|
Tarehe mosi mwezi Mei mwaka 2003 Rais George W. Bush alitangaza kumalizika kwa vita vya Iraq. Lakini miaka minne tangu Marekani itoe ahadi ya Marekani kuhusu kutimiza amani na usalama nchini Iraq haijatimizwa. Bw. Jamal ni mkazi wa mji wa Baghdad aliyeshuhudia vita vya Iraq. Alipohojiwa na mwandishi wetu wa habari alizungumzia kwanza hali ya usalama mjini Baghdad, ambayo inazidi kuwa mbaya siku hadi siku.
"Hali ya mji wa Baghdad bado ni ya wasiwasi. Hali ya usalama ni mbaya zaidi kuliko hali kabla ya Rais Bush wa Marekani kutangaza kuanzisha vita dhidi ya Iraq. Rais Bush alitangaza kuwa vita vya Iraq vimemalizika, lakini huu si ukweli. Ukweli ni kuwa vita dhidi ya jeshi la Saddam Hussein vimemalizika, lakini kwa wananchi wa Iraq vita ndio vimeanza tu. Kuna vizuizi barabarani hapa na pale, barabara nyingi zimefungwa. Hali mjini Baghdad ni mbaya sana. Sehemu za magharibi na kati za mji huo zimefungwa na jeshi la Marekani na jeshi la serikali ya Iraq, na maelfu ya watu wenye silaha wanafanya mashambulizi."
Migogoro inayotokea mara kwa mara imesababisha vifo na majeruhi ya maelfu ya watu wa kawaida wa Iraq, na zaidi ya watu milioni moja wamekuwa wakimbizi. Maisha ya wananchi wa Iraq hayana uhakikika. Bw. Jamal alisema,
"Mambo mengine pia yamebabadilika kuwa mbaya zaidi, kwa mfano hali ya matibabu ni mbaya, hospitali haziwezi kuendeshwa vizuri, na ni vigumu kupata dawa. Na ni vigumu kupata mahitaji ya kila siku. Ukitaka kuweka petroli kwenye magari, unahitaji kusubiri katika kituo cha mafuta kwa saa 4 hadi 6. Wakati fulani hakuna petroli kwenye vituo vya mafuta, tena bei ni kubwa. Ni vigumu kupata vitu hivyo."
Matatizo yanayowakabili wakazi wa mji wa Baghdad si kama tu yanatokana na hali ya usalama kuwa ya wasiwasi, bali pia yanatokana na operesheni za kijeshi za jeshi la Marekani ambazo haziendani na hali halisi. Jeshi la Marekani limeongeza askari mjini Baghdad na kufanya operesheni za kijeshi mara kwa mara, lakini hali ya usalama bado haijaboreshwa na hivi karibuni lilijaribu kujenga kuta za utenganishaji katika sehemu kadhaa mjini Baghdad ili kutenga sehemu ambazo wanaishi waislamu wa madhehebu ya Suni na sehemu ambazo wanaishi waislamu wa madhehebu ya Shia. Bw. Jamal alisema ingawa Marekani inasisitiza kuwa kujenga kuta hizo ni kwa ajili ya kuhakikisha usalama wa makazi ya watu, lakini kuta hizo haziwezi kuzuia mashambulizi ya watu wenye silaha, bali zimeleta matatizo kwa maisha ya watu na mchakato wa mapatano kati ya madhehebu mbalimbali. Alisema,
"Kuta za utenganishaji zimesababisha watu washindwe kutembea bila ya vizuizi. Ni lazima kuta hizo zijengwe kwa ajili ya kuzuia washambulizi badala ya watu walioshambuliwa. Jeshi la Marekani lilitenga sehemu mbalimbali kwa kuta za utenganishaji, kuna milango kadhaa kwenye kuta hizo ili watu wapite, lakini milango hiyo inafungwa mara kwa mara. Hatuwezi kupita kwenye kuta hizo kwa mabasi, na hata hatuwezi kupita kwa miguu. Kuta za utengenishaji zimeleta matatizo mengi kwa maisha ya watu. Watu hawaoni kuwa kuta hizo zinaweza kufanya kazi, bali wanaona kuwa ni lazima suala la Iraq litatuliwe kwa njia ya kisiasa na kutafuta maafikiano. Kujenga kuta za utenganishaji si utatuzi."
Licha ya hayo, jeshi la Marekani nchini Iraq pia linakabiliwa na hali ya wasiwasi. Tangu vita vya Iraq vianze, idadi ya wanajeshi wa Marekani waliouawa nchini Iraq imekuwa zaidi ya 3300. Mwezi Aprili idadi ya askari wa jeshi la Marekani waliouawa nchini Iraq ilikuwa zaidi ya 100. Bw. Jamal anaona kuwa, majeshi ya nchi za nje yakiondoka Iraq, basi Iraq itapata fursa ya kuwa na maafikiano.
Idhaa ya Kiswahili 2007-05-01
|