Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-05-14 14:46:49    
Matembezi ya kuangalia msitu wa mianzi wa Yunding ulioko katika mji wa Haiyang, mkoani Shandong

cri

Wasikilizaji wapendwa karibuni katika kipindi hiki cha safari nchini China, katika kipindi hiki cha leo tutawafahamisha kuhusu msitu wa mianzi wa Yunding, ulioko kwenye sehemu ya kiunga cha mji wa Haiyang, mkoani Shandong, sehemu ya kaskazini mwa China. Wakazi wa sehemu ya kusini mwa China wanaona misitu ya mianzi mara kwa mara, lakini kutokana na tofauti ya hali ya hewa, wakazi wa sehemu ya kaskazini mwa China ni nadra sana kuona msitu wa mianzi. Msitu wa mianzi wa Yunding unachukua nafasi ya kwanza kwa ukubwa kwenye sehemu ya kaskazini mwa China, hivi sasa msitu huo wa mianzi umeendelezwa kuwa sehemu yenye mandhari nzuri ya kimaumbile inayowavutia sana watalii wengi wa nchini China na wa nchi za nje.

Sehemu yenye mandhari nzuri ya msitu wa mianzi wa Yunding iko kwenye sehemu ya kaskazini mashariki mwa mji wa Haiyang, mkoani Shandong, sehemu hiyo yenye mandhari nzuri ina eneo la hekta zaidi ya 330, ambapo eneo la msitu wa mianzi ni kiasi cha hekta 60. Asilimia 60 ya mandhari nzuri ya msitu wa mianzi zimedumisha hali ya asili ya kimaumbile, ambapo inaota aina nyingi za mimea mwitu, licha ya hayo miti ya ginkgo na mipapai inayoota huko ilikuweko tokea miaka mia kadhaa iliyopita. Ni dhahiri kuwa, kitu kinachovutia watu zaidi ni mianzi inayoota kwenye milima ya huko.

Kiongozi wa sehemu yenye mandhari ya msitu wa Yunding Bw. Li Jinbao alisema, mianzi inayoota huko ililetwa Haiyang na mchoraji maarufu Bw. Zheng Banqiao wa enzi ya Qing ya China kutoka sehemu ya kusini mwa mto Changjiang zaidi ya miaka 200 iliyopita. Michoro ya mianzi iliyochorwa na Zheng Banqiao ni mizuri sana, na inahifadhiwa na watu wengi. Kuna sanamu moja kwenye mlango wa kuingilia kwenye sehemu ya mandhari ya msitu wa mianzi, sanamu hiyo ilichorwa na Zheng Banqiao. Bw. Li Jinbao alisema,

"Hayo ni maneno yaliyoandikwa kwenye vitabu vya historia na ya kuthibitishwa. Mchoraji Zheng Banqiao alikwenda huko kuangalia, aliona kuwa huko ni sehemu inayopendeza sana, hivyo alileta mianzi kadhaa kutoka kwao. Baadaye watu waligundua kuwa, mianzi inaweza pia kuota kwenye sehemu ya kaskazini, hivyo waliitunza vizuri hadi hivi sasa, msitu huo wa mianzi umekuwa urithi wa utamaduni wenye thamani kubwa kwa vizazi vya baadaye."

Bw. Li Jinbao amefanya kazi kwa miaka mitano kwenye sehemu ya mandhari ya msitu wa mianzi, na anafahamu sana hali ya ukuaji wa msitu wa mianzi wa Yunding. Alisema, Zheng Banqiao licha ya kuleta mianzi kwenye sehemu ya Yunding, pia alichora michoro mingi kwenye sehemu hiyo. Mbele ya sanamu ya Zheng Banqiao, kuna banda moja lililojengwa kwa mianzi, inasemekana kuwa banda hilo ndio sehemu ambayo Zheng Banqiao alipokuwa anafanya kazi ya kuchora.

