Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-04-30 18:16:12    
Msimamo wa serikali ya China kuhusu suala la Darfur ya Sudan

cri

Siku zote kwenye mgogoro wa Darfur wa Sudan, serikali ya China inatetea kulinda mamlaka ya Sudan na ukamilifu wa ardhi yake, na kutatua suala hilo kwa amani kwa njia ya mazungumzo. Na msingi wa serikali ya China katika kushughulikia suala la Darfur ni kuleta amani, utulivu na ukarabati wa kiuchumi wa Darfur kwa njia ya mazungumzo.

Tangu mgogoro wa Darfur uibuke, China imekuwa ikifanya jitihada kupatanisha pande zinazohusika ili kuondoa maoni tofauti kati yao na kusukuma mbele mazungumzo ya usawa. Juhudi zilizofanywa na China ni pamoja na kuwaalika viongozi wa nchi husika kutembelea China na viongozi wa China pia kuzizuru nchi husika, kutuma mjumbe maalumu wa suala la Darfur, kufanya upatanishi kwa njia za simu na barua na kusaidia kushughulikia suala hilo kwenye Umoja wa Mataifa na mashirika mengine ya kimataifa.

Rais Hu Jintao wa China aliizuru Sudan mwezi Februari mwaka huu. Katika ziara hiyo rais Hu Jintao alieleza msimamo wa kikanuni wa serikali ya China katika suala la Darfur, akisema China inaheshimu mamlaka ya Sudan na ukamilifu wa ardhi yake, inashikilia utatuzi wa amani wa suala hilo kwa njia ya mazungumzo, na inaunga mkono Umoja wa Afrika na Umoja wa Mataifa ufanye kazi ya kusaidia utatuzi wa suala hilo. Zaidi ya hayo China ilitoa misaada kwa sehemu ya Darfur.

Hivi karibuni mjumbe maalumu wa serikali ya China ambaye pia ni msaidizi wa waziri wa mambo ya nje Bw. Zhai Jun alitembelea Sudan, ambapo alibadilishana maoni na upande wa Sudan kuhusu utatuzi wa kisiasa wa suala la Darfur, hususan pendekezo alilotoa Bw. Kofi Annan. China inaona kuwa pendekezo hilo lilitolewa kutokana na hali halisi na linaweza kutekelezwa. China inatumai kuwa Sudan na pande husika zitafanya mazungumzo kuhusu mambo halisi ya pendekezo hilo ili kufikia maoni ya pamoja kwa haraka.

Kwa maoni ya China, kiini cha mgogoro wa Darfur ni suala la maendeleo, shughuli za kulinda amani na mchakato wa kisiasa zinapaswa kwenda sambamba. Sehemu ya Darfur haina maliasili nyingi, na ni sehemu yenye umaskini na hali duni ya kimaendeleo. Kwa hiyo msingi wa utatuzi wa suala la Darfur ni kukarabati na kukuza uchumi wa sehemu hiyo. Pamoja na kuendelea kutoa misaada ya kibinadamu kwa watu wa Darfur, jumuiya ya kimataifa pia inapaswa kuwapa misaada ya maendeleo watu wa huko.

China pia inaona kuwa tishio la nchi za magharibi la kuiwekea vikwazo Sudan halisaidii kuleta utatuzi wa suala, badala yake mazungumzo yanatakiwa kufanyika. Jumuiya ya kimataifa ina wajibu wa kuisaidia Sudan kutatua suala la Darfur, na si kuchochea masuala mapya wala kufanya hali iliyo sasa izidi kuwa mbaya. Tarehe 19 Aprili msemaji wa wizara ya mambo ya nje wa China Bw. Liu Jianchao alipozungumzia suala la Darfur alisema, hivi sasa si wakati unaofaa wa kujadili kuweka vikwazo, badala yake pande zinazohusika zinapaswa kuchukua hatua zinazosaidia utatuzi wa suala hilo na kuhimiza makubaliano yanayohusika yanayoweza kutekelezwa kihalisi mapema iwezekanavyo.

Idhaa ya Kiswahili 2007-04-30