Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-05-21 15:54:10    
Mchoraji na sufii wa dini ya Buddha Shi Guoliang

cri

Bw. Shi Guoliang mwenye kuvaa joho la dini ya Buddha ni mchoraji maarufu nchini China. Maishani mwake licha ya kufanya utafiti kuhusu ubuddha alikuwa anatumia wakati wote kuchora picha, na yeye pia ni profesa mwalikwa wa vyuo vikuu kadhaa.

Bw. Shi Guoliang mwenye umri wa miaka 51 ni mchoraji mkubwa wa picha zilizoonesha maisha ya binadamu, alichora picha nyingi za watu wa kawaida ikiwa ni pamoja na wakulima wanaovuna mazao, mwanamke wa kijijini anayeshona nguo akiwa na kuku aliowafuga na wauzaji wa nyama katika soko. Picha hizo zinaonesha vilivyo maisha ya kila siku.

Bw. Shi Guoliang alipenda kuchora picha toka alipokuwa mtoto. Katika miaka ya 70 ya karne iliyopita, kwa nyakati tofauti alijifunza uchoraji kwa wachoraji wa picha za mtindo wa Kichina Bi. Zhou Sicong na Bw. Huang Zhou. Tofauti na picha za mtindo wa Kimagharibi, picha za mtindo wa Kichina zinachorwa kwa wino na brashi ya kuandikia kwenye karatasi maalum, michoro michache kwenye picha inaonesha vilivyo hali hali ya kitu kilichochorwa. Walimu hao wawili walikuwa ni hodari wa kuchora picha za watu. Alipowakumbuka marehemu walimu wake alisema,

"Nilipata bahati nzuri ya kufundishwa na wachoraji wakubwa walipokuwa hai, na wamenisaidia kuwekea msingi imara wa uchoraji, hadi sasa najipongeza kutokana na bahati yangu."

Bw. Shi Guoliang alisema, kutokana na kuelekezwa na wachoraji wakubwa, kiwango chake cha uchoraji kiliinuka haraka. Mwishoni mwa karne iliyopita, Bw. Shi Guoliang alijiungana na Chuo Kikuu cha Uchoraji cha China kuendelea na sanaa yake kwa kina. Katika muda alipokuwa chuoni alifanya maonesho ya picha alizochora mara nyingi, akaibuka na akawa maarufu. Mwishoni mwa miaka ya 80 alihamia Canada, huko alijifunza uchoraji wa mtindo wa Kimagharibi kwa miaka karibu kumi. Kutokana na upweke katika nchi ya nje alikuwa sufii wa dini ya Buddha. Mwaka 1995 kwenye tafrija alikutana na sufii mmoja wa dini ya Buddha ambaye alimwambia anaonekana kama sufii mwaminifu wa dini ya Buddha. Bw. Shi Guoliang alisema,

"Kwenye tafrija yule sufii alisema yote niliyokuwa nayo moyoni mwangu, ilikuwa karibu nitokwe na machozi, kwani wakati huo niliona upweke mkubwa. Kutokana na kutofahamu lugha, nilikuwa sina marafiki, kwa hiyo nilitamani kuishi maisha ya usufii."

Mwaka 1995 Bw. Shi Guoliang alikuwa sufii halisi, na tokea hapo amekuwa na hadhi mbili, moja ni sufii, nyingine ni mchoraji.

Katika historia ya uchorani nchini China kulikuwa na wachoraji wengi walioamini dini ya Buddha, lakini wengi wao walikuwa ni wachoraji wa mandhari ya milima na mito na picha za waumini wakubwa wa dini ya Buddha. Tofauti na picha hizo, picha alizochora Bw. Shi Guoliang huonesha upendo na wema wa binadamu. Alisema yeye amekuwa mfuasi wa dini, na anatumai kutoa mchango wake kwa ajili ya kueneza upendo katika jamii. Alisema,

"Nimekuwa sufii, lakini sikuwa sufii kwa ajili ya kujinasua kutoka kwenye usumbufu, bali ni kwa ajili ya kuwanasua watu wengi kutoka kwenye usumbufu. Ukitaka kueneza upendo wako ni lazima ukumbuke yale yanayokusumbua na uwajibike kuonesha na kueneza upendo miongoni mwa watu."

Bw. Shi Guolian mara nyingi anakwenda Tibet kuchora picha za waumini wa dini ya Buddha. Alisema alipoona waumini jinsi walivyopiga magoti kila baada ya hatua kadhaa anasisimka sana. Nyumbani kwake kuna picha moja inayowaelezea waumini hao wakiwa na sura za utulivu na amani.

Wataalamu wanaona kuwa Bw. Shi Guoliang ni hodari wa kuonesha hisia za watu kwa picha zake. Watu wanapoangalia wanavutiwa sana na wanajikuta kama wako pamoja na watu waliochorwa kwenye picha.

Bw. Shi Guoliang pia ni mtu wa kwanza kupambana na picha za bandia katika nyanja ya uchoraji. Katika biashara ya picha za mnada, picha moja iliyoigwa ilipigwa mnada kwa bei ya picha halisi aliyochora, alikasirika sana na baadaye kwenye mtandao wa internet alionesha picha aliyochora na ile bandia. Bw. Shi Guoliang alisema, "Bidhaa bandia zinaumiza watu wema, nikiwa sufii nina wajibu wa kupambana na mambo mabaya na kueneza mambo mema."

Idhaa ya kiswahili 2007-05-21