Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-05-29 14:52:56    
Sehemu ya katikati ya China kuwa sehemu mpya inayofuatiliwa na wafanyabiashara wa nchi za nje

cri

Maonesho ya pili ya uwekezaji na biashara ya sehemu ya katikati ya China yalifanyika mwezi uliopita mjini Zhengzhou mkoani Henan, China, ambapo makampuni zaidi ya 300 yaliyoingia kwenye safu ya makampuni 500 yenye nguvu kubwa duniani, yakiwemo Microsoft, Metro na Carrefour yalishiriki kwenye maonesho hayo. Sehemu ya katikati ya China imekuwa ni sehemu mpya inayofuatiliwa na wafanyabiashara wa nchi za nje.

Sehemu ya katikati ya China ni pamoja na mikoa sita ya Shanxi, Anhui, Jiangxi, Henan, Hubei na Hunan, sehemu hiyo ina eneo la kilomita za mraba milioni 1.028, na idadi ya watu wa sehemu hiyo ni milioni 360. Sehemu hiyo ina maliasili nyingi na idadi kubwa ya watu, ambayo iko kwenye sehemu muhimu ya mawasiliano, na vilevile ni sehemu muhimu ya uzalishaji na usafirishaji wa nafaka, nishati na vifaa vya raslimali. Katika miaka ya hivi karibuni, mafanikio makubwa yamepatikana katika maendeleo ya uchumi kwenye mikoa mbalimbali ya sehemu hiyo.

Mkuu wa ofisi ya uchumi ya ubalozi wa Indonesia nchini China Bw. Arifianto Sofiyanto alishiriki kwenye maonesho hayo. Alisema hii ni mara yake ya kwanza kutembelea sehemu ya kati ya China, na wakati alipoona maendeleo ya mji wa Zhengzhou alishangaa sana, hakudhani kuwa sehemu hiyo imeendelezwa vizuri namna hii. Ingawa meya wa mji wa Schwerin wa Ujerumani Bw. Norbert Claussen ametembelea mji wa Zhengzhou mara ya tatu, lakini mabadiliko mapya ya Zhengzhou pia yalimshangaza. Mara hii alikuja China kwa ajili ya kuhimiza mradi wa ushirikiano kati ya uwanja wa ndege wa mji wa Schwein na uwanja wa ndege wa Zhengzhou. Mkalimani wake Bibi Zhang Peiyan alimwambia mwandishi wetu wa habari kuwa, Bw. Claussen alisifu sana mazingira ya uwekezaji ya sehemu ya katikati ya China. Alisema,

"Mara tu Bw. Claussen aliposhuka kutoka kwenye ndege aliniambia kuwa, mji wa Shanghai umeendelezwa kwa kasi, imekuwa mji mkubwa, na kiwango chake cha viwanda ni cha hali ya juu. Lakini miji ya sehemu ya katikati sio mikubwa wala midogo, ni ya wastani na bado haijaendelezwa sana, hivyo ina fursa ya kufanya miradi mikubwa."

Ikilinganishwa na sehemu nyingine, sehemu ya katikati ya China ina nguvu zake katika sekta fulani. Kwa mfano, gharama ya nguvu kazi ya sehemu hiyo ni asilimia 60 hivi ya sehemu ya mashariki ya China. Sehemu hiyo ina maeneo mengi yenye sifa bora, na ardhi inayoweza kutumika kwa ajili ya viwanda pia ni mara 1.4 kuliko sehemu ya mashariki ya China. Hivyo wawekezaji wengi wa nchi za nje wanatupia macho sehemu hiyo.

Kampuni ya Metro ya Ujerumani ni moja ya kampuni kubwa kabisa duniani ya biashara ya bidhaa za rejareja. Meneja mkuu wa idara inayoshughulikia mambo ya nje ya tawi la kampuni hiyo nchini China Bw. Huang Zhongjie alimwambia mwandishi wetu wa wa habari kuwa, kwa makampuni makubwa ya kimataifa ya biashara ya bidhaa za rejareja, bidhaa za sehemu ya kati ya China ni nzuri tena zina bei nafuu, hii inasaidia kuinua ushindani wa kampuni kwenye soko. Alisema,

"Sehemu ya katikati ya China hasa kama mikoa ya Henan na Hunan ni mikoa inayozalisha mazao mengi ya kilimo, ambayo ina maliasili nyingi za kilimo na vyakula vingi vya aina mbalimbali. Kupitia maonesho hayo, tunataka kufanya ushirikiano wa moja kwa moja na wakulima wa sehemu hiyo katika vyakula vya nyama, mboga na matunda."

