Mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje wa nchi za Asia na Ulaya tarehe 28 ulimalizika katika mji wa bandari Hamburg, kaskazini mwa Ujerumani. Mapema katika siku hiyo waziri mpya wa mambo ya nje wa China Bw. Yang Jiechi alikutana na mawaziri wa nchi tatu muhimu za Umoja wa Ulaya, nao ni waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Bw. Steinmeier, mjumbe wa Kamati ya Umoja wa Ulaya anayeshughulikia mambo ya nje Bi. Waldner na mwakilishi mwandamizi wa Umoja wa Ulaya anayeshughulikia mambo ya nje na sera za usalama Bw. Solana. Vyombo vya habari vinaona kuwa mkutano wa waziri wa mambo ya nje wa China na mawaziri wa nchi hizo tatu umeonesha tumaini na nia ya China na nchi za Umoja wa Ulaya kutaka kupandisha uhusiano wao kwenye ngazi mpya.
Kwenye mazungumzo, waziri wa mambo ya nje wa China Bw. Yang Jiechi na mawaziri wa nchi tatu, walibadilishana maoni kuhusu mabadiliko ya hali ya hewa duniani, usalama wa nishati, mapambano dhidi ya ugaidi, suala la nyuklia la Iran na suala la Iraq. Pande mbili ziliafikiana katika mambo mengi na zimezidi kuelewa misimamo ya kila upande. Bw. Yang Jiechi alisema,
"Viongozi wakuu wa pande mbili wanazidi kutembeleana, mazungumzo ya kisiasa yameongezeka katika ngazi tofauti na yamepata matokeo mazuri, maingiliano na ushirikiano kati ya pande mbili katika biashara yanazidi kuimarika na kupanuka." Bw. Yang Jiechi alisema, pande mbili zimeafikiana kimaoni katika mambo mengi kuhusu masuala mazito ya kimataifa na pande mbili zinafurahia hali ya uhusiano, na kusema zitaendeleza uhusiano huo kwa mtazamo wa mbali na wa kimkakati.
Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Bw. Steinmeier alisema,
"China na Umoja wa Ulaya zimeafikiana katika mambo mawili muhimu. La kwanza, ni lazima kuishinikiza zaidi Iran ili kuifanya iridhishe matumaini na matakwa ya jumuyia ya kimataifa kuhusu suala la nyuklia; Pili, pande mbili zimekubaliana kutatua suala la nyuklia la Iran kwa njia ya amani na kupinga kutumia nguvu."
Utaratibu wa mkutano wa Asia na Umoja wa Ulaya ulianzishwa mwaka 1996, nia yake ikiwa ni kujenga uhusiano wa kiwenzi wa aina mpya na wa pande zote, kuimarisha mazungumzo na kufahamu hali ya ushirikiano, ili kuleta mazingira mazuri ya kuendeleza uchumi na kudumisha amani na utulivu duniani. Hivi sasa kuna nchi wanachama 45, zikiwemo nchi za Ulaya 27, nchi 10 za Umoja wa Asia ya Kusini Mashariki, China, Japan na Korea ya Kusini.
Zikiwa nchi muhimu katika uchumi duniani, China na nchi za Umoja wa Ulaya zinasaidiana kisiasa na kuridhishana mahitaji ya kiuchumi. Umoja wa Ulaya ni mwenzi wa kwanza wa kibiashara wa China na China ni mwenzi wa pili wa kibiashara wa Umoja wa Ulaya.
Mwezi Januari mwaka huu, Umoja wa Ulaya ulitangaza rasmi kuanzisha mazungumzo kuhusu makubaliano ya kuanzisha ushirikiano wa kiwenzi. Mjumbe wa Kamati ya Umoja wa Ulaya, anayeshughulikia mambo ya nje Bi. Waldner alipotaja sherehe ya kuanzisha mazungumzo kuhusu ushirikiano wa kiwenzi kati ya China na Umoja wa Ulaya, yaliyofanyika mjini Beijing alisema,
"Makubaliano kati ya China na Umoja wa Ulaya yameziletea pande mbili majukumu mengi, na makubaliano hayo ni matokeo ya pamoja dhidi ya changamoto duniani, zikiwa ni pamoja na biashara, mabadiliko ya hali ya hewa duniani na mazungumzo na nchi za Afrika. Kwa pande mbili, makubaliano ya ushirikiano wa kiwenzi kati ya pande mbili ni chombo muhimu cha kupanua wigo wa ushirikiano."
Mwakilishi mwandamizi anayeshughulikia mambo ya nje na sera za usalama Bw. Solana, ilikuwa mara ya kwanza kuhudhuria mkutano huo, hii inamaanisha kuwa Umoja wa Ulaya unaithamini sana China katika masuala ya kulinda utulivu na usalama wa kikanda, kulinda amani ya dunia na utatuzi wa masuala muhimu duniani. Bw. Solana alidokeza kuwa Bw. Yang Jiechi atakutana na waziri wa mambo ya nje wa Iran, ili kutafuta utatuzi wa suala la nyuklia la Iran. Alisema,
"Sisi pamoja na waziri wa mambo ya nje wa China Bw. Yang Jiechi tulifanya mazungumzo muhimu ya kimkakati. Naona ni afadhali tudumishe utaratibu huo wa mazungumzo. China ni mwezi muhimu wa ushirikiano wa kimkakati, tunaihitaji China katika utatuzi wa masuala mengi ya kimataifa. Nafurahi kubadilishana maoni na Bw. Yang Jiechi."
|