Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-05-09 20:30:11    
Vitu vya sanaa za mikono vya makabila madogo madogo mkoani Qinghai

cri

Katika mkoa wa Qinghai, kaskazini magharibi mwa China, wanaishi watu wa makabila mengi yakiwemo Wa-han, Wa-tibet, Wa-hui, Wa-tu, Wa-sala na Wa-mongolia. Watu wa makabila hayo wanapojitahidi kujiendeleza kiuchumi, pia wamevumbua utamaduni wenye umaalum wa kikabila. Hadi baadhi ya ustadi wa kutengeneza vitu vya sanaa kwa mkono bado unaenea.

Suyouhua, Duixiu na Tangka ni Vitu vitatu maarufu vya sanaa za mikono vya kabila la Wa-tibet mkoani Qinghai. Suyouhua ni vitu vya sanaa vinavyotengenezwa kwa samli. Inasemekana kuwa, waumini wa dini ya kibudha ya kitibet waishio mkoani Qinghai walikuwa na desturi ya kutoa sadaka za samli kwa mahekalu kwa ajili ya kuwasha taa na kutoa chakula kwa watawa. Watawa walichanganya samli zilizobaki pamoja na madini yenye rangi mbalimbali, halafu kutengeneza maua ya samli na sanamu za mabudha, wanadamu, milima na pagoda, wanyama na ndege, miti na maua. Lakini kwa kuwa ni rahisi kwa samli kuyeyuka, hivyo iliwalazimu kutengeneza sanamu za samli katika hali ya baridi, watawa walipotengeneza sanamu za samli walipaswa kuingiza mikono yao kwenye maji baridi ili kupunguza joto la mikono yao.

"Duixiu" ni picha za sanaa zinazotengenezwa kwa njia ya kuunganishwa kwa ustadi wa tarizi na ustadi wa uchongaji. Yaani vitambaa vya hariri vyenye rangi mbalimbali vikatwe kuwa vipande vyenye umbo mbalimbali, kama vile mabudha, binadamu, maua, wanyama na ndege, vipande hivyo vishonwe na kujazwa sufu au pamba, halafu vitariziwe kwenye batiki nzito. Sanaa za "Duixiu" zinaonekana kama vitu vyenye uhai, na sanaa nyingi za "Duixiu" zinahusiana na dini ya kibudha. Ustadi wa kutengeneza "Duixiu" umerithishwa na wakazi wa mkoani Qinghai kwa miaka mamia na maelfu, hivi sasa utengenezaji wa "Duixiu" umekuwa shughuli zinazopendwa na wanawake wa huko wakati wa mapumziko ya kilimo.

Bi. Qiao Yinju ni mzaliwa kijijini, alijifunza ustadi wa kutengeneza "Duixiu" kutoka kwa mama yake. Alipoona kuwa vitu vya sanaa za mikono vya kikabila vinapendwa na watalii, aliacha kilimo na kuanzisha karakana ya kutengeneza sanaa za "Duixiu" na kufungua duka la kuziuza. Alisema:

"Mimi nafurahia biashara ya kuuza vitu vya sanaa za 'Duixiu'. Nimepanga kuwaajiri watu wengi zaidi ili kupanua biashara yangu."

Tangka ni sanaa ya michoro ya kabila la Wa-tibet, iliyoanza kujitokeza katika karne ya 7, sanaa hiyo ina umaalum wa kipekee wa kikabila na kidini. Rangi za kuchora picha za Tangka zinatokana na madini, hivyo hazibadiliki kwa muda mrefu. Sanaa za Tangka huonesha picha za mabudha, hutundikwa kwenye mahekalu, ukumbi wa kuwekea sanamu za Buddha, mahali pa kukaa watawa na hata nyumbani kwa waumini wa dini ya kibuddha ya kitibet. Bwana Dawa na mke wake wa kabila la Wa-tibet wanaishio Xining, mji mkuu wa Qinghai wanafanya biashara ya sanaa za "Tangka". Alisema:

"Zamani tuliishi maisha ya kujifungia, na vitu vya sanaa za mikono vilivyotengenezwa mkoani kwetu havikujulikana duniani. Hivi sasa watalii wengi wa nchini China na nchi za nje wanakuja kutembelea, na wanapenda sana vitu vya sanaa vya mikono vya kikabila. Naona biashara ya kuuza vitu hivyo ina mustakabali mzuri."

Bw. Dawa na mke wake wanapanga kutia mambo ya kisasa katika sanaa za "Tangka", kuvumbua "Tangka" za vinyago, samani za mtindo wa kabila la Tibet ili kuenzi na kurithisha vitu vya sanaa za mikono vya kikabila mkoani Qinghai. Bi. An Chunxiu na dada yake An Chunlan ni wa kabila la Wa-tu, nusu ya mwaka uliopita, walianzisha kiwanda cha kutengeneza Tangka ya Closionn kwa nyuzi za dhahabu na rangi mbalimbali za madini, Tangka za aina hiyo ni maridadi sana, hivyo zinapendwa sana sokoni.

Licha ya sanaa za sanamu za samli, sanaa za Duixiu na Tangka, vitu vya sanaa vya tarizi na picha zilizotengenezwa kwa sufu pia vinajulikana mkoani Qinghai. Hivi sasa watu wa Qinghai wanaoshughulikia biashara ya vitu vya sanaa vya mikono vya makabila madogo madogo wanazidi kuongezeka, na serikali ya huko pia imefanya juhudi kuwaandaa mafundi wa sanaa wa makabila mbalimbali. Bwana Lei Yilin kutoka kituo cha utamaduni cha wilaya ya Huangzhong alisema:

"Hivi sasa shule ya ufundi ya wilaya ya Huangzhong imeanzisha madarasa matatu ya kufundisha namna ya kutengeneza sanaa za Tangka, Duixiu na Tarizi, kila darasa lina wanafunzi zaidi ya 70."