Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-05-14 14:26:02    
Moja kati ya vipindi 24 katika kalenda ya kilimo ya China, "Siku ya Kuanza kwa Majira ya Joto"

cri

Katika kalenda ya kilimo ya China kuna vipindi 24 kutokana na mabadiliko ya hali ya hewa nchini China. Tunaposema siku ya kipindi fulani tuna maana ya siku ya kuanza kwa kipindi hicho. Kugawa vipindi 24 katika kalenda ya kilimo ya China ni busara za Wachina wa kale kutokana na uzoefu wao wa muda mrefu kuhusu hali ya hewa na unajimu, vipindi hivyo vinasaidia sana kwenye shughuli za kilimo. Kwa mujibu wa historia, mapema mwaka 104 K.K. watu wa China walikuwa wamepata vipindi hivyo 24.

Siku ya kuanza kwa majira ya joto huwa ni tarehe 5, 6 au 7 mwezi Mei katika kalenda ya Kikristo, mwaka huu siku hiyo ni tarehe 6. Siku ya kuanza kwa majira ya joto ina maana kwamba kuanzia siku hiyo, majira ya Spring yamepita na majira ya joto yameanza, na joto litaongezeka haraka, na mvua za radi zitakuwa nyingi. Kuna misemo miongoni mwa wakulima isemayo, "mvua isiponyesha katika siku ya kuanza kwa majira ya joto, plau na jembe vinakuwa haina kazi", kwa hiyo ni bora mvua inyeshe katika siku hiyo. Lakini kwa sababu China ni nchi kubwa, hali ya hewa kati ya sehemu ya kusini na ya kaskazini ni tofauti. Katika sehemu ya kusini, wakati huo baadhi ya mazao yanakuwa yameingia katika siku za kukomaa, kwa hiyo kuvuna kwa wakati na kukinga mvua ili mazao yasilowe ni kazi ya lazima. Lakini katika sehemu ya katikati na ya kaskazini ya China, majira ya Spring yamepita hivi karibuni na kabla na baada ya siku ya kuanza kwa majira ya joto, joto linaongezeka haraka na upepo huwa mwingi, hewa huwa kavu na ardhi huwa kame, hali hiyo inaathiri mimea, kwa hiyo wakati huo mvua ikinyesha itasaidia sana kukua kwa mimea, hasa ngano. Iwapo mvua huwa ni chache, umwagiliaji ni hatua za lazima. Baada ya majira ya joto kuanza, magugu yanaota haraka, wakulima wanasema, "siku moja usipopalilia, utashindwa kuyafyeka magugu hata kwa siku tatu". Wakati huo kufyeka magugu sio tu kunasaidia ardhi kuongezeka joto na kuyeyusha virutubisho ili mimea ifyonze, tena kunasaidia sana kuimarisha mimea ya pamba, mahindi, mtama na njugu nyasa.

Siku ya kuanza kwa majira ya joto pia ni siku ya aina moja ya utamaduni. Katika sehemu ya kaskazini ya China watu wana mila ya kula mayai yaliyochemshwa. katika siku hiyo, watu wanachemsha mayai, na baada ya kuiva yanatiwa ndani ya maji baridi, ili maganda yake yabanduliwe kirahisi, kisha kila mwanafamilia mmoja anakula moja. Labda kwa sababu yai linafanana na umbo la moyo, watu wanaona kula yai hilo katika siku hiyo msingi wa afya unaimarika, na baadhi ya watu wanaona kuwa baada ya siku ya kuanza kwa majira ya joto, joto litakuwa kali na kula yai hilo laini, ngozi pia itakuwa laini na haitapata majipu. Katika sehemu ya kusini ya China watu wana mila ya kula mazao mapya ya aina tatu, kama maharage, mchicha na matango. Na katika mkoa wa Fujian na kisiwa cha Taiwan, katika siku hiyo watu wana mila ya kula kamba, kwani watu wa sehemu hizo wanasema "kamba" na "majira ya joto" ni sawa katika lugha ya Kichina, wanakula kamba wanamaanisha kupita salama kwenye majira ya joto.