Rais George W. Bush wa Marekani tarehe 17 Mei alikuwa na mazungumzo na waziri mkuu wa Uingereza Tony Blair kwenye Ikulu ya Marekani, ambapo wamesisitiza uhusiano wa ushirika kati ya Marekani na Uingereza, na kutetea sera ya nchi hizo mbili kuhusu Iraq.
Kwenye Mkutano na waandishi wa habari uliofanyika baada ya mazungumzo hayo, rais Bush alisema yeye na Blair walijadili masuala kuhusu Iraq, Iran, Afghanistan, amani ya mashariki ya kati na Darfur ya Sudan, na wana msimamo wa pamoja kuhusu masuala mengi. Rais Bush alisema, Blair ni rafiki yake mzuri. Na Bw Blair alisema Uingereza itaendelea kuwa mshirika mtiifu wa Marekani katika mapambano dhidi ya ugaidi, masuala kuhusu Iraq, Afghanistan na mengineyo.
Kuhusu suala la Iraq Rais Bush na Bw Blair wameshikilia kuwa, kuanzisha vita vya Iraq na kudumisha kuwepo kwa jeshi nchini Iraq ni uamuzi sahihi, na hawasikitishwi na uamuzi wao. Bwana Blair alisema, hivi sasa hali ya Iraq bado ni ya wasiwasi na changamoto zilizoko ni kubwa, lakini dalili ya kuboreshwa kihalisi kwa hali zinaonekana. Rais Bush alifurahi kusema, Ikulu ya Marekani na Bunge linalodhibitiwa na chama cha democratic zitaafikiana kuhusu suala la kutenga fedha za vita, ili kutoa fedha za matumizi kwa vitendo vya jeshi la Marekani nchini Iraq na Afghanistan.
Kuhusu suala la Iran pande hizo mbili zimesisitiza kuwa zina misimamo ya pamoja, ambapo Rais Bush na Bw Blair wanaona kuwa, Iran hairuhusiwi kumiliki silaha za nyuklia, kwani Iran kumiliki silaha za nyuklia hakulingani na maslahi ya amani ya dunia. Wameonya kuwa kama Iran itaendelea kutekeleza mpango wake wa nyuklia, Marekani na Uingereza zitalihimiza Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa lipitishe hatua mpya za kuiwekea vikwazo Iran.
Pande hizo mbili pia zilijadili masuala kuhusu nishati na kuongezeka kwa hali ya joto duniani. Kwa kuwa Bw Blair alimfuata Rais Bush katika suala la vita dhidi ya Iraq, hivyo uungaji mkono wake kutoka kwa wananchi wa Uingereza umepungua kwenye kiwango cha chini kabiti katika historia. Ili kubadilisha hali hiyo, Bw Blair anataka kuihimiza serikali ya Bw Bush itoe ahadi kuhusu utoaji wa hewa ya carbon dioxide. Safari hii katika mazungumzo kati yake na Rais Bush, Bw Blair alidhihirisha kuwa, Marekani na Umoja wa Ulaya zote zinafuatilia suala la usalama wa nishati, na anatumai kuwa pande zote zitafikia makubaliano kuhusu suala la kuongezeka kwa hali joto kote duniani. Na Rais Bush anaona suala hili linatakiwa kuzingatiwa kwa makini.
Bwana Blair alitangaza kuwa hatashika tena wadhifa wa waziri mkuu wa Uingereza kuanzia tarehe 27 Juni, hivyo hii ni mara yake ya mwisho kuitembelea Ikulu ya Marekani akiwa waziri mkuu wa Uingereza, ndiyo maana ziara hiyo inachukuliwa kuwa ni ziara yake ya kuagana kisiasa na Bush ambaye ni mshirika wake wa jadi na rafiki yake binafsi. Bw Blair pia alijaribu kutumia fursa hiyo kutetea msimamo wake wa kuifuata serikali ya Bush siku zote katika vita dhidi ya Iraq na masuala mengine makubwa ya kimataifa, kama anataka kuwaoneshea wananchi wa Uingereza kuwa, kudumisha uhusiano maamlum na Marekani siyo jambo baya kwa Uingereza. Na Rais Bush pia anaelewa sana hisia za "ndugu yake mtiifu", kwenye mkutano na waandishi wa habari, Rais Bush alisema, Bw Blair ni rafiki yake mzuri ambaye ni mwanafikra wa mkakati mwenye mantiki safi. Kuhusu uhusiano kati ya Marekani na Uingreza baada ya Bw Blair kuondoka kazini, Bw Blair ameeleza matumaini yake kuwa pande hizo mbili zitaendelea na uhusiano wa washirika ulio wa kudumu, na zitadumisha ushirikiano katika mapambano dhidi ya ugaidi, masuala kuhusu nishati, kuongezeka kwa hali joto duniani na suala la Afrika.
Vyombo vya habari vinaona kuwa, kwa kuwa Bw Blair ataondoka kazini kuanzia tarehe 27 Juni, ambapo Rais Bush atapoteza mshirika wake mwenye msimamo imara zaidi katika jukwaa la siasa la kimataifa, hali hii italeta hali isiyojulikana kwa uhusiano kati ya Uingereza na Marekani. Baada ya Bw Blair kuondoka madarakani, huenda waziri wa fedha wa Uingereza Bwana Gordon Brown atakuwa waziri mkuu wa Uingereza. Na kutokana na Bw Blair kumfuata Rais Bush kuanzisha vita na kupoteza uungaji mkono nchini Uingereza, hivyo baada ya kushika wadhifa, huenda Bw Brown atakaa mbali kidogo na Rais Bush, na hataweza kumfuata Rais Bush kila mara kama alivyofanya Bw Blair.
|