Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-05-29 16:40:18    
Barua 0527

cri

Msikilizaji wetu Mubarouk Msabah wa sanduku la posta 52483 Dubai United Arab Emirates ametuletea barua pepe akisema, ni jambo la kufurahisha na kutia moyo sana baada ya Jamhuri ya watu wa China kufaulu kurusha satelaiti ya mawasiliano kwa ajili ya Nigeria hivi karibuni.

Anasema satelaiti hiyo ya Nigeria ijulikanayo kwa jina la Nigcosmat-1 iliyorushwa kwa msaada wa China, itaweza kusaidia sana kutumika kwa mawasiliano ya internet barani Afrika, jambo ambalo kwa maoni yake anadhihirisha wazi kwa vitendo na nia njema ya Jamhuri ya watu wa China katika kuliendeleza bara la Afrika, chini ya ushirikiano mpya.

Anasema bila shaka yoyote mataifa ya Afrika yataweza kunufaika vyema na ukuuaji wa teknolojia na maendeleo ya kiuchumi yaliyofikiwa na China, ili waafrika waweze kufikia kiwango kizuri cha maendeleo duniani kulingana na mataifa mengi, pamoja na kujikwamua katika matatizo yao mbalimbali. Ni matumaini yake makubwa kuwa mwanzo huu mpya utakuwa na mustakabali mzuri kwa bara la Afrika hapo baadaye.

Na katika barua yake pepe nyingine Bwana Mbarouk alisema, angependa kuchukua nafasi hii kuuungana na wasikilizaji wenzake wote nchini Kenya katika kuomboleza vifo vya raia wa nchi hiyo, pamoja na nchi nyingine za Kiafrika pamoja na raia wa China vilivyotokana na ajali ya ndege ya Shirika la ndege la Kenya hivi karibuni nchini Cameroon. Tunawatakia malazi mema peponi wale wote waliopoteza maisha yao na kuwapa subira wale wote walioondokewa na ndugu zao kutokana na ajali hiyo.

Tunamshukuru sana Bwana Mbarouk Msabah kwa barua yake ya kueleza maoni yake kuhusu habari aliyopata kutoka katika matangazo ya idhaa yetu ya Kiswahili ya Radio China Kimataifa, habari hiyo imetutia moyo watu wote na kuwa na matarajio makubwa kuhusu umuhimu wake kwa mawasiliano kwenye mtandao wa internet barani Afrika, na maendeleo ya kisayansi na kiteknolojia ya Bara la Afrika katika siku za usoni.

Msikilizaji wetu Mogire O. Machuki wa Kisii Kenya ametuletea barua pepe anasema yeye pamoja na Philip M.Machuki na Mabeya Machuki wa Kisii Kenya kwa ushirikiano wanawatakia heri na baraka watu wafuatao: Kefa O Gichana wa Kisii Kenya, Ouma Samwel wa Iganga Uganda, Francis N.Mose wa Eldoret Kenya, James Bosire Makori wa Nyamira, Willim Mekenye Nyambono na Bi.Jane Kerubo Mekenye wakiwa Keroka Kenya.

Ras Franz Manko Ngogo wa Tarime Mara Tanzania, Onesmo H.Mponda, Kilulu Kulwa, Bob Shega wa Shega, Zakaria Ndemfoo, Mtoto Happyness Julius, Liz Richie, Kaziro Dutwa, Husserin Mirachi, Paroko wa Paroko, Mchana J.Mchana, Emmanuel S.Kapera wote wakiwa Tanzania, mwisho kwa Mbarouk Msabah wa Dubai. Ujumbe wake unasema, anawatakia kila la kheri maishani.

Msikilizaji wetu Hillary K.Kirui wa sanduku la posta 42422 Nairobi Kenya ametuletea barua akisema kuwa, salamu nyingi ziwafikie wafanyakazi wote wa Radio China Kimataifa walioko Beijing, China, yeye ni mzima hapo chuoni K.I.M.C Nairobi Kenya. Pongezi kwa vipindi vyetu murua ambavyo mbali na kuelimisha, huburudisha.

Anasema ana hamu kubwa ya kujifunza Kichina, hivyo anaomba endapo tunayo CD zinazotoa mafunzo hayo tumtumie. Aidha, nyimbo za kale za wachina zina mahadhi yanayomburudisha sana, hivyo anaomba pia kama itawezekana tumtumie CD zenyewe. Anauliza, je, majibu yake ya chemsha bongo yametufikia? Lini tutatangaza washindi? . Anasema atatushukuru sana tukimfanyia hisani hii.

