Uchaguzi wa bunge la Algeria unafanyika tarehe 17 mwezi wa Mei, lakini tarehe 16, siku moja kabla ya uchaguzi huo, mlipuko ulitokea mjini Constantine, mashariki mwa Algeria, polisi mmoja aliuawa na wengine wawili kujeruhiwa. Katika siku hiyo kikosi kimoja kilipokuwa kikifanya doria mkoani Al-Madye kilishambuliwa kwa mabomu, askari wawili walijeruhiwa vibaya. Katika siku za karibuni mashambulizi ya kigaidi yamekuwa yanatokea mara kwa mara, hali hiyo imeleta wingu jeusi kwa uchaguzi wa bunge unaofanyika tarehe 17.
Tarehe 16 waziri wa mambo ya ndani wa Algeria Bw. Noureddine Yazid Zerhouni alitoa taarifa akishutumu magaidi kujaribu kuharibu uchaguzi wa bunge na utaratibu wa demokrasia nchini Algeria. Kwenye taarifa yake alisisitiza kuwa jibu zuri kwa mashambulizi hayo ni kuwa wananchi wa Algeria wajitokeze kwa wingi kushiriki kwenye uchaguzi. Alisema serikali imechukua hatua ili kuhakikisha uchaguzi unafanyika salama.
Tokea mwezi Oktoba mwaka jana, milipuko ilitokea mara nyingi kutokana vikundi vya kigaidi nchini Algeria kushirikiana na kundi la "al-Qaida". Mwezi Septemba mwaka jana, vikundi kadhaa vya kigaidi vya Algeria vilijiunga na kundi la Al-Qaida na kuunda kundi la Maghrebu, AQIM, na kuwa tawi muhimu la Kundi la Al-Qaida katika sehemu ya Maghrebu, kaskazini magharibi mwa Algeria.
Kadiri uchaguzi ulivyokuwa unakaribia, mapambano kati ya serikali na magaidi yalizidi kupamba moto siku baada ya siku. Tarehe 14 kituo cha televisheni cha Al jazeera kilitangaza hotuba ya kiongozi wa kundi la Maghrebu Bw. Abu Musaab Abdulwudud, kwenye hotuba yake Bw. Abdulwudud aliwataka watu wa Algeria wakatae uchaguzi wa bunge. Ni dhahiri kuwa hotuba yake ni tishio kwa watu watakaoshiriki kwenye uchaguzi huo na kuuharibu uchaguzi huo.
Vyama mbalimbali vya kisiasa vilitoa taarifa na kusema kwamba wito wa kundi la AQIM hautazuia watu wa Algeria kushiriki kwenye uchaguzi. Chama cha Utamaduni na Demokrasia, Chama cha Harakati za Amani ya Jamii na Chama cha Ukombozi wa Taifa vilitoa taarifa kwa nyakati tofauti kuwahamasisha wananchi wajitokeze kushiriki kwenye uchaguzi.
Ili kuhakikisha uchaguzi unafanyika bila matatizo, vyombo vya usalama vya Algeria vimechukua hatua za kuimarisha usalama mjini Algiers, kila kituo cha kupigia kura kinalindwa, na askari polisi wametapakaa kote mjini. Pamoja na hayo, kwenye barabara muhimu vimewekwa vikwazo na kuongeza askari polisi. Kabla ya hapo, tarehe 14 jeshi la Algeria lilifanya operesheni kabambe dhidi ya vikundi vya ugaidi vilivyojificha katika mkoa wa Tizi Ouzou, mashariki mwa Algiers, na liliwaua magaidi 17 akiwemo kiongozi muhimu wa kundi al Maghreb, AQIM. Katika siku hiyo jeshi la usalama la Algeria liliwaua wanachama sita wa kundi la Al-Qaida.
Kutokana na makadirio ya serikali ya Algeria, watu zaidi ya milioni 18 watajitokeza kupiga kura katika siku ya uchaguzi tarehe 17, kuwachagua wabunge 389, watu wanafuatilia sana jinsi hali itakavyokuwa kwenye uchaguzi huo.
Idhaa ya kiswahili 2007-05-17
|