Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-05-03 20:09:40    
Wanafunzi kutoka nchi za nje wafurahia kusoma na kuishi huko Shenzhen

cri

Mliyosikia ni rekodi ya watu wakisoma shairi kwa lugha ya Kichina sanifu. Lakini watu hao si Wachina, bali ni wanafunzi wa Korea ya Kusini wanaosoma huko Shenzhen, mji wa kusini mwa China. Hivi sasa wanafunzi wengi kutoka nchi za nje wanasoma kwenye vyuo vikuu mbalimbali vilivyopo mjini humo.

Badhe Utsab ni kijana kutoka Nepal, sasa anajifunza lugha ya Kichina kwenye chuo kikuu cha Shenzhen. Kijana huyo alimwambia mwandishi wetu wa habari kuwa, anaupenda mji wa Shenzhen japokuwa alikuwa amekuja kwenye mji huo muda si mrefu uliopita. Alisema"Nimeishi hapa Shenzhen kwa miezi 10 tu, lakini sasa nimepata marafiki Wachina. Naona Wachina ni wakarimu na wanafurahi kuwasaidia wengine. Hivi sasa bado sijaweza kuongea Kichina sanifu, nakabiliwa na shida fulani kimaisha na kimasomo, ni marafiki zangu Wachina ndio walionisaidia sana, jambo ambalo linanitia moyo sana na kunifanya nione kuwa Shenzhen ni kama maskani yangu."

Mji wa Shenzhen uliopo pwani ya kusini ya China ni moja kati ya maeneo ya China yaliyotangulia kufungua mlango mwishoni mwa miaka ya 70 ya karne iliyopita. Katika miaka karibu 30 iliyopita, mji huo ulipata maendeleo makubwa ya kiuchumi na kijamii. Hivi sasa kuna vyuo vikuu 10 huko Shenzhen, na vimewavutia wanafunzi wa kigeni zaidi ya 500 kutoka nchi zaidi ya 40. Vyuo vikuu hivyo vinatumia mbinu mbalimbali za kuwafundisha wanafunzi. Kwa mfano kwenye chuo kikuu cha Shenzhen, wanafunzi wa kigeni wanaweza kuchagua masomo kuhusu utamaduni wa China, kama vile maandishi ya Kichina, picha za Kichina, nyimbo za Kichina na mchezo wa Taiji ambayo ni aina ya Wushu ya China.

Zaidi ya hayo wanafunzi wa kigeni wameandaliwa hali nzuri ya maisha. Mwalimu Liang Qiuru anayefundisha wanafunzi wa shahada ya pili katika chuo kikuu cha Shenzhen chini ya chuo kikuu cha viwanda cha Harbin alisema "Tunawapatia huduma nzuri wanafunzi wa kigeni. Kwa mfano kwenye vyumba wanavyoishi wanafunzi wa kigeni, kuna majokofu, viyoyozi, majiko na misalani. Nyumba hizo zina zana bora zaidi kuliko nyumba wanazoishi wanafunzi Wachina."

Wanafunzi wa kigeni wanaosoma huko Shenzhen wanatoka nchi mbalimbali, wana dini tofauti pamoja na mila na desturi tofauti. Vyuo vikuu mbalimbali vya Shenzhen vimeandaa mazingira mazuri ya kusoma na kuishi kwa kufuata kanuni ya kuheshimu utamaduni, mila na dini za nchi nyingine. Kila zinapowadia sikukuu za dini ya kiislamu, vyuo vikuu hivyo vinawaandalia tafrija wanafunzi waislamu ili washerehekee sikukuu za kidini kwa pamoja. Na wakati wa sikukuu za Kichina, walimu na wanafunzi wa China pia wanasherehekea na wanafunzi wa kigeni.

Kijana Waqas Anwar anatoka Pakistan, sasa anasomea mchepuo wa sayansi na teknolojia zinazohusu kompyuta katika chuo kikuu kimoja huko Shenzhen. Kijana huyo alisema  "Walimu wa chuo kikuu chetu wanaoshughulikia mambo ya wanafunzi wa kigeni wanazingatia sana mila na desturi za wanafunzi wa Pakistan. Kila mwaka katika sikukuu ya Idi el-Fitri, wanatuandalia tafrija ya kuisherehekea sikukuu hiyo. Mbali na hayo, walimu pia wanafuatilia mahitaji ya wanafunzi wa nchi nyingine. Kwa mfano tafrija ya Krismas inafanyika kila mwaka. Zaidi ya hayo kuna tafrija nyingine za kuwakaribisha wanafunzi wapya na kuwaaga wanafunzi wahitimu, pamoja na tafrija zinazofanyika wakati wa sikukuu za jadi za China, kama vile sikukuu ya mwezi na mwaka mpya wa jadi wa China. Tunavutiwa na maisha ya hapa, mimi sijawahi kusikia upweke wa kuishi hapa katika nchi ya kigeni."

Ili kuwasaidia wanafunzi wa kigeni kutokuwa na matatizo na kupunguza upweke, walimu na wanafunzi wa China wanafanya jitihada kubwa kuwasaidia. Mwalimu Chen Yanfei anayeshughulikia mambo ya wanafunzi wa kigeni kwenye chuo kikuu kimoja huko Shenzhen, alielezea tukio moja, akisema "Kuna mwanafunzi mmoja kutoka Pakistan, mke wake aliumwa na kulazwa hospitali. Wakati huo ilikuwa ni likizo ya siku za baridi. Tulipopata habari hiyo, tuliandaa zawadi tukaenda hospitali kumtembelea mke wake na kumpa pole. Mwanafunzi huyo aliguswa sana moyo wake na tukio hilo, alisema hakutarajia kama wafanyakazi wa chuo kikuu wangekwenda hospitali kumtembelea mke wake."

 

Katika siku za kusherehekea mwaka mpya mwaka huu, vyuo vikuu kadhaa huko Shenzhen vilishirikiana kuandaa tafrija ya mwaka mpya kwa ajili ya wanafunzi wa kigeni. Tafrija hiyo iliwapa wanafunzi hao nafasi ya kuonesha uhodari wao na kufanya mawasiliano. Wanafunzi wa kigeni waliohudhuria tafrija hiyo walifanya maonesho ya michezo ya kisanaa kwa kutumia lugha ya Kichina. Na kabla ya kumalizika kwa tafrija hiyo, wakiwa pamoja waliimba wimbo mmoja wa Kichina uitwao marafiki, ili kuonesha urafiki mkubwa kwa walimu na wanafunzi wa China. Sasa wasikilizaji wapendwa, tunawaburudisha kwa wimbo huo uitwao marafiki ulioimbwa na wanafunzi wa kigeni kwa lugha ya Kichina.