Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-05-15 14:45:59    
Barua 0513

cri
 Msikilizaji wetu Gulam Haji Karim wa S.L.P. 50 Lindi Tanzania ametuletea barua akitujulisha kuwa amepokea Kalenda ya mwaka 2007, pamoja na fomu ya maswali ya chemsha bongo kupitia anuani ya Zanzibar. Kuhusu vivutio vya mkoa wa Sichuan anasema makala ya chemsha bongo imeshasomwa, hivyo anaomba irudiwe kwa faida ya wasikilizaji ambao walikosa kusikia. Anasema anasikitika kuwa kwa miaka miwili amekosa kushiriki kutokana na kuhamia Tanzania bara. Kutokana na shughuli za biashara, anapata muda mfupi wa kupumzika.

Msikilizaji wetu huyo anaendelea kusema safari hii atajaribu kwa uwezo wake wote na ajinyakulie nafasi kama ilivyokuwa zamani, kuwa mshindi wa kwanza au wa pili au mshindi maalumu. Anasema kitu muhimu ni kurudia makala ya chemsha bongo, kila Jumapili katika sanduku la barua.

Pia anapenda kutujulisha kuwa msikilizaji wetu mwingine, Bi Khadija ambaye anashirikiana naye kusikiliza matangazo yetu amepokea kalenda yake na anapenda tupokee salamu zake. Mwisho msikilizaji wetu Gulam anapenda kutupongeza kwa kazi nzuri tunayofanya kwani anasema wanaridhika.

Tunamshukuru sana msikilizaji wetu bwana Gulam haji Karim kwa Barua yake, na kutueleza kuwa sasa yeye ni mkazi wa Lindi na sio Zanzibar tena. Tunafahamu kuwa katika miaka miwili iliyopita alikuwa kwenye pilikapilika za kuhama kutoka Zanzibar, tunafurahi pia kusikia kuwa sasa hamu yake ya kushiriki kwenye shindano la chemsha bongo na kujitahidi kupata ushindi tunamtakia kila la heri. Hapa tunapenda kuwaambia wasikilizaji wetu kuwa, kila mwaka kipindi cha chemsha bongo huandaliwa kwanza na ofisi maalum ya Radio China Kimataifa, kuhusu tarehe ya kuanzishwa kwake na tarehe ya kukamilika kwake, halafu idhaa za lugha mbalimbali za CRI ziandaae tena vipindi vya chemsha bongo, twasubiri vipindi vya chemsha bongo vya mwaka huu na kutumai vipindi hivyo vitaweza kuwasaidia wasikilizaji wetu waijue zaidi China.

Msikilizaji wetu mwengine Bw Simon Mandu S.L.P. 302 Bungoma, Kenya ametuletea barua akitupongeza kwa kazi nzuri tunayoifanya. Anasema tangu alipoanza kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya Radio China Kimataifa, ameweza kunufaika kwa elimu, burudani na vile vile habari kutoka kila upande duniani. Anasema matangazo yanapoanza yeye huwa habanduki kwenye Radio yake mpaka matangazo yanapomalizika. Pia anatoa pongezi kwa watangazaji kwa kazi nzuri, na kwa sauti zao zilizo nyororo ambazo zinamfanya msikilizaji asibanduke kwenye Radio yake wakati anasikiliza matangazo.

Anasema anasikia matangazo yetu kupitia Idhaa ya Kiswahili ya KBC, baada ya msikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili ya Radio China Kimataifa, anayeitwa Muchwangi Sakula wa Bungoma, kumtia moyo asikilize matangazo.

Mussa Emmanuel Duttu S.L.P.56, Kahama Shinyanga Tanzania ametuletea barua yake ambayo ameanza kwa kuomba kuzidi kuwa na Ushirikiano kati ya wafanyakazi na wanachama wote wa CRI katika kuendeleza msingi wa maendeleo ya Radio China Kimataifa duniani, katika mwaka 2007. Anashukuru kwa barua kutoka Radio China Kimataifa, tuliyoituma tarehe 22/12/2006 ya 1319 japokuwa ilichelewa kumfikia, lakini aliipata salama. Anasema mara ya mwisho kupata barua kutoka Radio China Kimataifa ilikuwa mwezi Juni, mwaka 2006, ilikuwa ni wakati tulipomtumia kidadisi.

