Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-05-09 20:19:24    
Kampuni ya Huawei ni mfano mzuri wa ushirikiano kati ya China na Misri

cri

Kampuni ya Huawei ni kampuni kubwa ya kutengeneza vifaa vya mawasiliano ya habari nchini China, kampuni hiyo ni mfano mzuri wa ushirikiano kati China na Misri. Mwaka 1999 kampuni ya Huawei ilianzisha tawi lake nchini Misri, katika miaka minane iliyopita kampuni hiyo ilipata maendeleo makubwa katika kutoa huduma ya vifaa vya mawasiliano ya habari nchini Misri, kufunga vifaa hivyo na mtandao mkubwa wa internet. Kuhusu maendeleo ya kampuni hiyo nchini Misri, mwakilishi wa mambo ya biashara katika ubalozi wa China nchini Misri Bw. Jin Jing alisema,

"Katika muda wa miaka minane ya maendeleo kampuni hiyo nchini Misri imekuwa na soko kubwa. Hivi sasa kampuni hiyo ina wafanyakazi zaidi ya 700, na kati yao 65% ni Wamisri, kampuni hiyo imeiletea Misri nafasi nyingi za ajira. Hivi sasa kampuni hiyo imekuwa mtengenezaji mkubwa wa vifaa vya mawasiliano ya habari, na vifaa vyake vinahudumia maeneo 70% katika mawasiliano ya habari nchini Misri."

Bw. Jin Jing alieleza kuwa kwa kushirikiana na kampuni ya mawasiliano ya habari ya Misri, shughuli za kampuni ya Huawei zimeenea kwenye miji mingi ya utalii na yenye wakazi wengi katika mtandao wa CDMA. Katika shughuli za simu za mkononi, baada ya kufanya majaribio kwa makini, kampuni hiyo ilianza kushirikiana na kampuni ya Mobinil ambayo ni kampuni kubwa nchini Misri, na kuwa mhudumu mkubwa wa vifaa. Tarehe 10 Septemba mwaka 2006 Misri ilitangaza kuwa kampuni ya Huawei imefanikiwa kupata zabuni na kuwa mhudumu wa vifaa vya simu za mkononi nchini Misri.

Kwa kuzingatia maendeleo ya simu za mkononi nchini Misri, kampuni ya Huawei inajitahidi kudhibiti uchafuzi wa mazingira kwa kutumia vifaa vilivyo bora ambavyo kwa kiasi kikubwa vinaweza kutumiwa kwa marudio. Meneja mkuu wa kampuni ya Huawei ya China ya kaskazini mashariki Bw. Wang Jiading alisema, kampuni ya Huawei nchini Misri imepata uungaji mkono wa rais Hosni Mubaraka wa Misri na Wizara ya Mawasiliano ya Habari ya Misri, vifaa na huduma bora ya kampuni ya Huawei inasifiwa sana.

"Kampuni ya Huawei ikiwa ni moja ya makampuni makubwa duniani inatilia maanani kuleta manufaa kwa nchi inayoshirikiana nayo na watu wake. Misri ni moja ya nchi zinazoendelea haraka katika masoko duniani, teknolojia ya kampuni ya Huawei imetoa mchango mkubwa katika ushirikiano wa kiuchumi kati ya China na Misri."

Kampuni hiyo imeanzisha vituo vya mafunzo ya teknolojia na kuajiri wenyeji wengi. Mkurugenzi wa kitengo cha teknolojia katika kampuni hiyo, kijana wa Misri Bw. Moheb Adel Ramses alisema

"Nimefanya kazi katika kampuni ya Huawei zaidi ya miaka mitano sasa. Mwanzoni nilikuwa na shida kutokana na kutoelewa sana Wachina, lakini sasa baada ya miaka mitano nimefanikiwa kwenye mambo ya usimamizi na teknolojia."

Balozi wa China nchini Misri Bw. Wu Sike alipotembelea kampuni ya Huawei hivi karibuni alisema,

"Kutokana na kuungwa mkono na serikali za China na Misri, ushirikiano kati ya nchi mbili unaendelea vizuri sana. Hivi sasa makampuni 270 ya China yamewekeza nchini Misri. Ushirikiano kati ya China na Misri ni wa usawa na wa kunufaisha pande mbili, ni ushirikiano unaowanufaisha wananchi wa nchi mbili. Ushirikiano huo pia umesukuma mbele ushirikiano wa teknolojia kati ya China na Misri. Hivi sasa mashirika ya China nchini Misri yamewapatia ajira watu 6,000 wa Misri."