Habari zinasema, kwenye maonesho hayo mikataba ya miradi iliyosainiwa katika mazungumzo ya ununuzi wa makampuni makubwa ya kimataifa ni yenye thamani Yuan za RMB milioni 850, na miradi ya kuvutia mitaji iliyotangazwa na wafanyabiashara wa China na nchi za nje kuhusu utengenezaji wa mitambo, vipuri vya magari, nishati, maliasili, utalii na nyinginezo ilikuwa zaidi ya elfu 10.

Bibi Zhu Jie kutoka kampuni ya Capel ya Chile alimwambia mwandishi wetu wa habari kuwa, shughuli muhimu za kampuni yake ni uuzaji wa mvinyo, na inataka kutafuta wafanyabiashara wanaofaa kufanya biashara ya uuzaji wa mvinyo katika sehemu ya kati ya China kupitia maonesho hayo. Anaamini kuwa soko la sehemu ya kati ya China lina mustakabali mzuri. Akisema:

"Mvinyo ni kinywaji maarufu katika nchi za nje, lakini nchini China, hasa katika sehemu ya kati ya China, watu bado hawajazoea kunywa mvinyo, hivyo kuna soko kubwa hapa, kwa kuwa katika sehemu hiyo ukinywa chupa moja ya mvinyo kwenye mkahawa wa kimagharibi utalipa Yuan za RMB mia mbili au tatu hivi."

Mwezi Aprili mwaka jana, China ilianza kutekeleza rasmi mkakati wa taifa kuhusu "kujiendeleza kwa sehemu ya katikati". Hadi hapo, kujitokeza kwa sehemu ya kati na uendelezaji wa sehemu ya magharibi, kustawisha sehemu ya kaskazini mashariki na kuharakisha maendeleo ya sehemu ya mashariki kumekuwa mkakati kamili wa maendeleo ya uchumi wa kisehemu wa China. Meneja wa mauzo ya shirika la ndege la Ying la Indonesia Bw. Xing Qiang aliona kuwa, utekelezaji wa mkakati wa China ni fursa nzuri kwa maendeleo ya sehemu ya kati. Alisema:

"Kwa kuwa hivi sasa tumeanzisha masoko ya Beijing, Shanghai na Guangzhou, na tunajua uchumi wa sehemu ya mashariki ya China umeendelezwa, hivyo mkakati wa China unafuatilia sehemu ya katikati na sehemu ya magharibi ya China hatua kwa hatua. Tukiwa shirika la ndege la kigeni, sisi pia tunataka kutafuta wageni wengi zaidi katika sehemu ya katikati na sehemu ya magharibi ya China."

Licha ya kueleza hamu yake kubwa kwa sehemu ya katikati ya China, Bw. Xing Qiang pia alitoa maoni yake za dhati kuhusu sehemu ya katikati. Alisema lipo pengo kati ya sehemu ya katikati na sehemu ya pwani ya mashariki, kwa mfano mitizamo ya huduma wa watu wa huko kuhusu utoaji wa huduma na utalii bado vinatakiwa kuimarishwa zaidi.

Waziri wa biashara wa China Bw. Bo Xilai kwenye maonesho hayo alisema, jiografia pekee ya sehemu ya katikati ya China, mawasiliano rahisi, mazingira mazuri ya uwekezaji na maliasili nyingi za kimaumbile zinaifanya sehemu hiyo iwe na uwezo mkubwa wa soko. Katika miongo kadhaa ijayo, wafanyabiashara wa nchi za nje watakuwa na fursa nzuri kabisa kujiendeleza katika sehemu hiyo.

Idhaa ya kiswahili 2007-5-29