Pamoja na hayo anasema kama kawaida yake amekuwa akisikiliza Radio China Kimataifa. Pia anashukuru kwa barua tuliyomtumia ambayo anasema ilikuwa na kalenda ya mwaka 2007 na karatasi ya chemsha bongo yenye maswali kumi, pamoja na baadhi ya maelezo kuhusu mkoa wa Sichuan, wenye vivutio vingi vya utalii ikiwa ni pamoja na maskani ya Panda.

Anasema barua tuliyomtumia ameisoma na kuelewa maelezo yote. Anatupongeza kwa ubunifu wa vipindi vingi, lakini anaomba kwa mwaka 2007 tuwe na mabadiliko. Anasema kwa kuboresha zaidi matangazo ya Radio China Kimataifa duniani, kama inawezekana kupata kituo na wawakilishi wa Radio China Kimataifa itakuwa vizuri sana, kwani wanahangaika sana na wakati mwingine inakuwa shida kupata mawimbi ya matangazo yetu, hivyo vipindi vingi vinapita, na inakuwa vigumu kujibu maswali mbalimbali katika vidadisi, chemsha bongo na kadhalika.

Anatuambia kuwa kwenye eneo la Kahama, katika mkoa wa Shinyanga nchini Tanzania anakoishi, sio rahisi kupata vizuri matangazo yetu ikilinganishwa na ilivyo nchi ya Kenya. Lakini anasema alifarijika sana aliposikia matangazo ya Radio China Kimataifa, mtangazaji Fadhili Mpunji akizungumza na baadhi ya wananchi wa Kenya kuhusu sikukuu ya Christmas.

Bwana Mussa Duttu pia ana maombi yake kadhaa kwetu anaomba vitabu na magazeti angalau kwa lugha ya Kiswahili kuhusu Historia ya China, ili apate msaada wa kujibu maswali. Anaomba Kalenda, Ratiba ya vipindi vyote vya Radio China Kimataifa, pamoja na masafa ya mawimbi mafupi na mawimbi ya FM ili aweze kupata matangazo vizuri. Ombi lake jingine ni kuhusu kupata picha inayoonesha mandhari nzuri ya kituo cha Radio China Kimataifa, na picha ya wafanyakazi wa Radio China Kimataifa. Anaomba kutumiwa picha hiyo ili aweze kuwafahamu wafanyakazi hao kwani kuwasikia kwenye Radio tu anasema haitoshi. Ombi lake la mwisho ni kuwa kama kuna vitabu vya masomo yoyote yanayotolewa na Idhaa ya Kiswahili ya Radio China Kimataifa tumtumie, kama vile kitabu cha mafunzo ya lugha ya kichina.

Tunamshukuru sana msikilizaji wetu huyu Bw Musa Emanuel Duttu kwa barua yake. Barua yake imetuonesha ufuatiliaji wake wa matangazo yetu. Tunafahamu kuwa kwenye baadhi ya maeneo mkoani Shinyanga matangazo yetu hayasikiki vizuri, lakini juhudi zinaendelea ili kuyafanya matangazo yetu yasikike vizuri zaidi katika siku za baadaye.

Msikilizaji wetu mwingine Jackline Andeyo Savala S.L.P. 64 Mautuma, Kenya. ametundikia barua akisema anatupongeza kwa kipindi chenye mafunzo,kwani anafuraha sana akiwa mmoja wa wasikilizaji kuona matanazo yetu yameendelea kuwa na mafunzo mengi.Pia anaomba tumtumie kadi ili aweze kupata wasikilizaji wengi.

Mwisho anapenda kuwashukuru wasikilizaji kwa maoni waliyonayo na kuendelea kuyapongeza matangazo yetu kuwa yanatia for a na yana mpangilio,mafunzo. Pia anawaomba watangazaji wanaotangaza waendelee hivyo hivyo.

Na vile vile anaomba wasikilizaji wafuatao tuwatumie kadi ili waweze kutoa maoni yao zaidi.

Vincet Angaya, Mautuma,Violet Ajema, Hellen Iganihizu, Mauline Vuguzza, Lylone Mangala na Polet Masitsa.

Tunamshukuru sana msikilizaji wetu Jackline Andeyo Savala na wasikilizaji wetu wenzake, ni matumaini yetu kuwa mtaendelea kusikiliza vipindi vyetu na kutoa maoni na mapendekezo yenu ili kutusaidia kuboresha vipindi vyetu.

Idhaa ya kiswahili 2007-5-15