Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-05-02 18:02:39    
Rais George Bush akataa mswada wa sheria ya kutenga fedha kwa ajili ya vita

cri

Rais George W. Bush wa Marekani tarehe mosi mwezi Mei alikataa mswada wa sheria ya kutenga fedha kwa ajili ya vita uliowasilishwa na bunge, jambo hilo limeongeza mvutano kati ya Ikulu na bunge la Marekani kuhusu suala la kutenga fedha kwa ajili ya vita.

Baraza la chini na baraza la juu ya bunge la Marekani tarehe 25 na tarehe 26 mwezi Aprili yalipiga kura kupitisha mswada wa sheria ya kutenga fedha za dharura kwa ajili ya vita. Ingawa kwa mujibu wa mswada huo fedha zitakazotengwa kwa ajili ya vita ni nyingi kuliko matarajio ya serikali, lakini mswada huo pia una sharti moja, yaani kuitaka serikali ianze kuondoa jeshi lake kutoka Iraq kabla ya tarehe mosi mwezi Oktoba, na kujaribu kuondoa vikosi vyote nchini Iraq kabla ya tarehe 31 mwezi Machi mwakani.

Kabla ya mswada huo kuwasilishwa kwa Rais Bush, kiongozi wa chama cha Democrat kwenye baraza la juu la bunge la Marekani Bw. Harry Reid na spika na baraza la chini Bibi Nancy Pelosi, mara nyingi walimtaka Rais George Bush asaini mswada huo. Maofisa hao wawili wa chama cha Democrat walisisitiza kuwa mswada huo unaheshimu matumaini ya wananchi wa Marekani kuhusu kusimamisha vita vya Iraq, lakini mara kwa mara Rais Bush alisema atakataa mswada huo.

Baada ya rais Bush kukataa mswada huo, Bush alitoa hotuba kwa nchi nzima kwenye televisheni, akisema, mswada huo unataka jeshi la Marekani liondoke Iraq kabla ya tarehe 1 Oktoba bila kujali hali yoyote nchini humo, hii itaifanya Iraq ijitumbukize katika hali ya vurugu. Alisema, kuweka ratiba ya kuondoa jeshi la Maekani ndiyo kuweka ratiba ya kutangaza siku ya kushindwa kwa jeshi la Marekani.

Baada ya Rais Bush kukataa mswada huo, baraza la juu na baraza la chini yakitaka kupitisha mswada huo, ni lazima yapate zaidi ya theluthi mbili ya tatu ya kura za ndiyo. Lakini chama cha Democrat hakiwezi kupata kura nyingi za ndiyo kwenye baraza la juu na baraza la chini, hivyo ni vigumu kubadilisha uamuzi wa Rais Bush. Katika hali hiyo ni lazima bunge la Marekani litunge mswada mpya wa sheria ya kutenga fedha kwa ajili ya vita, na kufanya majadiliano na kuupigia kura mswada huo, na mwishowe kuwasilisha mswada huo kwa rais.

Wachambuzi wanaona kuwa Chama cha Democrat kitakapotunga mswada mpya kitalegeza msimamo wake, na Rais Bush pia atafikiria kulegeza masharti yake. Hivi sasa chaguo moja la Chama cha Democrat kuhusu mswada mpya ni kuweka malengo kadhaa kwa serikali ya Iraq, kama serikali ya Iraq haiwezi kutimiza malengo hayo, jeshi la Marekani litaondoka kutoka Iraq.

Msimamo wa Chama cha Republic pia una dalili ya kulegeza. Baadhi ya maofisa wa Chama cha Republican wamesema wataunga mkono hatua ya kuiwekea serikali ya Iraq malengo kadhaa.

Wachambuzi wanaona kuwa, pande mbili hazitaki kuwajibika na athari mbaya ya kucheleweshwa kwa fedha za jeshi, hivyo kulegeza masharti bila shaka kutakuwa matokeo ya mwisho. Hivi sasa Rais George Bush anakabiliwa na shinikizo kubwa. Aliwahi kusema kwa sasa fedha kwa ajili ya jeshi la Marekani si nyingi, kama bunge la Marekani halitapitisha mswada wa sheria ya kutenga fedha kwa ajili ya vita, italibidi jeshi la Marekani kupunguza vifaa na utengenezaji wa vifaa, na kushusha kiwango cha maisha ya askari wa jeshi la Marekani ili kubana matumizi ya fedha. Pia inalibidi jeshi la Marekani lipunguze mafunzo ya askari nchini Marekani. Kama jeshi la Marekani halitapata fedha ifikapo katikati ya mwezi Mei, mafunzo ya askari wapya yataathiriwa, na halafu mabadiliko ya askari wa Marekani nchini Iraq na Afghanistan yataathiriwa. Vyombo kadhaa vya habari vinasema mwishowe bunge la Marekani litapitisha mswada wa kutenga fedha kwa ajili ya vita kutokana na matakwa ya serikali.

Idhaa ya Kiswahili 2007-05-02