Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-05-22 10:30:25    
Supamaketi zaanzisha katika vijiji vingi nchini China

cri

    

Zamani nchini China kulikuwa na usemi mmoja unaohusu njia ya kununua bidhaa kwa wakulima, yaani "kununua viungo kwenye vijiji vyao, kununua vitu kwa matumizi ya kila siku kwenye magulio, na kununua bidhaa kubwa katika miji ya wilaya". Usemi huo unaonesha hali halisi ilivyokuwa kuhusu upungufu wa bidhaa kwenye maduka vijijini. Mwaka 2005 wizara ya biashara ya China ilianzisha mradi wa kuzihimiza makampuni yanayomiliki supamaketi kuanzisha matawi yao vijijini. Baada ya juhudi za miaka miwili, supamaketi ambazo zinaonekana hapa na pale mijini sasa zimeanzishwa kwenye vijiji vingi, na zimewanufaisha wakulima kihalisi.

Katika sehemu ya milimani ya wilaya Xianyou mkoani Fujian kusini mashariki mwa China, kuna kijiji kimoja kiitwacho Yunfeng. Zamani wanakijiji wa kijiji hicho wakitaka kununua vitu kwa matumizi ya kila siku, walipaswa kwenda mji wa wilaya ambako ni kilomita 60 kutoka kwenye kijiji hicho. Hivi sasa hali hiyo imebadilika, wanakijijini wanaweza kununua vitu vingi kwenye supamaketi kijijini humo kwa kutembea dakika chache tu.

Mwandishi wetu wa habari aliona kuwa supamaketi hiyo yenye eneo la mita za mraba 150 inauza vinywaji, matunda, vyombo vya umeme n.k. Bw. Yang Shicai aliyenunua vitu kwenye supamaketi hiyo alisema,

"Bei za bidhaa zinazouzwa hapa ni nafuu, sifa za bidhaa pia ni nzuri. Naweza kununua vitu vingi vinavyotumiwa nyumbani hapa."

Bidhaa zinazouzwa kwenye supamaketi hiyo zinanunuliwa na kuletwa hapa na kampuni kuu iliyoko wilayani Xianyou, hivyo bei za bidhaa ni nafuu kuliko zile zinazouzwa katika maduka ya watu binafsi, pia sifa za bidhaa zinazouzwa hapa ni nzuri zaidi.

Kuna supamaketi nyingi katika miji mikubwa ya China, lakini kununua vitu kwenye supamaketi bado ni jambo jipya vijijini. Baadhi ya supamaketi vijijini zinatoa huduma za kuagiza bidhaa na kuzipeleka nyumbani. Licha ya kuuza bidhaa kwa matumizi ya kila siku, supamaketi kadhaa zinatoa huduma pekee kwa wakulima, zikiwemo kuuza bidhaa kwa uzalishaji wa kilimo, na kuwaalika wataalamu wa kilimo kutoa mapendekezo kwa wakulima.

Mabadiliko hayo yanatokana na mradi mmoja wa masoko ulioanzishwa na serikali ya China, ambao unalenga kuwasaidia wakulima wengi zaidi kununua bidhaa nzuri kutoka kwenye maduka yaliyo karibu na nyumba zao. Serikali ya China inauita mradi huo "mradi wa masoko kwenye maelfu ya vijiji". Waziri wa biashara wa China Bw. Bo Xilai alipoeleza mradi huo alisema,

"Mradi huo unalenga kuwawezesha wakulima wanunue bidhaa nzuri, pia unaweza kuongeza matumizi ya fedha vijijini. Kutokana na mradi huo supamaketi laki 1.6 zimejengwa nchini kote, na mwaka huu zitafikia laki 2.5 ambazo zitakapakaa kwenye asilimia 75 ya wilaya nchini China. Mwaka jana mradi huo uliongeza matumizi ya fedha yuan bilioni 60 vijijini, na inakadiriwa kuwa mwaka huu utaongeza matumizi ya fedha yuan bilioni 85."

Takwimu zinaonesha kuwa thamani ya matumizi ya fedha kwa wakulima ambao wanachukua asilimia 70 ya idadi ya watu wa China inachukua theluthi moja tu ya matumizi ya fedha ya jamii nzima. Ili kubadilisha hali ya hivi sasa ya kusukuma mbele maendeleo ya uchumi kwa uwekezaji na mauzo ya bidhaa katika nchi za nje, kazi muhimu ya kufanya mageuzi ya utaratibu wa kiuchumi nchini China ni kuongeza matumizi ya fedha, hasa matumizi ya fedha vijijini,.

