Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-05-08 18:29:36    
Mabadiliko mapya yaliyotokea kwenye maonesho ya 101 ya kimataifa ya bidhaa zinazosafirishwa nje na zinazoagizwa kutoka nje ya China

cri

Maonesho ya kimataifa ya bidhaa zinazosafirishwa nje ya China ni maonesho maarufu ya kimataifa ya bidhaa. Maonesho hayo yanafanyika katika majira ya mchipuko na majira ya mpukutiko kila mwaka mjini Guangzhou. Mpaka sasa yamefanyika kwa miaka 50. Maonesho ya 101 yaliyofanyika katika majira ya mchipuko mwaka huu yakilinganishwa na maonesho 100 yaliyopita, yana mabadiliko mawili makubwa. Kwanza jina la maonesho hayo imebadilika na kuwa maonesho ya kimataifa ya bidhaa zinazosafirishwa nje na zinazoagizwa kutoka nje ya China; pili eneo maalumu la maonesho ya bidhaa zinazotaka kuingia kwenye soko la China liliwekwa kwenye maonesho hayo kwa mara ya kwanza. Wachambuzi wamesema mabadiliko hayo ni hatua iliyochukuliwa na China ili kupunguza urari wa biashara kati ya China na nchi za nje

Kwenye eneo la maonesho ya bidhaa zinazotaka kuingia kwenye soko la China, Bibi Jan Wilson kutoka jimbo la Washington la Marekani aliwaelezea wanunuzi wa China kuhusu madawa yanayozalishwa na kampuni yake.

Bibi. Wilson alisema kampuni yake iliamua kushiriki kwenye maonesho hayo kwa kuwa China ina soko kubwa la bidhaa akisema:

"Hayo ni maonesho makubwa ya kimataifa, na yatakuwa makubwa zaidi katika siku zijazo. Tunaweza kukutana na wafanyabiashara kutoka sehemu mbalimbali duniani ambao wanaweza kuwa wateja wa bidhaa za kampuni yetu. Tutumai kuwa tutakutana na wafanyabiashara ambao wanapenda kushirikiana nasi, na kununua bidhaa za kampuni yetu kila baada ya muda fulani."

Bibi Wilson alimwambia mwandishi wa habari kuwa makampuni ya Marekani hasa makampuni madogo na ya kati yanatumai kuingia kwenye soko la China, lakini hayajapata njia nzuri ya kuingia kwenye soko la China. Maonesho hayo maarufu yameyapatia makampuni hayo fursa ya kuingia kwenye soko la China, pia yatasaidia kuboresha hali ya kutokuwepo kwa uwiano wa biashara kati ya China na Marekani.

Mwaka huu eneo maalumu la maonesho ya bidhaa zinazotaka kuingia kwenye soko la China liliwekwa kwenye maonesho hayo, na wafanyabiashara wengi wa nchi za nje akiwemo Bibi Wilson walikuja China kushiriki kwenye maonesho hayo, ili kutafuta fursa ya kuingia kwenye soko la China.

Msemaji wa maonesho hayo Bw. Xu Bing alipozungumzia maeneo ya maonesho hayo alisema,

"Maeneo ya maonesho ni ya aina mbili, yaani maeneo ya maonesho ya bidhaa kwa matumizi ya viwandani na kwa matumizi ya nyumbani. Kuna maeneo 9 ya maonesho yakiwemo maeneo ya maonesho ya mashine, magari madogo na vipuri, vifaa vya umeme, vyombo vya metali, vifaa vya ujenzi, bidhaa za matumizi ya maisha ya kila siku, mapambo, vito, chakula na mazao ya kilimo. Makampuni 314 kutoka nchi na sehemu 36 yakiwemo makampuni 7 kutoka nchi 6 zilizo nyuma zaidi kiuchumi duniani yameshiriki kwenye maonesho hayo."

