Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-05-10 20:14:02    
Wakili anayetoa msaada wa kisheria kwa wakulima

cri

Siku ya wafanyakazi wa duniani mwaka huu, yaani tarehe mosi Mei ni siku yenye umuhimu mkubwa kwa Bw. Tong Lihua ambaye ni wakili mmoja nchini China, kwani katika siku hiyo alipewa tuzo ya wafanyakazi na serikali ya China, ambayo ni tuzo yenye heshima kubwa kabisa kwa wafanyakazi wa China. Wakili Tong Lihua alipata tuzo hiyo kutokana na mchango mkubwa alioutoa katika kulinda maslahi halali ya wakulima wanaofanya kazi za vibarua mijini.

Mliyosikia ni rekodi ya sauti iliyonaswa kwenye kituo cha kutoa msaada wa kisheria kwa wakulima wanaofanya kazi za vibarua mjini Beijing. Wakulima wanakifahamu sana kituo hicho, ambapo wanaweza kupata ushauri wa kisheria na mawakili wa huko wanawatetea katika kesi mahakamani bila malipo.

Mkulima Wang Songqiang mwenye umri wa miaka 25 anatoka mkoa wa Henan, sehemu ya kati ya China. Alifika Beijing miaka mitano iliyopita na kuanza kufanya kazi kwenye kiwanda kimoja cha kutengeneza mkanda wa filamu. Lakini mwajiri hakumwingiza kwenye utaratibu wa mkataba wa ajira, wala bima za ajali kazini, afya na utunzaji wa uzeeni kwa kufuata sheria. Kwa hiyo mkulima huyo alikwenda kutafuta msaada wa kisheria kwenye kituo hicho.

Alisema "Wenzangu waliniambia kuwa kuna kituo hicho, na walisema naweza kupata ushauri wa kisheria kutoka kwa mawakili wa hapa, pia wanaweza kunitetea katika kesi mahakamani. Kwa hiyo nimekuja. Natumai kuwa kituo hiki kitanisaidia kuishinikiza kampuni ili nilindwe na bima."

Utandawazi wa miji nchini China umevutia nguvu kazi nyingi ya ziada kutoka vijijini. Pamoja na wakulima hao kutoa mchango kwa ujenzi wa miji, matukio yanayoathiri maslahi yao yanatokea mara kwa mara. Kwa sababu maisha ya mijini ni mageni kwa wakulima, na wakulima wengi hawana elimu ya kiwango cha juu, kwa hiyo wana uwezo mdogo katika kulinda maslahi yao.

Mwanzilishi wa kituo hicho cha kutoa msaada wa kisheria kwa wakulima hao ni wakili Tong Lihua mwenye umri wa miaka 36. Amefanya kazi ya uwakili kwa miaka 12. Alitaja tukio lililotokea miaka minne iliyopita ambalo lilimfanya aanze kujishughulisha na kuwahudumia wakulima. Alisema "Marafiki zangu wawili wa utotoni waliokuwa wanafanya kazi za vibarua mjini Tianjin, walidai mishahara yao ya zaidi ya Yuan elfu 8 kwa muda mrefu bila mafanikio. Baada ya kukata tamaa, walinipigia simu kuomba msaada. Kwa hiyo nilianza kujihusisha na shughuli hizo, nikitaka kuwasaidia marafiki na kuangalia ni matatizo gani yanayowasumbua wakulima wanaofanya kazi za vibarua mijini."

Wakili Tong Lihua na wenzake walianzisha kituo hicho cha kutoa msaada wa kisheria bila malipo mwezi Septemba mwaka 2005. Alisema "Hatudai hata senti moja kwa wakulima wanaofanya kazi za vibarua mijini. Zaidi ya hayo iwapo mawakili wetu wakiambatana na wakulima kwa teksi wakati wa kushughulikia kesi, tunalipa nauli ya teksi. Mawakili wetu wakila chakula pamoja na wakulima, tunalipa pia. Kesi zikikamilishwa, katika baadhi ya kesi wakulima wanadai fidia ya Yuan laki kadhaa, hatudai hata seti moja kutoka kwa wakulima."

Bw. Tong Lihua alieleza kuwa utendaji wa kituo hicho unasaidiwa na idara ya mambo ya sheria ya Beijing, yaani kwa kushughulikia kesi moja, kituo hicho kinapata posho kutoka kwa serikali, na sehemu nyingine ya gharama inatokana na ufadhili kutoka kwa jamii.

Sawa na hali ilivyo katika nchi nyingi, mawakili wa China ni miongoni mwa watu wanaolipwa vizuri. Lakini wakili Tong Lihua na wenzake wana mishahara inayolingana na ile ya wafanyakazi wa kawaida wa Beijing. Ofisi yake ina samani chache za kawaida tu, meza, kiti, safu ya vitabu na vyungu viwili vya maua. Wakili huyo alisema,

 "Kituo chetu hakifanyi biashara, hatuna pesa za kugharimia ununuzi wa samani nyingi, tena hatuoni vitu kama hivyo vina umuhimu sana. Tunataka pesa zitumike kazini na kuwahudumia watu wengi zaidi."

Mbali na wakili Tong Lihua kituo hicho kina mawakili wengine zaidi ya 10. Kutokana na mfano mzuri wa Bw. Tong, mawakili wenzake pia hawajali kiwango cha mishahara, wanashughulikia kila kesi kadiri wanavyoweza na kutoa ushauri kwa kina kwa kila mkulima anayekwenda kutafuta msaada wa kisheria. Katika siku za mapumziko, mara kwa mara mawakili hao wanapaswa kufanya kazi. Baadhi ya siku wanapaswa kwenda kazini mapema sana asubuhi. Wanafanya bidii kubwa zaidi kuliko mawakili wa kibiashara, lakini wanalipwa kidogo sana kuliko mawakili wenzao.

Wakili Xing Wei wa kituo hicho alisema "Tuliamua kufanya kazi kwenye kituo hicho kutokana na kuvutiwa na utendaji wa Bw. Tong Lihua. Naona yeye ni mtu anayefanya kazi halisi, na amefanya kazi nyingi halisi kwenye shughuli za kuhudumia jamii. Sisi pia tunataka kutenda kazi halisi na kutoa mchango kwa jamii. Kama tunazingatia sana pesa zetu tunazoweza kupata, hakika tusingefanya kazi hapa kituoni."

Hivi sasa Bw. Tong Lihua ni mmoja wa wakuu wa kamati ya msaada wa kisheria iliyo chini ya shirikisho la mawakili la China. Alisema anaridhika na hatua mbalimbali zilizochukuliwa na serikali katika miaka ya hivi karibuni katika kulinda maslahi ya wakulima wanaofanya kazi za vibarua mijini, na hatua hizo zimepata mafanikio. Alitoa mfano wa marafiki zake wawili wa utotoni, kwamba hivi sasa waajiri wanaweza kulipa mishahara kwa wakati kwenye kadi za benki za wafanyakazi. Hata hivyo matukio ya kuathiri maslahi ya wakulima wanaofanya kazi za vibarua mijini yanaendelea kutokea katika sehemu fulani, kwa hiyo wakili Tong Lihua alieleza kuwa kamati hiyo itashirikisha mashirika ya mawakili ya mikoa mbalimbali ya China, kuendelea kutoa msaada wa kisheria kwa wakulima hao.