Katika miaka mingi iliyopita, mapato ya wakulima yalikuwa ni madogo, hii ni sababu kubwa iliyozuia matumizi ya fedha vijijni. Ili kuboresha maisha ya wakulima vijijini, serikali ya China imefuta kodi ya kilimo, kuimarisha ujenzi wa miundo mbinu vijijini zikiwemo barabara, zana za utoaji wa maji, mtandao wa umeme na mawasiliano ya habari, pia imeongeza fedha kwa ajili ya maendeleo ya sekta za elimu, utamaduni na afya vijijni. Kutokana na mafanikio ya sera hizo, uwezo wa kununua vitu wa wakulima umeinuliwa.

Lakini hivi sasa maduka madogo ya watu binafsi vijijini hayawezi kukidhi mahitaji ya wakulima. Aidha, kuna uwezekano wakulima wanaweza kununua bidhaa bandia. Uchunguzi uliofanyiwa na wizara ya biashara ya China unaonesha kuwa, asilimia 74 ya wakulima wamewahi kununua bidhaa bandia, hasa mbegu, dawa za kuwaua wadudu na mbolea za kemikali. Katika hali hiyo, kuanzisha supamaketi vijijini si kama tu kutasaidia kuinua kiwango cha maisha ya wakulima, bali pia kutasaidia kuzuia kuingia kwa bidhaa bandia sokoni.

Kuanzishwa kwa upamaketi vijijini kumekuwa ni shinikizo kwa maduka ya watu binafsi, hivyo mameneja wa maduka hayo wanajiandaa kushiriki kwenye mafunzo ya usimamizi wa maduka na uchukuzi wa bidhaa kwa pamoja, ili kuyafanya maduka yao yawe matawi ya supamaketi kubwa.

Katika mji wa Nanning mkoani Guangxi, duka la mwanakijiji Lei Jinqing lilishiriki kwenye mfumo wa supamaketi mwishoni mwa mwaka jana. Hivi sasa supamaketi yake imekuwa duka linalopendwa zaidi na wanakijiji. Bw. Lei alisema serikali ilimpatia ruzuku ya karibu yuan elfu 10 ili kupamba duka lake. Ananunua bidhaa nzuri zinazoweza kuaminika, na bidhaa za aina mbalimbali zinawekwa kwenye maduka tofauti, hivyo mauzo ya bidhaa yameongezeka.

"Mapato ya kila siku katika duka langu yameongezeka kwa mara moja kuliko zamani, zamani niliweza kupata yuan elfu moja hivi kwa siku, na sasa naweza kupata yuan elfu mbili."

Hivi sasa tatizo kubwa kwa supamaketi vijijini ni faida. Inakadiria kuwa kama ya vitega uchumi ni sawasawa, faida zinazopatikana kwenye supamaketi za vijijini ni theluthi moja ya zile za mijini. Miundo mbinu iliyo nyuma na gharama kubwa za uendeshaji wa maduka vijijini ni kikwazo kwa kuanzisha mfumo wa supamaketi vijijini.

Ili kutatua matatizo hayo, serikali ya China inatenga fedha kwa ajili ya maendeleo ya supamaketi vijijini. Kuanzia mwaka 2005, serikali kuu ya China ilitenga yuan milioni 500, na benki ya maendeleo ya taifa ya China ilitoa mikopo yuan bilioni 10.

Wizara ya biashara pia inasukuma mbele mtandao wa uchukuzi vijijini kushirikiana na "mradi wa masoko kwenye maelfu ya vijiji", na kuanzisha mtandao wa uchukuzi wa bidhaa vijijini. Supamaketi zinaweza kununua mazao ya kilimo yakiwemo mayai na mboga kutoka kwa wakulima, na kuongeza uzalishaji wa kilimo kutokana na mahitaji ya bidhaa sokoni. Hatua hizo zimewasaidia wakulima kuongeza mapato yao.

Hivi sasa supamaketi zinazoshiriki kwenye "mradi wa masoko kwenye maelfu ya vijiji" zinaongeza matawi yao vijijini. Lakini huu bado ni mwanzo wa kazi ya kuendeleza masoko vijijini. Waziri wa biashara wa China Bw. Bo Xilai alisema,

"Tunajenga mtandao wa uchukuzi wa mazao ya kilimo, yaani kujenga masoko 100 makubwa ya uuzaji wa jumla. Aidha tutaendeleza makampuni 100 ya uuzaji wa jumla wa mazao ya kilimo, halafu tutaendeleza masoko elfu 2 kwenye sehemu mbalimbali ili yawe masoko ya kisasa yenye utaratibu mzuri."