Ofisi ya biashara ya serikali ya jimbo la Washington la Marekani nchini China imeongoza makampuni 8 ya jimbo hilo kushiriki kwenye maonesho hayo. Mkuu wa ofisi hiyo Bw. Cheng Yandong alisema, makampuni mengi yaliyoshiriki kwenye maonesho hayo ni makampuni madogo na ya kati, ya sekta mbalimbali zikiwemo dawa na software. Jimbo hilo linatazamiwa kuongoza makampuni mengi zaidi kushiriki kwenye maonesho yajayo, na bidhaa zitakazooneshwa kwenye maonesho hayo zitakuwa za kisasa zaidi. Alisema:

"Kwenye maonesho hayo makampuni mengi ya Marekani ni madogo na ya kati, makampuni makubwa yanasubiri matokeo ya maonesho hayo ili kuamua kama yatashiriki kwenye maonesho yajayo au la."

Wafanyabiashara wa China wana hamu kubwa kuhusu eneo la maonesho ya bidhaa zinazotaka kuingia kwenye soko la China. Mfanyabiashara wa mkoa wa Henan Bw. Yang Ruijun alisema kampuni yake haikupata njia nzuri ya kuagiza bidhaa kutoka nchi za nje. Maonesho hayo yamewapatia fursa nyingi za kujadiliana na makampuni ya nchi za nje, na wanafikiria kuongeza biashara na nje kutokana na kuboreshwa kwa njia ya kuagiza bidhaa kutoka nchi za nje. Alisema:

"Kuanzishwa kwa eneo la maonesho ya bidhaa zinazotaka kuingia kwenye soko la China ni jambo zuri sana. Zamani kampuni yetu iliagiza bidhaa kupitia mtandao wa Internet, sasa tunaweza kuona bidhaa moja kwa moja, Natumai kwenye maonesho yajayo kutakuwa na eneo kubwa zaidi la bidhaa zinazotaka kuingia kwenye soko la China, na wakati huo hatuna budi kwenda nchi za nje ili kununua bidhaa."

Wachambuzi wanaona kuwa, hatua hiyo itasaidia makampuni mengi ya nchi za nje kulifahamu soko la China, kusukuma mbele ongezeko la bidhaa zinazoagiza kutoka nchi za nje, na kuboresha hali ya kutokuwepo kwa uwiano wa biashara kati ya China na nchi za nje. Mwaka 2006 urari wa biashara kati ya China na nchi za nje ulikuwa dola za kimarekani bilioni 177.5 ambao ulikuwa mkubwa zaidi katika historia. Kutokana na hali hiyo China inakabiliwa na shinikizo kubwa kutoka kwa nchi za Ulaya na Marekani.

Ili kupunguza urari wa biashara, serikali ya China imechukua hatua nyingi zikiwemo kurekebisha miundo ya bidhaa zinazouzwa katika nchi za nje na kuongeza uagizaji wa bidhaa za teknolojia ya juu. Wizara ya biashara ya China imetunga mpango kuwa hadi kufikia mwaka 2010 thamani ya uagizaji wa bidhaa kutoka nchi za nje na thamani ya mauzo ya bidhaa za China katika nchi za nje iwe na uwiano. Mwezi Machi mwaka huu thamani ya urari wa biashara kati ya China na nchi za nje ulipungua kwa kiasi kikubwa, ambayo ilikuwa ni asilimia 28.9 ya thamani ya mwezi Februari.

Naibu waziri wa biashara wa China Bw. Gao Hucheng alisema, "Serikali ya China imebadilisha maonesho ya kimataifa ya bidhaa zinazosafirishwa nje ya China ambayo yalilenga kusukuma mbele mauzo ya bidhaa za China katika nchi za nje kuwa maonesho ya kimataifa ya bidhaa zinazosafirishwa nje na zinazoagizwa kutoka nje ya China ambayo yanasukuma mbele maendeleo ya biashara yenye uwiano. Hii imeonesha udhati na juhudi za serikali ya China katika kuboresha uwiano wa biashara. Hatua hiyo bila shaka itayapatia makampuni ya nchi za nje fursa nyingi za kufahamu na kuweza kuingia kwenye soko la China, pia itawapatia wananchi wa China aina nyingi za bidhaa."

Wataalamu wanaona kuwa ingawa makampuni ya nchi za nje yaliyoshiriki kwenye maonesho ya 101 ya kimataifa ya bidhaa zinazosafirishwa nje na zinazoagizwa kutoka nje ya China bado yalikuwa machache, lakini kutokana na mabadiliko ya sera za biashara ya China, bila shaka makampuni ya nchi za nje yatakayoshiriki kwenye maoneosho ya 102 yataongezeka.