Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-05-21 16:19:47    
Kutembelea vijiji vya mji wa Jian, mkoani Jiangxi

cri

Hivi sasa ni majira ya Spring nchini China, ambapo hali ya hewa inaanza kubadilika kuwa joto, na maua yanachanua, ikiwa unataka kuitembelea China hivi sasa, basi ni vizuri utembelee kwenye sehemu ya vijiji ya mji wa Jian, mkoani Jiangxi. Kwenye sehemu ya vijiji ya mji wa Jian, si kama tu utaweza kushiriki kwenye shughuli za kilimo shambani na kushiriki kwenye mashindano ya mbio ya mashua, bali pia unaweza kuonja vitoweo vyenye umaalumu wa sehemu ya vijiji.

Kijiji cha Meipo ni maarufu zaidi kwenye sehemu ya vijiji ya Jian. Kijiji hicho chenye eneo la kilomita za mraba 1 hivi kiko kusini mashariki mwa mji wa Jian. Ingawa kijiji cha Meipo si kijiji kikubwa, lakini kimeshakuwa na historia ya zaidi ya miaka 800. Kwenye njia ya kuingia kwenye kijiji cha Meipo kuna lango kubwa lililojengwa kwa aina ya mawe meupe ya marumaru, kwenye sehemu ya juu ya lango hilo kumeandikwa maneno makubwa ya Meipo.

Wakazi wa kijiji cha Meipo karibu kila siku wanafanya maonesho ya mchezo unaoitwa "Caiqing". Wachezaji wa mchezo huo wote ni watoto wa kijijini, ambao wanavalia mavazi ya wahusika wa drama mwilini pamoja na vinyago usoni, wakijifanya kama ni watu mashuhuri kwenye historia ya China au ni wahusika wa michezo ya drama. Miguu ya wachezaji imefungwa kwenye fremu za mbao zinazobebwa na wanakijiji wanaotembea katika muziki uliopigwa na bendi ya kijijini, huku watoto wachezaji wakifanya maonesho. Bibi Park Zung Shoo kutoka Korea ya Kusini alivutiwa na maonesho ya mchezo, alisema,

"Sikutarajia kuona mchezo mzuri wa "Caiqing" katika kijiji cha Meipo! Licha ya mchezo huu, hapa pia kuna mahekalu ya jadi ya kuabudu mizimu ya mababu-jadi pamoja na mtaa wa kale, ambavyo ni utamaduni wa kale wa China. Hapa pia nimeona sura ya vijiji vya enzi za Ming na Qing za China, ambayo inanivutia sana. Ninaipenda sana sehemu hiyo, nitawaeleza marafiki zangu na kuwataka watembelee kijiji hicho."

Kijiji cha Meipo kinachukuliwa kama ni "jumba la makumbusho ya vijiji vya kale vya sehemu ya kusini mwa China", katika kijiji hicho kuna nyumba 503 pamoja na mahekalu 19 ya kale yaliyohifadhiwa vizuri, mbali na hayo kijijini pia kuna majumba 8 ya kale ya kusomea pamoja na lango moja kubwa la kale. Kwenye sehemu ya kaskazini mwa kijiji cha Meipo kuna mtaa wa kale wenye umbo la "S" na urefu wa mita karibu 1,000, ambao ulijengwa kabla ya miaka mia tano au mia sita iliyopita. Upana wa mtaa huo ni mita tatu hivi, na ulijengwa kwa mawe. Wazee wa huko wanasema, mtaa huo ulikuwa na shughuli nyingi za biashara, na ulikuwa na maduka mengi, ambayo wakati fulani yalikuwa zaidi ya 100. Hata hivi sasa kwenye kuta za majengo hayo, watu bado wanaweza kuona baadhi ya maneno ya matangazo ya biashara yakiwemo "Mchele" na "Mafuta".

Wakati watalii wanapotembelea mtaa wa kale wa kijiji cha Meipo, licha ya kuvutiwa na majengo ya zamani, wanataka kujua tofauti wanayoona kuishi ndani yake. Mwaka huu kijiji cha Meipo kimejanga nyumba za wageni zaidi ya 10 zinazofanana na majengo ya kale ya huko nje kidogo na kijiji cha Meipo, mpango huo licha ya kuweza kutosheleza mahitaji ya watalii, tena unaweza kudumisha mazingira ya kale ya kijijini. Bw. Liang Xingfa ni mkazi wa kijiji hicho, alisema kujenga nyumba za wageni nje ya kijiji ni wazo zuri.

