Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-05-02 19:20:48    
Kabila la wamiao la China

cri
Miao ni moja kati ya makabila madogomadogo ya China. Nchini China kuna wamiao milioni saba na laki nne, ambao wanakaa huko Guizhou, Yunan, Guangxi, Hainan na mikoa mingine zaidi ya 10. Hapo zamani, wamiao walikuwa wanahamahama kukimbilia vita na maisha magumu. Kwa hivyo, wamiao wanaishi katika sehemu mbalimbali nchini kote, na hata wamevuka bahari na kuelekea katika nchi za Ng'ambo. Hivi sasa wamiao zaidi ya laki moja wanaishi nchini Marekani.

    Watu wa kabila la Miao wana lugha yao rasmi pamoja na lahaja tatu. Mwaka 1956, wamiao walibuni lugha ya kuandika kwa msaada wa serikali ya China. Katika imani ya kidini, wamiao wanaabudu maumbile au mizimu ya mababu. Pia wamiao wanafuata dini ya kikristo.

    Kabila la wamiao la China linajulikana kwa aina kemkem za nguo, rangi na mapambo ya nguo. Inasemekana kwamba, kuna zaidi ya mitindo mia moja ya nguo za wanawake wa kabila la Miao. Nguo rasmi wanazovaa wamiao katika sikukuu ni maridadi sana. Mapambo ya kichwani ni mengi sana. Kwa kawaida, wanawake wa kabila la wamiao husokota nywele na kuzifunga kichwani pamoja na pambo la fedha lenye umbo la ng'ombe, kitana na mengineyo. Wanawake wanapenda kuvaa sketi fupi na ndefu. Katika sikukuu au sherehe rasmi, wanawake hujipamba kwa mapambo ya fedha ya aina mbalimbali kama vile hereni, mikufu, bangili na kadhalika.

    Wanaume wa kabila la wamiao wanavaa nguo za kawaida, lakini wanapenda kuvaa vilemba vyenye rangi nyeusi.

    Wanawake wa kabila la Miao ni hodari sana wa kufuma nguo, na kushona nguo zao. Kazi ya tarizi na utiaji rangi wa vitambaa na mapambo ya fedha vinavuma sana kwa umaarufu wake na vina historia ndefu zaidi ya miaka elfu moja. Vitu hivyo vya kisanaa vinauzwa katika nchi nyingine nyingi.

    Chakula kikuu cha wamiao ni wali, pia wanapenda kula mahindi, pamoja na viazi vitamu. Siku hizi aina za vyakula zimeongezeka zaidi kadiri maisha yao yanavyoinuka.

    Wamiao wengi wanakaa kwenye sehemu za milima, kwa hivyo nyumba zao ni za mbao, lakini zinatofautiana na zile za sehemu nyingine. Nyumba za mbao za wamiao hujengwa kwenye miteremko. Mihimili ya nyumba hizo huwa mirefu sana na nyumba za wamiao huwa za ghorofa, lakini chini huwa wazi ambako wanaweka mifugo au wanaweka vitu mbalimbali na watu wanakaa ghorofa ya juu.

    Wamiao ni hodari sana kuimba nyimbo. Wamiao wanapopokea au kuwaaga wageni wanaimba nyimbo kwa kuelezea hisia zao; akina mama wanapokutana husimuliana mambo ya nyumbani kwa nyimbo; wasichana na wavulana wanapokutana huimba nyimbo za mapenzi ili kufahamiana zaidi. Nyimbo za wamiao ni za kuvutia sana.

    Lushen ni aina moja ya kinanda kinachotumiwa na wamiao. Kinanda hicho cha Lushen hutengenezwa kwa mianzi. Lushen hutofautiana kwa urefu. Lushen ndefu hufikia mita kadha; na zile fupifupi huwa na sentimita 30. Wamiao wanapenda sana kupiga kinanda cha Lushen. Kwenye ngoma za wamiao huwezi kukosa kusikia sauti nyororo ya Lushen. Wamiao pia wanapenda sana ngoma. Ngoma maarufu sana ni ngoma ya Lushen ambayo yenye historia zaidi ya miaka elfu moja. Katika sherehe za sikukuu, makumi hata mamia ya wanaume kwa wanawake, wavulana kwa wasichana wanajikusanya katika duara wakisakata dansi wakiongozana na wapigaji Lushen. Ngoma hiyo ya Lushen inajulikana kama "Disko la mashariki". Ngoma ya Lushen huchezwa wakati wa sikukuu kwenye uwanja mkubwa.

    Zaidi ya hayo, wamiao wana sikukuu kadha wa kadha za kijadi kama vile sikukuu ya majahazi yenye umbo la joka kubwa, sikukuu ya mavuno, sikukuu ya tarehe nane Aprili na kadhalika; na sikukuu kubwa kabisa ni sikukuu ya mwaka mpya wa wamiao. Sikukuu hiyo husherehekewa na wamiao baada ya kupata mavuno mazuri na kutakiana maisha bora zaidi kwa mwaka ujao. Asubuhi ya siku hiyo, wamiao hupanga vyakula vitamu kwa kutambikia mizimu ya mababu na pia hunyunyizia kidogo pombe kwenye pua za ng'ombe kwa kuwashukuru kazi zao za mwaka mzima. Wasichana huvaa nguo maridadi na kujipamba kwa mapambo ya kuvutia. Usiku huandaliwa sherehe kubwa katika kila kijiji huku wamiao wakiimba nyimbo na kucheza dansi kwa furaha.

Idhaa ya kiswahili 2007-05-02