Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-05-01 19:25:39    
Barua 0422

cri

Msikilizaji wetu Lewis Juma Munyasia wa sanduku la posta 2566 Bungoma Kenya ametuletea barua akianza kwa salamu kwa watangazaji na wasikilizaji wa Radio China kimataifa. Anasema ana furaha kemkem kuchukua fursa hii kuishukuru Radio China Kimataifa kwa kuendelea kuwaletea matangazo, na kuwa na uhusiano mwema na wasikilizaji wake, na pia anashukuru sana kwa zawadi nzuri ya kalenda ambayo ameipokea.

Pia anasema ilikuwa ni furaha kubwa kwake kusikia kuwa Bwana Ayub Mutanda Shariff alipewa nafasi na Radio China kimataifa kutoa maelelzo juu ya safari aliyoifanya nchini China, nafasi hii ilimpa picha nzuri jinsi Radio China Kimataifa na watu wa China walivyo marafiki kweli.

Bwana Lewis anasema kwa hakika CRI imeongeza urafiki mkubwa kati ya Afrika na China. CRI pia imekuwa chombo kikubwa cha elimu kwa watu kote duniani, maana imewafanya wasikilizaji wake waelewe vizuri historia na utamaduni wa watu wa China, na hatua ambazo nchi ya China inachukua ili kuzileta maendeleo katika Afrika na nchi nyingine zinazoendelea.

Anasema waliweza kusherehekea siku kuu ya jadi ya mwaka mpya wa China tarehe 18 Februari mwaka huu ambapo Bwana Ayub Mutanda alikuwa mgeni wa heshima, ambaye aliwafahamisha mengi kuhusu Radio China Kimataifa na nchi ya China. Waliweza kufurahia siku hii japo kuwa hawakuwa na vyakula vya kichina. Waliweza pia kutumia fursa hii kufungua maktaba ya vitabu katika kijiji cha Luuya, tarafa ya Nalondo. Alisema ombi lao ni kwamba wangependa kuwa na jarida pamoja na vitabu vya kichina katika maktaba yao.

Anasema vipindi vya Radio China Kimataifa vimempa hamu kubwa mno ya kutamani kuizuri China, ili kujionea mengi na hata angalau kuweza kuonja chakula cha kichina. Anatoa pongezi kwa watangazaji wote wa Radio China Kimataifa, pia hongera kwa vipindi vyenye mafunzo katika Radio China Kimataifa. Ana matumaini kuwa mwaka huu huenda atakuwa mshindi wa chemsha bongo. Angependa kuomba, kipindi cha sanduku la barua jumamosi na jumapili kiongezwe muda. Anaomba tumtumie kadi zaidi za salamu, jarida na zawadi yoyote.

Tunamshukuru sana Bwana Lewis Juma Munyasia kwa barua yake ambayo imetueleza mengi ya kututia moyo, ni matumaini yetu kuwa, ataendelea kusikiliza matangazo yetu, kushiriki kwenye mashindano ya chemsha bongo, kutuletea barua kutoa maoni na mapendekezo, ili kutusaidia kuboresha vipindi vyetu, kudumisha urafiki na kuongeza maelewano kati yetu ni lengo letu daima. Tunafurahi kusikia kuwa ana matumaini makubwa ya kuwa mshindi katika chemsha bongo

Msikilizaji wetu Dominic Nduku Muhoro wa sanduku la posta 397 Kakamega, Kenya ametuletea barua akianza kuwa kutoka salamu kwa wasikilizaji na watangazaji wa Radio China kimataifa, akitarajia kuwa wote ni wazima kwa uwezo wake mwenyezi Mungu. Bw. Dominic anaipongeza serikali na watu wa Jamhuri ya China kwa kufanya sherehe ya mwaka mpya wa jadi wa China, ambayo ilipita miezi michache iliyopita.

Licha ya hilo msikilizaji wetu huyu anasema tarehe 28 mwezi wa kwanza mwaka 2007 alikuwa mwenye furaha sana aliposikia jina lake likitangazwa kupitia matangazo ya idhaa ya Kiswahili ya radio China kimataifa kuwa ni mshindi wa tatu katika shindano la chemsha Bongo la mwaka 2006. Anasema kweli bidii huleta mafanikio bora na ya kupendeza, ushindi huu wa nafasi ya tatu umempa matumaini na imani kuwa, siku moja atapata ushindi wa nafasi maalum au nafasi ya kwanza katika shindano la chemsha bongo la mwaka ambalo litamalizika mwezi April mwaka huu wa 2007.

