Spika wa bunge la umma la China Bwana Wu Bangguo ambaye yuko ziarani nchini Misri tarehe 20 alipotembelea kiwanda cha kutengeneza ndege aina ya K-8E kilichoko sehemu ya kusini ya Cairo, alitumai kuimarisha ushirikiano kati ya China na Misri katika sekta ya usafiri wa ndege.
Ndege aina ya K-8E ni ndege za kutoa mafunzo zenye teknolojia ya kisasa zinazohitajiwa kwa dharura na jeshi la anga la Misri. Mwishoni mwa mwaka 1999, kampuni inayoingiza na kuuza teknolojia ya usafiri wa ndege ya China na wizara ya ulinzi ya Misri zilisaini mikataba ya aina mbalimbali kuhusu kushirikiana kutengeneza ndege za kutoa mafunzo aina ya K-8E, kuanzisha mstari wa kuunda ndege nchini Misri, kituo cha kufanya utafiti wa ndege na kutoa huduma za jumla kwa ndege. Hadi kufikia sasa kiwanda cha kutengeneza ndege aina ya K-8E kimeshakabidhi ndege 81 kwa jeshi la anga la Misri. Kushirikiana kutengeneza ndege aina ya K-8E ni mmoja wa miradi ya ushirikiano wa kimkakati kati ya China na Misri katika karne ya 21, hivyo unaungwa mkono sana na serikali za nchi hizo mbili. Mwenyekiti wa jumuiya ya viwanda ya Arabic ya Misri AOI Bwana Hamdi Wahib katika sherehe ya kumkaribisha spika Wu Bangguo alitoa risala akisema:
"Tunamshukuru spika Wu Bangguo kwa kutembelea kiwanda cha ushirikiano cha ndege aina ya K-8E. Kiwanda hicho kinaonesha hali halisi ya uhusiano mzuri wa kisiasa kati ya Misri na China. Ndege aina ya K-8E zimefikia kiwango cha juu duniani, na kukidhi mahitaji ya jeshi la anga la Misri. Tunatarajia kupanua ushirikiano na makampuni ya China katika uzalishaji wa bidhaa za matumizi ya kiraia na kijeshi."
Meneja mkuu wa kampuni ya pili ya viwanda vya usafiri wa ndege ya China Bwana Zhang Hongbiao alisema, kampuni hiyo siku zote inafuata kanuni ya kutilia maanani sifa ya bidhaa na kufuata ahadi. Alisema:
"Katika miaka ya karibuni, sekta ya usafiri wa ndege nchini China imepata maendeleo makubwa. Naamini kuwa siku zijazo China na Misri zitaimarisha zaidi ushirikiano katika eneo la usafiri wa ndege. Tulikuwa tumefanya ushirikiano mzuri, na tutaendelea kuzidisha ushirikiano kati yetu."
Bw. Wahib na waziri wa uwekezaji wa Misri Bw. Mahmoud Mohieddin walimwambatana na spika Wu Bangguo katika kutembelea karakana za kukuunganisha ndege aina ya K-8E. Kabla ya kuondoka kiwandani, spika Wu Bangguo alisema:
"China na Misri zina msingi mzuri wa kufanya ushirikiano katika kuunda ndege aina ya K-8E, hivi sasa suala linalotukabili ni namna ya kuzidisha ushirikiano kati yetu. Yaani ushirikiano wa kuunda ndege aina ya Xiaolong, ndege hiyo imefanyiwa marekebisho ya kiteknolojia, na inasifiwa sana na rais Musharaf wa Pakistan. Uhusiano kati ya China na Misri ni uhusiano wa kimkakati, na ushirikiano katika kuzalisha bidhaa za matumizi ya kijeshi ni sehemu muhimu ya ushirikiano kati yetu, hivyo natumai kuwa Misri itafanya juhudi za kuunga mkono ushirikiano huo ."
|