Katika mji wa Addis Ababa, Ethiopia kuna barabara ya urafiki ya Ethiopia na China inayojulikana kwa wakazi wote wa mji huo. Miaka mitatu iliyopita, kampuni ya barabara na daraja ya China ilikamilisha ujenzi wa barabara hiyo yenye sifa bora katika muda mfupi, ambapo kampuni hiyo ya China ilisifiwa sana nchini humo.
Barabara ya urafiki ya Ethiopia na China iko katika sehemu zenye pilikapilika za kibiashara mjini Addis Ababa, ni moja ya barabara kubwa za mji huo. Mwezi Desemba mwaka 2003, barabara hiyo iliyojengwa na kampuni ya barabara na daraja ya China chini ya msaada wa serikali ya China ilianza kufanya kazi rasmi. Ujenzi wa mradi huo uliosanifiwa kukamilika kwa miezi 17 ulikuwa umekamilika katika muda wa zaidi ya miezi 2 tu. Meneja mkuu wa tawi la kampuni hiyo la Addis Ababa Bwana Cheng Sai alisema:
"Nilipomwambia mkurugenzi wa idara ya barabara ya Ethiopia kuwa, tutakamilisha ujenzi wa mradi huo tarehe 17 Desemba,
alidhani ni siku hiyo ya mwaka wa pili. Hakuweza kuamini maneno niliyosema."
Jambo hilo lilikuwa ajabu kubwa nchini Ethiopia, wakati huo vyombo vya habari vya nchi hiyo vilitoa habari nyingi kuhusu muujiza huo uliofanywa na kampuni ya barabara na daraja ya China. Wakazi wa Ethiopia pia wanakumbuka vizuri jambo hilo, dereva wa Addis Ababa Bw. Ermias Tekelemariam aliwaambia waandishi wetu wa habari, akisema:
"Niliwahi kushuhudia ujenzi wa barabara nyingi, huwa zilitumiwa muda mrefu kukamilika, lakini wachina walitumia muda usiozidi miezi mitatu kujenga barabara ya urafiki ya Ethiopia na China. Barabara hiyo imetunufaisha sana."
Hivi sasa makampuni kadhaa makubwa ya ujenzi ya China yameingia nchini Ethiopia na miradi ya barabara na madaraja iliyojengwa na wachina inaonekana kote nchini humo. Mhusika wa Ethiopia Bwana Samson Wondimu alisema, katika miaka 8 iliyopita, makampuni ya China yalipata kandarasi nyingi za ujenzi wa barabara. Hivi sasa serikali ya Ethiopia inatekeleza mpango wa miaka mitano wa maendeleo ya barabara, na makampuni ya China kwa jumla yamesaini mikataba ya ujenzi wa miradi ya barabara yenye urefu wa kilomita 2549.
Balozi wa China nchini Ethiopia Lin Lin alishuhudia maendeleo makubwa ya uhusiano wa kiuchumi na kibiashara kati ya China na Ethiopia katika miaka miwili iliyopita. Alisema:
"Miaka miwili na nusu iliyopita, thamani ya ujenzi wa miradi iliyosainiwa mkataba na makampuni ya China nchini Ethiopia ilikuwa dola za kimarekani milioni 800, sasa thamani hiyo imeongezeka maradufu. Hivi sasa Ethiopia iko katika kipindi cha kujenga miundo mbinu kwa wingi, makampuni ya China yanaweza kuchangia ujenzi wa miundo mbinu wa nchi hiyo kama vile barabara, vituo vya kuzalisha umeme, mawasiliano ya simu, nyumba na utoaji maji."
Balozi Lin Lin alisema waziri mkuu wa Ethiopia Bw. Meles Zenawi aliwahi kusema, maendeleo ya China yameleta fursa nyingi kwa Ethiopia na nchi za Afrika kwa ujumla. Kushiriki kwa makampuni ya China katika ujenzi wa Ethiopia na nchi nyingine za Afrika, kumepunguza gharama za ujenzi wa miradi, na juhudi kubwa za wachina katika ujenzi wa miradi pia zimekuwa mfano wa kuigwa kwa watu wa Ethiopia.
|