Bw. Dominic anaendelea kusema anafahamu kuwa si rahisi kuchaguliwa kuwa mshindi kati ya washiriki wengi, lakini usikivu mzuri wa vipindi vya idhaa ya Kiswahili ya Radio China Kimataifa na bidii vinaweza kuchangia mtu kupata ushindi katika nafasi yoyote. Hivyo anawaomba wasikilizaji wenzake wote wazingatie usikivu wa vipindi vyote vya Radio China kimataifa na kushiriki katika chemsha bongo, hapo ndio wanaweza kupata ushindi. Anamalizia barua yake kwa kuwapongeza wafanyakazi wote wa idhaa ya Kiswahili ya Radio Kimataifa kwa kazi za kila siku, na ana ujumbe unaosema: Mtafutaji hachoki mpaka anapopata.

Bw Hamis Hassan wa seminari ya Mtakatifu Carol iliyopo Sengerema, Mwanza Tanzania, kwenye barua aliyotuandikia kwanza ameanza kuwasalimu wasikilizaji wenzake, halafu anatoa pongezi za dhati kwa watangazaji wote wa Radio China Kimataifa, na shukrani za dhati kwa upendo wa wafanyakazi wa Radio China kimataifa waliouonesha kwake. Anasema anapenda sana kusikiliza matangazo ya idhaa ya Kiswahili ya Radio china kimataifa, lakini anaipata katika masafa mafupi, lakini ameshukuru kusikia kuwa juhudi zinafanyika matangazo yaweze kusikika kupitia Radio Tanzania, ili kuweza kukidhi matakwa ya wasikilizaji.

Msikilizaji wetu huyu pia anaomba atumiwe ratiba ya vipindi vya idhaa ya Kiswahili vya CRI ili aweze kufuatilia vizuri matangazo, pia anaomba atumiwe picha ya ukuta mkuu wa China na historia yake. Anauliza je, kama akitaka kutapa matangazo ya yetu kupitia tovuti atatumia tovuti gani? Anaomba ajulishwe ili aweze kuingia katika njia za utandawazi. Pia anasema yeye ni mtazamaji mzuri wa filamu za kichina, ana anamfahamu mcheza filamu maarufu sana duniani Jet Li kutokana na uwezo wake wa kucheza gongfu, anauliza je anaweza kupata picha yake na historia yake? na kwa sasa yuko wapi? Mwisho ameandika neno la kichina ????, anauliza neno hili la kichina maana yake nini?

Tunakushukuru sana Bw Hamisi kwa barua yako yenye maelezo kuhusu unavyopenda kusikiliza matangazo ya Radio China kimataifa. Na tunafurahi sana kusikia kuwa wewe ni mfuatiliaji wa filamu za kichina na hata unataka kujua habari kuhusu Jet Li. Kwa ufupi ni kuwa Jet Li alizaliwa mwaka 1963 hapa Beijing, na sasa yuko Hollywood Marekani akiendelea kuigiza kwenye filamu, na hivi karibuni ametoa filamu mpya. Familia yake iko hapa Beijing, na mara kwa mara huwa anakuja kwao hapa Beijing, yeye ni msanii anayeweza kucheza gongfu, tofauti na wengine ambao wanaigiza tu. Pia tunaona Bw Hamisi aliandika vizuri au tuseme alichora vizuri neno hilo la kichina, lenye maana Tanzania, kweli anastahili kusifiwa kwa kujaribu. Vilevile ametupa ujumbe unaosema: "Hakuna jambo jema kama kuwa na matumaini".

Msikilizaji wetu Pius Bitamale wa S.L.P 3030 Mwanza Tanzania ametuletea barua akitoa salamu nyingi na pole kwa shughuli za kila siku kwa watangazaji wote wa idhaa ya Kiswahili ya radio China Kimataifa, anasema yeye ni mzima wa afya. Lengo la barua yake ni kutuoa shukrani kwa Radio China kimataifa kuweza kurusha matangazo hadi Afrika Mashariki yanayosikika vizuri huko Mwanza Tanzania. Msikilizaji wetu anasema anafurahishwa na habari na vipindi motomoto vilivyopangiliwa vizuri.

Kwa mfano anakumbuka tarehe 7 mwezi wa kwanza mwaka 2007 katika kipindi cha daraja la urafiki kulielezwa mambo mengi sana mazuri, yeye binafsi alifurahishwa sana na aliyosikia na ndio akaamua kuandika barua hii ya pongezi. Na yeye pia ameomba ratiba ya matangazo, kalenda ya mwaka 2007, magazeti na picha za watangazaji wa Radio China Kimataifa pamoja na kadi za salamu.

Idhaa ya kiswahili 2007-05-01