Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-04-30 16:34:34    
Beijing yaimarisha hifadhi ya majengo ya kale kuchangia mazingira ya "Olimpiki ya utamaduni"

cri

Kutokana na michezo ya Olimpiki ya mwaka 2008 kukaribia siku baada ya siku, maandalizi yamekuwa yakiendelea haraka ikiwa ni pamoja na juhudi za kuimarisha hifadhi ya majengo ya kale mjini Beijing. Katika miaka ya hivi karibuni juhudi hizo zimekuwa kubwa kadiri miaka inavyozidi kwenda. Katika siku za karibuni majengo 18 ya kale yametakiwa kuimarisha mazingira ya hifadhi. Mkuu wa Idara ya Hifadhi ya Mabaki ya Kale mjini Beijing Bw. Kong Fanshi alisema majengo ya kale mjini Beijing yanatakiwa kuchangia kuwepo kwa mazingira bora ya michezo ya Olimpiki.

Mji wa Beijing una historia ya miaka 850, majengo ya kale yapo kila mahali, na kuna majengo hayo zaidi ya 2,000. Kutokana na majengo hayo kuwepo kwa miaka mingi na mengi kati yake yalijengwa kwa mbao na udongo, baadhi yamekuwa yakizidi kuharibika na hayana miundombinu ya zimamoto wala nyaya za kukinga radi, hali ambayo ni hatari kwa usalama. Mwaka 2000 mji wa Beijing ulianzisha mradi wa miaka mitatu wa kukarabati kwa kutenga fedha Yuan milioni 330. Kutokana na fedha hizo zilizotengwa na serikali ya Beijing, fedha nyingine Yuan bilioni tano kutoka wilaya na jamii zimekusanywa. Juhudi kubwa kama hizo hazijawahi kutokea katika historia ya kuhifadhi mabaki ya kale nchini China.

Mwanzoni mwa mwaka huu, Idara ya Hifadhi ya Mabaki ya Kale ya Beijing kwa mara nyingine tena ilikagua usalama wa kila jengo na imethibitisha kuwa majengo 18 muhimu yana hatari hiyo. Kwa mfano, jumba la Huixian lililoko katika sehemu ya mapunziko ya Shi Sha Hai katikati ya mji, ambalo limekuwepo kwa miaka zaidi ya 100 halikukarabatiwa kwa miaka mingi na halina waya wa kukinga radi, wala miundombinu ya zimamoto. Majengo mengine yaliyoonywa pia yako katika hali kama hiyo. Naibu mkuu wa Idara ya Hifadhi ya Mabaki ya Kale ya Beijing Bi. Yu Ping alieleza,

"Hivi sasa tumetoa 'taarifa ya ukarabati unaotakiwa kukamilishwa kwa muda maalumu' kwa idara zinazosimamia majengo hayo, na kuweka katika ratiba yetu ya kazi muhimu katika mwaka 2007, na tutasaidia idara hizo kuandaa mpango wa ukarabati."

Baada ya kukamilisha mradi wenye thamani ya Yuan milioni 330, kuanzia mwaka 2003 Beijing imeanza kutekeleza mpango wa ukarabati wa majengo ya kale kwa ajili ya michezo ya Olimpiki ya utamaduni kwa kutenga fedha Yuan milioni 600. Kwa mujibu wa mpango huo, majengo yote yataondolewa hatari ya usalama kupitia kuyaimarisha, kuweka nyaya za kukinga radi, miundombinu ya zimamoto na mitaro ya kuondoa maji. Mkuu wa Idara ya Hifadhi ya Mabaki ya Kale ya Beijing Bw. Kong Fanshi alisema, hifadhi ya majengo ya kale mjini Beijing italeta mazingira bora ya utamaduni kwa ajili ya michezo ya Olimpiki itakayofanyika mwaka 2008 mjini Beijing. Alisema,

"Kuna umuhimu mkubwa kutatua hatari ya usalama iliyopo kwenye majengo ya kale mjini Beijing. Kwa sababu matatizo yaliyopo kwenye majengo hayo hayalingani na mazingira ya michezo ya Olimpiki, ni lazima yatatuliwe. Majengo ya kale ni sehemu muhimu ya utamaduni wa Beijing, na ni lazima yachangie kuweka mazingira ya utamaduni kwa ajili ya michezo ya Olimpiki."

Kazi ya kuhifadhi majengo ya kale mjini Beijing imepata mafanikio makubwa. Kwa mfano, lango la Yong Din Men ambalo ni lango la kusini la Beijing lilibomolewa mwaka 1954, limejengwa upya na kuyafanya majengo ya kale yaliyopangwa kwenye mstari wa katikati wa Beijing kukamilika, kwani mstari huo umeonesha wazi fikra za mpangilio wa majengo ya Beijing na ni utamaduni mkubwa, mstari huo ni muhimu katika kundi la majengo ya kifalme. Majengo mengine kama kasri la kifalme, pango la watu wa kale wa China lililoko Zhou Kou Dian, hekalu la Tiantan na ukuta mkuu, yote yamekarabatiwa, na nyumba za chini zenye ua wa mraba ambazo ni alama maalumu ya mtindo wa makazi ya Beijing pia zimetengewa sehemu za kuhifadhiwa. Majengo yaliyokarabatiwa ni mengi, mtu akija Beijing kila baada ya mwaka mmoja atashituka kuona mabadiliko hayo. Naibu mkuu wa Idara ya Hifadhi ya Mabaki ya Beijing Bi. Yu Ping alisema, hifadhi ya majengo ya kale sio tu kazi ya serikali, pia inahitaji ushirikiano wa wakazi wote. Alisema,

"Kutokana na maendeleo ya uchumi, watu wamekuwa na uwezo, na serikali imekuwa na fedha kuweza kuhifadhi vizuri zaidi majengo hayo, huu ni upande mmoja. Upande mwingine ni kwamba, watu wamekuwa na mwamko wa kuthamini majengo ya kale, wanaona ni wajibu wao kuhifadhi majengo hayo licha ya serikali. Na mwamko huo unazidi kuwa mkubwa kadiri jamii inavyoendelea." Kwa mfano, bustani ya kifalme Yuan Ming Yuan ambayo imekuwepo kwa miaka 300, iliwahi kuunguzwa mara mbili na wavamizi wa nchi za nje, watu wa leo wanaweza tu kupata tswira ya utukufu wake kutoka magofu yake. Magofu hayo ni muhimu kati ya majengo ya kale yanayohifadhiwa mjini Beijing. Miaka miwili iliyopita magofu hayo yalipofanyiwa ukarabati, wakazi wengi walitoa maoni yao tofauti na hatua za namna ya kuyakarabati, mwishowe hatua zilizopangwa zilibadilishwa ili sura yake ya awali isiharibike.

Lengo la kipindi kifupi katika hifadhi ya majengo ya kale ya Beijing ni kuboresha kimsingi hifadhi ya majengo hayo ili kuchangia mazingira bora ya michezo ya Olimpiki mwaka 2008, na lengo la kipindi kirefu ni kuyafanya majengo hayo yote yawe wazi kwa wananchi.

Idhaa ya kiswahili 2007-04-30