Tunamshukuru Bwana Hillary K.Kirui kwa barua yake ambayo imetuelezea hamu yake ya kujifunza Kichina. Hapa tunaweza kumwambia kuwa, kutokana na makubaliano kati ya Radio China Kimataifa na Ofisi ya uenezaji wa lugha ya Kichina ya China, Darasa la Confucius la kujifunza Kichina litaanzishwa siku chache baadaye huko Nairobi Kenya, baada ya kuzinduliwa rasmi kwa darasa hilo, wasikilizaji wenye hamu wakiwasiliana na Kituo cha waandishi wa habari wa Radio China kimataifa huko Nairobi Kenya, watapata nafasi ya kujifunza Kichina kwenye darasa hilo, ambapo watapewa vitabu vya mafunzo. Na suala lake jingine kuhusu chemsha bongo, tunapenda kumwambia kuwa, hakika jibu lake limewasilishwa hapa Idhaa ya Kiswahili ya Radio China Kimataifa, na matokeo ya mwisho hakika yatajulikana kwa kupitia matangazo yetu kwenye kipindi hiki cha Sanduku la barua. Ni matumaini yetu kuwa ataendelea kusikiliza vipindi vyetu kwa makini na kutoa maoni na mapendekezo ili kutusaidia kuboresha zaidi vipindi vyetu.

Na msikilizaji wetu Martin Wekesa Wanyama ambaye barua zake huhifadhiwa na Alfred W. Wanami wa sanduku la posta 903 Bungoma Kenya ametuletea barua pepe akisema, yeye amefurahishwa na huduma tunazotoa kwa wasikilizaji wetu yeye akiwa mmoja wao. Hakika mtindo tunaotumia kwa kuwaelimisha ama kutoa mafunzo ya Kichina ni wa hali ya juu kwa sababu unawavutia wasikilizaji wasikilize na kujifunza Kichina, ambapo, pia hawataki kipindi kiwapite.

Anasema pia anafurahia matangazo yetu ya habari za duniani zinazowavutia. Anasema matangazo ya Radio China Kimataifa yanawaunganisha wasikilizaji wa sehemu mbalimbali duniani kwa kupitia salamu na habari ambazo zimemfanya hata kuwa na tamaa ya kuja China. Na vilevile ametazama vipindi vya runinga vinavyovutia mno hasa vipindi vile kuhusu desturi za China, utamaduni, uzalendo na vingine vingi kuhusu China vimefanya ajiandikishe rasmi kuwa shabiki mkuu kutoka magharibi mwa Kenya. Hongera sana kwa matangazo ya Radio China Kimataifa, natarajia mtaongeza vipindi na muda wa matangazo.

Tunamshukuru sana Bwana martin Wekesa Wanyama kwa barua yake inayotutia moyo kwamba tunaona juhudi zetu zinawafurahisha wasikilizaji wetu. Na kuhusu mafunzo ya Kichina, tutajitahidi kuboresha kipindi cha kujifunza Kichina kwa ajili ya wasikilizaji wetu.

Msikilizaji wetu Dominic Nduku Muholo wa sanduku la posta 397 Kakamega Kenya, ametuletea barua akisema kuwa, salamu zake zimewafikia wafanyakazi wote wa Radio China Kimataifa na wananchi wote wa Jamhuri ya watu wa China na kuwatakia amani na ufanisi wa kimaendeleo katika mwaka huu wa 2007.

Anatushukuru kwa zawadi tulizomtumia zikiwemo kalenda ya mwaka wa 2007, kadi za salamu na zawadi nyingine.

Anasema kwa hakika wanapata usikivu mzuri zaidi radioni kwa kupitia katika mawimbi ya masafa ya kati na mafupi ya Radio China Kimataifa. Pia anashukuru hatua ambazo zimechukuliwa na Radio China Kimataifa za kushughulikia wasikilizaji wake kwa wakati.

Anatoa maoni kuhusu chemsha bongo, angependa wawe wakipata kidadisi baada ya muda mfupi kwa sababu inawachemsha bongo kweli kweli.

Mwisho anapenda kutaja ziara ya rais Hu Jintao wa Jamhuri ya watu wa China barani Afrika iliyomalizika tarehe 10 Februari mwaka huu, anasema ziara hiyo iliyochukua muda wa siku 10 ilikuwa ya kutembelea nchi 8 zikiwemo Sudan, Zambia, Msumbiji, Liberia, Cameroon, Shelisheli, Namibia na Afrika ya kusini, na ilichukua takriban kilomita elfu 40. Ziara hiyo ilikuwa ya kuhimiza nchi hizo na nchi nyingine barani Afrika kuachana na mizozo ya ndani na ya kimataifa na badala yake wawe watulivu na kuwa amani, baadaye watapata maendeleo ya kiuchumi katika nchi zao.

Na mwisho anatutakia kila la heri kwa mwaka huu wa 2007.

Tunamshukuru kwa dhati Bwana Dominic Nduku Muholo kwa barua yake ya kuelezea usikivu wake wa matangazo yetu na maoni yake kwa vipindi vyetu. Ni matumaini yetu kuwa tutadumisha mawasiliano na urafiki kati yetu.