Jeshi la ulinzi la Israel alfajiri ya tarehe 24 liliwakamata maofisa 33 wa kundi la Hamas kwenye ukingo wa magharibi wa Mto Jordan, kati ya maofisa hao alikuwapo waziri mmoja. Sambamba na hayo, migogoro ya kisilaha kati ya jeshi la Israel na vikundi vyenye silaha vya Palestina inaendelea kwenye sehemu ya Gaza, pande zote mbili zinakataa kusimamisha vita, mapambano ya kutumia silaha kati ya Palestina na Israel yatakuwa makali.
Mke wa waziri wa elimu Bw. Naser al-Shaer aliyekamatwa na jeshi la Israel alisema siku hiyo alfajiri askari wa Israel walikuja kwa ghafla kwenye makazi yao mjini Nablus, wakamkamata Shaer pamoja na kompyuta yake, licha ya Bw. Shaer, pia waliwakamata maofisa wengine 32 wakiwemo meya na naibu meya wa mji wa Nablus.
Baadaye jeshi la Israel lilitoa taarifa ikishutumu kundi la Hamas kuunga mkono na kuhamasisha "vitendo vya ugaidi" kwa kutumia madaraka ya serikali. Waziri wa ulinzi wa Israel Shimon Peres, kwenye hotuba yake, pia alitetea msako huo wa jeshi la Israel, alisema "kuwakamata ni bora kuliko kuwaua kwa risasi, msako huo ni ishara kwa vikundi vyenye silaha, kwamba ni lazima visimamishe mara moja kurusha makombora kuishambulia Israel."
Serikali na maofisa wa kundi la Hamas walishutumu vikali msako huo. Msemaji wa waziri mkuu Ismail Haniyeh wa serikali ya Palestina Bw. Ghazi Hamad, aliitaka Israel iwaachie huru maofisa waliokamatwa. Alisema, msako huo utaizamisha kanda ya Mashariki ya Kati kwenye mzunguko wa kulipiza kisasi, na Israel ni lazima ibebe matokeo yoyote yatakayotokea. Pamoja na hayo vikundi vyenye silaha vya kundi la Hamas pia vilitoa taarifa ikiahidi kuendelea kuifyatulia Israe makombora.
Kutokana na hali hiyo ambayo migogoro inazidi kuwa mikubwa, maoni tofauti yametokea ndani ya uongozi wa Palestina kuhusu suala la kusimamisha vita dhidi ya Israel. Mwenyekiti wa mamlaka ya Palestina Bw. Mahmoud Abbas, kiongozi wa kundi la Hamas ambaye pia ni waziri mkuu Bw.Ismail Haniyeh tarehe 23 walikutana kwenye sehemu ya Gaza, kujadili suala la kusimamisha vita, lakini mkutano wao haukufanikiwa chochote. Tarehe 24 baada ya kukutana na mwakilishi wa Umoja wa Ulaya, anayeshughulikia mambo ya nje na sera za usalama Bw. Javier Solana, Bw. Abbas alisema, vikundi vyenye silaha vya Palestina ni lazima visimamishe mashambulizi ya makombora ili kusimamisha vita kati ya Palestina na Israel. Lakini kundi la Hamas linataka Israel likubali kusimamisha kwanza vita kwenye ukanda wa Gaza na kwenye ukingo wa magharibi wa mto Jordan. Afisa mwandamizi wa kundi la Hamas Bw. Mahmoud al-Zahar alisema, msako wa jeshi la Israel kwenye ukingo wa magharibi wa mto Jordan unamaanisha kuwa ombi la Abbas la kutaka kusimamisha vita "halina maana yoyote", alisema mradi tu ukaliaji wa Israel unaendelea, vikundi vyenye silaha vya Palestina vitaendelea kuirushia Israel makombora, na alimshutumu Abbas "kutotaka kupambana" na "kwenda kinyume na maoni ya pamoja ya watu wa Palestina".
Hivi sasa Israel pia haina nia ya kusimamisha vita. Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Israel Bw.Mark Regev alisema, kama usimamishaji wa vita ukiweza kupatikana katika sehemu ya Gaza, basi Israel itafikiria kuueneza usimamishaji huo kwenye ukingo wa magharibi wa mto Jordan, lakini tatizo ni kuwa watu wenye silaha wa Palestina hawakuwahi kusimamisha vita katika sehemu ya Gaza.
Mpaka hivi sasa, mapambano mapya ya kisilaha yameendelea siku kumi, mashambulizi ya angani ya Israel yamesababisha karibu watu 50 wa Palestina kupoteza maisha, na wengi wao ni raia wa kawaida. Watu wenye silaha wa Palestina wameifyatulia Israel makombora karibu 200, katika muda wa wiki mbili na kusababisha watu wengi kujeruhiwa, na mtu mmoja kupoteza maisha. Kutokana na kuwa pande mbili zote zinakataa kusimamisha vita, pengine mgogoro utakuwa mkubwa zaidi.
Idhaa ya kiswahili 2007-05-25
|