Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-05-24 19:12:41    
Soko la pamoja la mashariki na kusini mwa Afrika lapiga hatua za maendeleo kwenye utandawazi wa uchumi.

cri

Wasikilizaji wapendwa, mkutano wa 12 wa wakuu wa nchi wa soko la pamoja la mashariki na kusini mwa Afrika, ulifungwa tarehe 23 huko Nairobi, mji mkuu wa Kenya. Mkutano huo ulipitisha mpango wa kuanzisha umoja wa ushuru wa forodha wa mashariki na kusini mwa Afrika kabla ya mwishoni mwa mwaka 2008, hatua ambayo inaonesha umoja huo wa uchumi wa kikanda, ambao unachukua nafasi ya kwanza kwa ukubwa barani Afrika, umepiga hatua moja kwa kuelekea katika lengo la utandawazi wa uchumi wa kanda hiyo.

Kwenye sherehe ya ufungaji wa mkutano siku hiyo, mwenyekiti wa baraza la uratibu la soko la pamoja la mashariki na kusini mwa Afrika, ambaye ni waziri wa biashara na viwanda wa Kenya, Bw. Mukhisa Kituyi, alisoma taarifa ya mkutano wa 12 wa wakuu wa nchi wa soko la pamoja la mashariki na kusini mwa Afrika.

"Mkutano wa wakuu wa nchi unakariri ahadi ya kuanzisha umoja wa ushuru wa forodha wa soko la pamoja la mashariki na kusini mwa Afrika, tarehe 8 mwezi Desemba mwaka 2008, ambapo kiasi cha ushuru wa bidhaa zinazoagizwa na nchi wanachama wa umoja huo kutoka nchi nyingine zisizo wanachama wa umoja huo, kitakuwa cha namna moja, mali-ghafi na bidhaa za uzalishaji mali na utoaji huduma zitasamehewa ushuru, bidhaa za mwanzo zitatozwa ushuru kwa 10% wakati bidhaa kamili zitatozwa kwa 25%. Mkutano wa wakuu wa nchi, pia unakubali kuboresha biashara ya utoaji huduma, kwani biashara ya utoaji huduma ina uwezo mkubwa, ambao bado haujatumika, katika kukuza maendeleo ya uchumi wa nchi wanachama."

Soko la pamoja la mashariki na kusini mwa Afrika ni umoja wa uchumi ulio mkubwa zaidi katika Afrika, ambao ulianzishwa mwezi Desemba mwaka 1993, na hadi hivi sasa umekuwa na nchi wanachama 20. kutokana na maagizo ya mkataba wa umoja huo, eneo la biashara huria na umoja wa ushuru wa forodha vitaanzishwa kwa vipindi mbalimbali, na kuanzisha umoja wa sarafu ili hatimaye kutimiza utandawazi wa uchumi wa kanda hiyo.

Mwezi Okatoba mwaka 2000, umoja huo ulianzisha eneo la biashara huria la soko la pamoja la mashariki na kusini mwa Afrika, ambalo ni eneo la kwanza la biashara huria katika bara la Afrika. Hivi sasa, eneo hilo la biashara huria limetimiza miaka 7 tangu lianzishwe, lakini ni nchi 13 tu kati ya nchi wanachama 20 wa umoja huo, ambazo zimejiunga nalo. Bw. Kituyi alisema,

"Mkutano wa wakuu wa nchi unaridhika na ongezeko la mfululizo na la kasi la biashara kati ya nchi wanachama wa umoja huo, na unapongeza uamuzi wa nchi wanachama wa kuondoa vikwazo vilivyowekwa kuhusu ushuru wa forodha. Mkutano wa wakuu wa nchi unahimiza nchi wanachama, ambazo bado hazijajiunga na eneo la biashara huria zijiunge nalo kabla ya mwezi Desemba mwaka 2008, yaani kabla ya kuasisiwa umoja wa ushuru wa forodha." Sababu zilizofanya baadhi ya nchi, ambazo hazijajiunga na eneo la biashara huria, ni kukosa uliingano katika maendeleo ya uchumi na jamii kwa nchi wanachama hao, ambao uwezo wao wa kuhimili changamoto zinazoletwa na utandawazi ni wa viwango mbalimbali. Mbali na hayo, baadhi ya nchi wanachama wa soko la pamoja la mashariki na kusini mwa Afrika, hivi sasa pia ni nchi wanachama wa umoja wa uchumi wa kanda nyingine za bara la Afrika. Kushiriki katika umoja wa uchumi mbalimbali pia ni kitu kinachokwamisha maendeleo ya uchumi wa soko la mashariki na kusini mwa Afrika.ili kutatua matatizo hayo, viongozi wa nchi wanachama walikuwa na majadiliano marefu kwenye muda wa mkutano huo, na hatimaye waliamua kuanzisha mfuko wa fedha wa maendeleo ya kanda hiyo. Mkutano wa wakuu wa nchi unatoa wito wa kutaka nchi wanachama wake waidhinishe haraka mfuko huo wa fedha na wanufaike pamoja kutokana na mfuko huo wa fedha.