Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-05-22 18:43:13    
Spika Wu Bangguo aeleza kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi kati ya makampuni ya China na Afrika

cri

Spika wa bunge la umma la China Bwana Wu Bangguo ambaye yuko ziarani nchini Misri tarehe 21 alihudhuria mkutano wa ushirikiano kati ya makampuni ya China na Afrika uliofanyika huko Cairo. Kwenye mkutano huo spika Wu Bangguo alitoa hotuba iitwayo "Tuandike kwa pamoja ukurasa mpya wa ushirikiano kati ya China na Afrika". Kwenye hotuba yake, alidhihirisha kuwa, ushirikiano wa makampuni unapaswa kuzingatiwa zaidi katika ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara kati ya China na nchi za Afrika.

Mwezi Novemba mwaka 2006, viongozi wa nchi 48 za Afrika walihudhuria mkutano wa wakuu wa baraza la ushirikiano kati ya China na Afrika uliofanyika mjini Beijing, rais Hu Jintao wa China alitangaza hatua zinazochukuliwa na serikali ya China za kuimarisha ushirikiano kati yake na Afrika katika miaka mitatu. Spika Wu Bangguo alifahamisha hali ya utekelezaji wa hatua hizo. Akisema:

"Hivi sasa China imesaini makubaliano ya msaada na nchi 17 za Afrika, makubaliano ya kutoa mikopo yenye riba nafuu na nchi 6 za Afrika, na kusaini makubaalino na nchi 14 za Afrika kuhusu kufuta madeni yaliyodaiwa, shughuli za kufuta madeni 81 ya nchi 19 za Afrika zitakamilika mwaka huu. Bidhaa za nchi zilizo nyuma kabisa kimaendeleo za Afrika zinazosamehewa ushuru nchini China zimeongezeka kufikia aina 440 kutoka zile za 190."

Spika Wu Bangguo alisema, ushirikiano wa kiuchumi kati ya China na nchi za Afrika una mustakabali mzuri, aliyapendekeza makampuni ya China na Afrika yaimarishe ushirikiano katika kilimo, ujenzi wa miundo mbinu, utafutaji, uchimbaji na matumizi ya madini na nishati, na uzalishaji wa nguo, na kuhimiza ushirikiano katika miradi mikubwa.

Mwenyekiti wa shirikisho la wanaviwanda na wafanyabiashara wa Afrika Bwana Mohamed El Masry katika hotuba yake alitathmini vizuri umuhimu wa mkutano wa wakuu wa baraza la ushirikiano kati ya China na Afrika, kusifu sana hatua nane zilizotolewa na serikali ya China kuhusu kuimarisha ushirikiano kati yake na Afrika na juhudi inazozifanya China. Alisema:

"Leo tunakutana hapa kwa ajili ya kusukuma mbele maendeleo ya uhusiano wa kimkakati na kiwenzi kati ya China na Afrika, na kuhimiza ongezeko la biashara ya pande mbili. Naamini kuwa ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara kati ya China na Afrika katika sekta mbalimbali hakika utaleta manufaa mengi. Pande mbili za China na Afrika zitafanya juhudi kwa pamoja ili kupata maendeleo ya uchumi na usitawi katika eneo lenye theluthi moja ya idadi ya watu duniani na kukabiliana kwa pamoja na changamoto zilizotokea duniani."

Spika wa bunge la Misri Bw. Ahmed Fathy Sorour alisisitiza kuwa, ziara hii ya spika Wu Bangguo nchini Misri itasukuma mbele ushirikiano kati ya mabunge ya nchi hizo mbili. Alisema:

"Tuna imani kubwa kwa mustakabali wa ushirikiano kati ya China na Misri, ifikapo mwaka 2012 China itakuwa mshirika wa kwanza wa kibiashara wa Misri. Misri itaendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji ili kuvutia uwekezaji kutoka nje."

Bw. Sorour alisema, Misri itatoa mchango kama ilivyokuwa katika kuimarisha ushirikiano kati ya China na Afrika.

Maofisa waandamizi wa Misri, wajumbe wa nchi mbalimbali za Afrika nchini Misri na wanakampuni 500 kutoka nchi zaidi ya 40 za Afrika na China walihudhuria mkutano huo.