Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-05-11 20:58:03    
Wakulima wa China waanzisha shamba la kilimo nchini Sudan

cri

Sudan ni nchi iliyoko kaskazini mashariki mwa bara la Afrika, lakini wachina wote wa huko wanaweza kupata mboga za kichina, hali hii inatokana na wakulima wa China waliokwenda Sudan kufanya shughuli za kilimo kuanzia miaka ya 90 ya karne iliyopita. Katika nchi hiyo yenye joto kabisa duniani, wachina hao wanajishughulisha na kilimo kwa juhudi na kuwatosheleza mboga wachina wanaofanya kazi nchini Sudan pamoja na wasudan.

Kilimo cha Sudan kina nafasi kubwa ya kuendelezwa, na serikali ya Sudan inawakaribisha wageni kwenda kuwekeza na kufanya shughuli za kilimo, na kuwapa sera yenye nafuu katika usimamizi wa kuingia na kukaa nchini Sudan, kutoza kodi ya mapato na kodi ya biashara. Hali hii inawasaidia wakulima wa China kwenda kufanya shughuli za kilimo nchini Sudan.

Katika miaka 10 iliyopita, wakulima wa aina tatu wa China walikwenda Sudan kujishughulisha na kilimo.

Aina ya kwanza ni wakulima waliosaini mkataba wa kazi na makampuni ya China. makampuni yanakodi ardhi kutoka kwa wasudan na kutoa vifaa vya kilimo kwa wakulima. Wakulima wa China wanapata mishahara kila mwezi, na mazao ya kilimo pia yanatumika kwa wafanyakazi wa makampuni hayo. Kampuni ya Sinopec na kampuni ya ujenzi ya China ni makampuni yaliyoanzisha shamba la kilimo mapema sana nchini Sudan.

Aina ya pili ni wafanyakazi wa China wanaoajiriwa na makampuni ya China kufanya kazi nchini Sudan. Muda wao wa mkataba wa kazi ni miaka miwili. Baada ya kumaliza muda wa mkataba, watu wachache kati yao hawarudi nyumbani na wanaanzisha mashamba yao na kufanya uzalishaji wa kilimo.

Aina ya tatu ni wakulima waliopata habari kuwa kulima nchini Sudan kunaweza kupata pesa, ambao walikwenda Sudan kufanya kazi hiyo. Baadhi yao wana nguvu halisi ya kiuchumi kwa kiasi fulani, na wengine ni wataalamu wa uzalishaji wa kilimo, hivyo wanaweza kuendesha mashamba vizuri na kupata mapato makubwa.

Mazingira ya kimaumbile nchini Sudan si mazuri, hali ya hewa ni ya joto na hewa huwa kavu, hasa vijijini, mazingira ya usafi si mazuri na utoaji wa maji ya kunywa ni duni. Wakulima wa China wanaotaka kuanzisha mashamba nchini humo, wanapaswa kutatua matatizo kadha wa kadha. Ni kwa kutatua matatizo mengi tu, ndipo wachina wanapoweza kuishi kwenye mazingira hayo kufanya shughuli za uzalishaji wa kilimo.

Hivi sasa, wachina wameanzisha mashamba 7 yenye ukubwa wa kiasi nchini Sudan.

Bw. Li Qiang ambaye anatoka mji wa Dezhou mkoani Shandong, alikwenda Sudan miaka 10 iliyopita, yeye ni mmoja wa wakulima wa China waliokwenda Sudan mapema zaidi kujishughulisha na kilimo. Shamba lake la kilimo linapanuka siku hadi siku, hivi sasa ukubwa wa shamba lake umefikia zaidi ya hekta 20.

Bw. Fan Chuanzhao ambaye anatoka mji wa Binzhou mkoani Shandong anashughulikia mashamba karibu na Khartoum mji mkuu wa Sudan. Alianzisha shamba lake tangu mwaka 2005. ingawa yeye alichelewa kufika Sudan kuliko wachina wengine, lakini kutokana na juhudi zake sasa amekuwa mkulima hodari zaidi kati ya wakulima wa China nchini Sudan.

Wakulima wa China siyo tu wanafanya shughuli na kujipatia pesa, bali pia wanasaidia kuwafundisha wakulima wa Sudan ujuzi wa kilimo.

Bw. Fan aliajiri wakulima zaidi ya 20 kutoka sehemu ya Darfur magharibi mwa Sudan. Bw. Fan alisema "Wadarfur wana matatizo makubwa ya kiuchumi, nitawasaidia kwa juhudi kadiri niwezavyo."

Bw. Khalil Ibrahim mwenye umri wa miaka 27 hivi karibuni alikuwa mtu mwenye furaha, kwa sababu atarudi nyumbani kutembelea jamaa zake. Maskani yake yako katika kijiji kimoja karibu na Geneina mji mkuu wa jimbo la Darfur ya magharibi. Yeye hajawahi kurudi nyumbani kwa miaka miwili tangu mwaka 2005 alipoanza kufanya kazi kwenye shamba hilo. Alisema "sasa nina pesa, naweza kurudi nyumbani." Na ameamua kurudi nyumbani pia kwa sababu ya hali ya usalama ya Darfur inazidi kuwa nzuri siku hadi siku.

Bw. Ibrahim alisema wazazi wake, mke wake na mtoto wake wako kwenye maskani yake. Kila baada ya muda fulani alikuwa anawatumia pesa, ili kuwatosheleza maisha yao. Anaridhika na kazi yake, siyo tu kutokana na mapato anayopata, bali pia kutokana na wafanyakazi wa China wanaofanya kazi katika shamba hilo kumtendea kwa usawa, na kumfundisha ujuzi mwingi wa kilimo.

Bw. Mohamud Yaqub mwenye umri wa miaka 38, ni mkulima wa Darfur aliyeanza kufanya kazi kwenye shamba hilo zamani sana, wengi wa wakulima wa shamba hilo wanatoka Darfur kutokana na yeye kupendekeza, na yeye amekuwa mkuu wao na anapata pesa nyingi zaidi. Alisema wakulima hao wa Darfur walikuja Khartoum miaka miwili iliyopita, jamaa zao bado wako Darfur. Wanatuma pesa zao zote kwenye maskani yao, ili kuwafanya jamaa zao wawe na mapato. Alisema, hakuna hata mmoja wa jamaa wa wakulima wa Sudan wanaofanya kazi huko, waliokwenda kwenye kambi ya wakimbizi. Watu hawapendi kwenda kwenye kambi ya wakimbizi baada ya kupata uhakikisho wa maisha.

Bw. Fan alisema, wakati alipoanzisha shamba hilo mwishoni mwa mwaka 2004, aliambiwa kuwa kuna wasudan waliokimbilia karibu na shamba lake kutoka Darfur, hivyo aliamua kuwaajiri. Alisema kama ukimpa mtu maskini mfuko mmoja wa mchele, atakufa kutokana na njaa baada ya kumaliza mchele huo, lakini kama ukimpa mtu huyo ajira, mtu huyo hatakufa. Njia nzuri zaidi ya kuwasaidia wadarfur ni kuwasaidia kupata ajira.

Bw. Fan pia alisema anajua Darfur ni sehemu yenye mazingira mazuri kabisa ya kimaumbile nchini Sudan, kama Darfur ikitimiza amani, bila shaka ataanzisha shamba huko Darfur.