya Japan, ambao watakutana na waziri wa biashara na viwanda wa Saudi Arabia Bw. Hashim Yamani na wanaviwanda na wafanyabiashara wa nchi hiyo, na kufanya majadiliano kuhusu uhusiano wa kiuchumi na kibiashara kati ya nchi hizo mbili, uwekezaji na jinsi ya kupanua wigo wa ushirikiano katika sekta ya nishati. Inasemekana kuwa Japan na Saudi Arabia zina mpango wa kuanzisha mradi wa ushirikiano wa kiuchumi usiohusiana na mafuta nchini Saudi Arabia, ili kuimarisha uhusiano wa kiuchumi na kibiashara kati ya nchi hizo mbili.

Aidha katika ziara hiyo Bw. Abe na viongozi wa nchi husika pia watazungumzia masuala yanayohusu kanda ya Mashariki ya Kati, yakiwemo hali ya Iraq, suala la nyuklia la Iran na mchakato wa amani ya Mashariki ya Kati. Ni dhahiri kwamba hali ya usalama na utulivu wa kanda ya Mashariki ya Kati, inahusiana moja kwa moja na usalama wa nishati wa Japan. Hivi sasa hali ya Iraq inazidi kuwa mbaya, migongano kati ya Iran na nchi za magharibi hususan Marekani katika suala la nyuklia ya Iran inaendelea kuwepo, na migongano hiyo huenda itasababisha vita na kuathiri uzalishaji wa mafuta wa nchi za kanda hiyo, vile vile hali ya mvutano katika mchakato wa amani kati ya Palestina na Israel inatishia usalama na utulivu wa Mashariki ya Kati. Hayo yote kwa hakika yanafuatiliwa sana Japan ambayo inategemea kwa kiasi kikubwa nishati kutoka kwa kanda ya Mashariki ya Kati. Kwa hiyo kufanya mazungumzo na nchi husika ili kutafuta ufumbuzi wa masuala mbalimbali pia ni kazi muhimu ya ziara hiyo ya Bw. Abe.

Idhaa ya Kiswahili 2007-04-29