Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-05-04 18:00:44    
Mabasi ya abiria yaliyotengenezwa na China yakaribishwa na Zimbabwe

cri

Katika siku za karibuni Zimbabwe ilitangaza kuwa mwaka huu itanunua mabasi ya abiria 245 kutoka China, yakiwemo mabasi kadhaa ya kiwango cha juu yatakayotumika kwa safari ndefu. Hayo ni mabasi mengi zaidi kuliko yale ya mwaka 2005, wakati China ilipoiuzia Zimbabwe mabasi 50 ya abiria.

Mabasi hayo yatakayonunuliwa na Zimbabwe, ni sehemu moja ya makubaliano kati ya kampuni ya uchukuzi wa abiria ya pamoja ya Zimbabwe?na kampuni ya magari ya kwanza ya China yaliyosainiwa katika kipindi cha ziara ya rais Robert Mugabe wa Zimbabwe nchini China mwaka 2005. Kutokana na makubaliano hayo, China itaiuzia Zimbabwe mabasi 300 ya abiria na misingi ya mabasi 100. Mwezi Aprili mwaka 2005, mabasi 50 mapya ya abiria yalisafirishwa kwa meli kwenda mjini Harare, Zimbabwe kutoka mjini Shanghai. Magari hayo yenye rangi ya kibuluu yalisifiwa na wakazi wa huko kuwa ni "mandhari maalumu mjini Harare". Mkazi mmoja wa Harare alisema, anajisikia vizuri sana kwenda na kutoka kazini kwa kupanda mabasi yaliyotengenezwa China, anaona kuwa mabasi hayo ni mazuri sana.

Hadi sasa kampuni ya uchukuzi wa abiria ya pamoja ya Zimbabwe imetumia mabasi 118 ya ngazi ya juu yaliyotengenezwa na kampuni ya magari ya kwanza ya China. Kati ya hayo kuna mabasi kumi makubwa zaidi yanayotumika katika safari za kwenda Beira nchini Msumbiji, Johannesburg nchini Afrika ya Kusini, na Lilongwe nchini Malawi. Habari nyingine zinasema kampuni ya Dazhong ya mkoani Jiangsu, China na kampuni nyingine ya mabasi ya abiria ya Zimbabwe zilisaini makubaliano ya ushirikiano wa muda mrefu, kutokana na makubaliano hayo, kwanza kampuni ya Dazhong itaiuzia Zimbabwe mabasi 35 ya abiria ya ngazi ya juu yenye urefu wa mita 12.

Zimbabwe ni nchi ambayo haipakani na bahari, eneo lake ni kilomita za mraba laki 3.9, na usafiri wa reli haujaenezwa sana. Lakini ina barabara za ngazi mbalimbali zenye urefu wa kilomita elfu 90, hivyo magari ni njia muhimu sana kwa uchukuzi. Idadi ya mabasi yanayohitajika kwa ajili ya matumizi ya nchi hiyo ni kiasi cha elfu 40, na kwa kuwa Zimbabwe haina uwezo wa kutengeneza mabasi, hivyo mabasi yanayotumika nchini humo yanaagizwa kutoka nchi za nje.

Zamani Zimbabwe ilinunua mabasi kutoka nchi za Afrika ya Kusini na Kenya, lakini bei ya mabasi yaliyonunuliwa kutoka kwenye nchi hizo ilikuwa ni kubwa sana. Meneja mkuu wa kampuni ya usafiri ya Zimbabwe alisema, Zimbabwe si nchi tajiri, ni vigumu sana kwake kumudu gharama za uendeshaji wa usafiri, na bei ya mabasi ya China ni nusu ya ile ya mabasi ya Afrika ya Kusini, hivyo mabasi yaliyotengenezwa na China yana uwezo mkubwa wa ushindani nchini Zimbabwe.

Kampuni iliyonunua mabasi kutoka kampuni ya Dazhong ya China ilieleza kuwa, mabasi ya China ni mazuri sana, pia yanakidhi matakwa ya hifadhi ya mazingira, bei ni rahisi na sifa yake kwenye upande wa usalama pia ulivutia macho. Kampuni hiyo inaona kuwa mabasi ya China yatainua kiwango chake cha safari za abiria, na mabasi hayo yanafurahisha.

Sababu nyingine inayofanya mabasi ya China yakaribishwe barani Afrika ni huduma nzuri. Mkurugenzi wa kituo cha huduma cha kampuni ya magari ya kwanza ya China nchini Zimbabwe Bw. Bai Shengcheng alisema, kampuni yao ina wahandisi wanne wa kudumu wanaohudumia mabasi yote yaliyouzwa nchi humo. Tangu mara ya kwanza mabasi hayo ya abiria yalipowasili nchini Zimbabwe, wahandisi hao wanne waliishi pamoja na wafanyakazi wa Zimbabwe, na kutatua matatizo ya kiufundi. Kama mabasi ya abiria yaliyotengenezwa na kampuni hiyo yakiharibika, vipuri vinavyotumika kwenye mabasi hayo vinatolewa na kampuni hiyo bila malipo.

Zimbabwe ni nchi ya kwanza barani Afrika iliyonunua ndege kutoka China, pia ni nchi ya kwanza barani Afrika iliyonunua mabasi ya abiria kwa wingi kutoka China. Wachambuzi wanaona kuwa, uhusiano wa ushirikiano kati ya China na Afrika katika sekta za uchumi na biashara unazidi kuimarika siku hadi siku, ushirikiano kati ya pande hizo mbili katika sekta ya mabasi ya abiria pia utapata mafaniko makubwa. Serikali ya China inapaswa kutunga sheria husika mapema, ili kuboresha zaidi uuzaji wa mabasi ya abiria kwa nchi za nje.

Habari nyingine zinasema vyombo vya habari vya Zimbabwe hivi karibuni vilitoa makala vikiitaka serikali ya Zimbabwe ivutie vitega uchumi zaidi kutoka China, kwa msingi wa mkutano wa wakuu wa baraza la ushirikiano kati ya China na Afrika, ili kutatua matatizo ya kiuchumi yaliyosababishwa na vikwazo vya kiuchumi kutoka magharibi na maafa ya kimaumbile. Makala hizo zinasema Zimbabwe inahitaji uwekezaji kutoka China, kwa sababu China ni moja ya nchi zinazoendelea haraka duniani tu, tana kwa sababu uwekezaji kutoka China unaambatana na kanuni za usawa na kunufaishana, kutoingiliana mambo ya ndani, na kuheshimiana mamlaka ya nchi. Makala hizo zimesema China inawekeza barani Afrika bila masharti yoyote, hivyo serikali ya Zimbabwe inapaswa kutunga sera husika ili kuhimiza kuvuta uwekezaji kutoka China.

Vyombo vya habari vya Zimbabwe pia vimesema, Zimbabwe ina matumaini kuwa China inaweza kutuma wataalamu nchini Zimbabwe kufundisha teknolojia na maarifa ya usimamizi, ili kuwawezesha wazimbabwe waelewe namna China inavyoendeleza uchumi na kushughulikia mambo ya taifa.

Idhaa ya kiswahili 2007-05-04