Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-05-07 19:01:12    
Kwanini Bwana Sarkozy ameweza kupata ushindi kwenye uchaguzi mkuu nchini Ufaransa?

cri

Katika duru la pili la upigaji kura wa uchaguzi wa rais uliofanyika nchini Ufaransa, mgombea wa rais wa chama cha muungano wa harakati za umma cha mrengo wa kulia cha Ufaransa Bw Nicolas Sarkozy alimshinda mgombea mwingine Bibi Segolene Royal wa chama cha jamii cha mrengo wa kushoto cha Ufaransa, na kuchaguliwa kuwa rais mpya wa Ufaransa, ushindi wake unatokana na sababu mbalimbali.

Katika duru la kwanza la upigaji kura, kura alizopata Bwana Sarkozy zilizidi kwa asilimia 6 tu zile alizopata Segolene Royal, ambapo wagombea hao wawili wote hawakupata kura zaidi ya nusu, hivyo uchaguzi mkuu wa Ufaransa ulilazimika kuingia katika duru la pili la upigaji kura. Kabla ya kuanza kwa duru la pili la upigaji kura, Bwana Sarkozy alifanya chini juu kuwashawishi wapiga kura kumwunga mkono, na juhudi zake zilikuwa na mafanikio.

Zaidi ya hayo Bwana Sarkozy ni ofisa mwenye uzoefu mkubwa katika mambo ya utawala. Alipokuwa na umri wa miaka 22 alichaguliwa kuwa mbunge wa mji wa Neuilly huko Paris. Baadaye alichaguliwa kuwa meya wa Neuilly, mbunge wa bunge la serikali ya mtaa, waziri wa bajeti wa serikali ya Ufaransa na msemaji wa serikali, waziri wa mambo ya ndani, waziri wa uchumi, fedha na viwanda na kadhalika. Katika miaka mingi iliyopita, amepata uzoefu mwingi katika kazi za nyadhifa mbalimbali muhimu. Bibi Segolene Royal akilinganishwa na Bw Sarkozy anaonekana kuwa uzoefu wake katika mambo ya utawala si mkubwa, na siku zote Bibi Royal alishughulikia mambo yanayohusu mazingira, familia, watoto na walemavu, hayo yote yako mbali na masuala yanayofutiliwa zaidi na wafaransa wengi kuhusu nafasi za ajira, mambo ya uchumi na usalama wa jamii.

Aidha Bwana Sarkozy anaonekana kuwa na afya nzuri na ari kubwa, anaweza kutoa maamuzi bila kusitasita, na mafanikio aliyopata katika kazi zake yalisifiwa na watu, hivyo ameaminiwa na wapiga kura wengi zaidi. Mwaka 2002 baada ya kushika wadhifa wa waziri wa mikoa huru, usalama wa nchini na mambo ya ndani wa Ufaransa, Bwana Sarkozy alichukua hatua nyingi madhubuti kuboresha hali ya usalama wa jamii. Kwanza alishughulikia mawasiliano barabarani, ambapo watu walioendesha magari kwa mwendo wa kasi kwa kupita kiasi, walioendesha magari wakiwa wamelewa, au waliokimbia baada ya kusababisha ajali wote waliadhibiwa vikali, ndipo matukio ya ajali barabarani yalipungua kwa kiasi kikubwa; pia aliwapanga upya polisi na askari kote nchini, hatua hiyo ilizuia kwa ufanisi shughuli mbalimbali za uhalifu; tatu aliongoza kutunga sheria mpya ya wahamiaji na kupiga vita vikali uhamiaji haramu; nne aliimarisha kazi ya kukinga na kupambana na magaidi. Bwana Sarkozy alisifiwa na kuaminiwa na wafaransa wengi kwa sura yake ya kufanya mageuzi kwa hatua imara, wafaransa hao wanaona kuwa yeye anaweza kuiongoza Ufaransa kufanya mageuzi ya lazima.

Zaidi ya hayo ilani ya uchaguzi wa rais ya Sarkozy pia inalingana na matakwa ya wafaransa wengi. Hivi sasa nchini Ufaransa kuna ukosefu mkubwa wa ajira, na bei za vitu zinapanda juu, katika hali hiyo halisi, kuongeza nafasi za ajira na kuongeza nguvu ya kununua bidhaa ya wananchi kumekuwa masuala yanayofuatiliwa zaidi na wapiga kura. Juu ya hayo, Bwana Sarkozy alitoa mwito wa "Kazi zaidi kwa muda mrefu zaidi", akiwataka wananchi wasifuate utaratibu wa kazi wa saa 35, bali wafanye kazi zaidi kwa muda mrefu zaidi ili kupata mapato mengi zaidi, tena amependekeza kupunguza kodi ili kuhimiza uuzaji kwenye soko, na kuvumbua nafasi za ajira. Mapendekezo hayo yamewafurahisha watu wa kawaida wa Ufaransa na waendeshaji wa viwanda na makampuni wa nchi hiyo. Lakini Bibi royal alichelewa kutoa mwongozo wa utawala, tena aliathiriwa na nguvu ya mrengo wa kushoto katika kupunguza matumizi ya umma ya serikali na hatua kuhusu nguvu kazi huria, hivyo alionekana kuwa na udhaifu wakati wa kushindana na Bwana Sarkozy. Kuhusu uwezo wa rais katika mambo ya kidiplomasia, Bwana Sarkozy alionekana kuwa na uzoefu mkubwa na kumshinda zaidi Bibi Royal.

Ingawa Bwana Sarkozy amepata ushindi, lakini hakika kuna vipengele vingi katika njia yake ya kushika madaraka ya urais, na jukumu linalomkabili ni kubwa sana. Uchumi wa Ufaransa uliodidimia katika miaka ya hivi karibuni, si rahisi kuweza kuuboresha kwa muda mfupi tu.