Zaidi ya aina 20 za mianzi inaota kwenye msitu wa mianzi wa Yunding, ambayo mingi yake ni mianzi ya Dan na Gang. Mianzi ya aina ya Dan ni miembamba na si rahisi kukatika, hivyo inatumika sana katika kusuka vyombo vya mianzi; Mianzi ya aina ya Gang ni mirefu, imenyooka na yenye rangi ya kijani kibichi, mianzi ya aina hiyo inaweza kuota katika mazingira magumu bila tatizo lolote. Bw. Wang Xuefeng, ambaye anapenda kutalii kwenye msitu wa mianzi wa Yunding, alisema yeye anapenda sana mianzi, tena alieleza umaalumu mwingine wa msitu wa mianzi wa Yunding. Alisema,

"Mianzi ya aina ya Dan inaota zaidi kwenye mlima wa Kunlun na mlima wa Lao, lakini mianzi mikubwa ya aina ya Mao inayoota hapa ni sawa sawa na ile inayoota kwenye sehemu ya kusini mwa China, kwani mianzi ya aina hiyo ni nadra kuonekana kwenye sehemu ya kaskazini, kwa hiyo ninasema huu ni umaalumu wa msitu wa mianzi wa Yunding."

Kwenye msitu wa mianzi wa Yunding, kuna sehemu moja yenye kundi la mianzi inayojulikana kama mianzi ya mbalamwezi. Kiongozi msimamizi wa msitu wa mianzi Bw. Li Jinbao alisema, kila siku baada ya giza kuingia huko mianzi hiyo yenye rangi ya kijani inarudisha mwangaza wa mwezi, upepo mwororo ukivuma, mwangaza unaorudishwa na mianzi inaonekana kama mamilioni ya vimetameta vinavyorukaruka, na hii pia imekuwa moja ya mandhari nzuri maarufu ya sehemu ya msitu wa mianzi wa Yunding.

Baada ya kupita kwenye sehemu ya msitu mnene wa mianzi ya "mianzi ya mbalamwezi", watalii wanaweza kuona hekalu moja la kibudha linalojulikana kwa jina la "hekalu la Yunding". Hekalu la Yunding lenye eneo la mita za mraba 1,000, ingawa haijulikani lilijengwa mwaka gani, lakini habari zilizoandikwa kwenye vitabu vya historia zinaonesha kuwa, hekalu hilo lilijengwa katika enzi ya Tang nchini China zaidi ya miaka 1,000 iliyopita, ambapo watu wengi walikwenda kuabudu mabudha kwenye hekalu hilo.

Baada ya kuondoka kutoka kwenye hekalu, ni msitu mnene sana wa mianzi ambapo maji yanatiririka kwenye mfereji. Watu wanakwenda mbele kwa kufuata mfereji huo wanaweza kuona mpapai mmoja wa kale ulioota miaka zaidi ya 300 iliyopita.

Baada ya kutoka kwenye msitu wa mianzi wa Yunding, sehemu inayofuata ni mahali ambapo watu wanakula chakula kwenye sehemu yenye mandhari ya kupendeza. Watalii licha ya kuweza kula vichipukizi vya mianzi, pia wanaweza kula aina ya uyoga mtamu sana, ambao unapikwa pamoja na kuku mwitu.

Kwenye msitu wa mianzi wa Yunding, vitu wanaoangalia watu ni mianzi, chakula wanachokula ni vichipukizi vya mianzi, hata mashua wanazojiburudisha nazo pia zilitengenezwa kwa mianzi. Mashua za huko kwa kawaida zina urefu wa mita 9 na upana wa mita 5, kila mashua inachukua watu 20, watalii wanaweza kuzungumza, kunywa chai na kuangalia mandhari za kando mbili za mfereji. Usiku watu wanaweza kulala kwenye sehemu ya msituni, ambapo ni tofauti kabisa na hoteli za mijini. Msimamizi wa sehemu ya utalii Bw. Li Jinbao alisema,

"Kulala mlimani ni tofauti kabisa na kulala hotelini. Watu wanaweza kusikia milio ya ndege na vyura, hali hiyo inafanya watu wajione kama wako katika mazingira ya kimaumbile kabisa."