"Kujenga nyumba za wageni nje ya kijiji kwa mpango kunachangia kuhifadhi sura ya kijiji cha kale, pia kunanufaisha uendeshaji wa shughuli zake."

Kijiji cha Luzhou ni kijiji kingine chenye umaalumu katika utalii. Kijiji hicho kiko kwenye kisiwa cha Luzhou, eneo la kijiji hicho ni kilomita za mraba elfu 45, watu wakitaka kufika huko wanapaswa kutumia mashua. Gati la kisiwa cha Luzhou ni jengo la kale lenye ujia mrefu, watalii wanaweza kusubiri mashua wakikaa kwenye viti vya mawe vilivyoko kwenye ujia, huku wakiangalia mandhari nzuri.

Asilimia 80 ya kisiwa cha Luzhou ni misitu ya kimaumbile pamoja na michenza, ufukwe wa kisiwa hicho una urefu wa kilomita 3.5 wenye mchanga mweupe na nyembamba, ambao ni mahali pazuri kuogelea. Kusafiri kwa mashua kutoka kisiwa hicho kuelekea upande wa magharibi, baada ya kupita mto mmoja ni mahali palipojengwa jengo la kijeshi zaidi ya miaka 800 iliyopita. Jengo hilo la kijeshi linajulikana kwa "Dianjiangtai" ni mahali, ambapo zamani za kale jemadari alichagua askari na viongozi wao kabla ya kwenda kupigana vita sehemu ya nje; kwenye sehemu ya mtiririko wa chini ya mto kuna jumba la makumbusho, ambalo vinaoneshwa vyombo vya shaba nyeusi vya zaidi ya miaka 3,700 iliyopita; kwenye kando ya kaskazini mwa mto ni tarafa maarufu ya kale inayoitwa "Maziwa Matatu", ambayo inazalisha machenza matamu ya aina ya "kanzu nyekundu" yenye maganda membamba, machenza ya aina hiyo yalikuwa matunda maalumu yanayotumiwa tu na wafalme na jamaa zao. Hivi sasa, kijiji cha Luzhou hufanya "tamasha ya machenza ya Luzhou" katika mwezi Oktoba kila mwaka wakati machenza yanapokomaa.

Watalii wanapotembelea kijiji cha Luzhou, huvutiwa na shughuli za mchezo wa jadi wa mbio ya mashua. Mashua zinazotumika katika mchezo ni zenye umbo la dragon. Mtalii Bw. Gong Jianyu alitoka mkoa unaojiendesha wa Mongolia ya ndani ulioko kaskazini mwa China, aliyekuwa ametoka kwenye mashindano ya mbio ya mashua, alifurahi sana na kusema,

"Katika mbuga kubwa ya kwetu hakuna shughuli hizo za kilimo, hususan mchezo wa mashua, leo nimefurahi sana."

Katika kijiji cha Luzhou, watalii licha ya kuweza kufanya shughuli za kilimo za kupandikiza miche ya mpunga, kuchimba vichipukizi vya mianzi na kuchuma matunda pori, pia wanaweza kushiriki shughuli za jadi zikiwemo sherehe ya harusi na kupika chakula porini.

"Heil, Mical, njooni haraka mnisaidie kuchimba, Lina ametuzidi. Usituangalie huko, njoo kijana. Hii ni ya kufurahisha zaidi. Nina uhakika kuwa utapenda mchezo huu!"

Bw. Eric Clapp kutoka Canada alicheza kwa furaha, huku akifanya shughuli za kilimo, huku akimwita mwenzake. Hivi sasa mbali na watalii kutoka sehemu nyingine za China, watalii wengi kutoka nchi za nje pia wanapenda kufanya matembezi kwenye sehemu ya vijiji karibu na mji wa Jian.

Katika mji wa Jian, mbali na vijiji vya Meipo na Luzhou, kuna vijiji vingine vyenye mandhari nzuri ya kimaumbile na mabaki ya kale vinavyowavutia watalii. Utalii kwenye sehemu ya vijiji ya mji wa Jian unawavutia watalii wengi wa nchini na wa nchi za nje, ambao wanaburudishwa sana na milima na mito ya kupendeza, hali isiyo na kelele za vijijini pamoja na jadi na desturi za asili.

Idhaa ya kiswahili 2007-05-21