
Mkutano wa mawaziri wa mambo ya nje, wa Asia na Umoja wa Ulaya, ulimalizika tarehe 29 huko Hamburg, nchini Ujerumani. Mkutano huo umeonesha nia ya pande mbili, Asia na Ulaya, kutaka kuimarisha ushirikiano kati yao, ili kukabiliana na changamoto kwa pamoja.
Ujerumani ikiwa ni mwenyeji wa mkutano huo, ilitangaza taarifa ya mwenyekiti, ikisisitiza kuwa nchi wanachama, zinapaswa kutumia utaratibu huo wa mkutano ziimarishe zaidi mazungumzo, ili kukabili changamoto kwa pamoja. Waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Bw. Stainmeier alisema,
"Kama nchi fulani wanachama zimekuwa tayari kupambana na changamoto ya utandawazi duniani, basi nchi nyingine wanachama zinapaswa zifikirie hatua gani zichukuliwe, ili kupambana na changamoto hiyo kwa pamoja. Iwapo tunataka watu walio wengi wanufaike na mchakato wa utandawazi, mfumo wa kimataifa wenye haki na usawa, ni lazima uanzishwe, na lengo hilo haliwezi kutimizwa bila nchi za Asia kushiriki. Kwa hiyo, mazungumzo kati ya Ulaya na Asia ni muhimu sana."
Toka mwaka 1996 utaratibu wa mkutano huo uanzishwe, kiwango cha mkutano huo, kinainuka hatua kwa hatua na kupata maendeleo kadiri muda unavyopita. Hapo mwanzo, nchi wanachama, zilikuwa 26 na sasa zimeongezeka na kuwa 45. hivi sasa watu wa nchi wanachama wa mkutano wa Asia na Ulaya wanachukua 58% ya watu wote duniani, na thamani ya biashara inachukua 60% ya thamani ya biashara duniani. Mkutano ukiwa kama daraja kati ya Asia na Ulaya, umekuwa nguvu kubwa ya kiuchumi na hakika utakuwa muhimu zaidi katika mambo ya kimataifa. Waziri wa mambo ya nje wa China Bw. Yang Jiechi aliyeshiriki kwenye mkutano huo alisema,
"Kwenye mkutano huo, mawaziri wa mambo ya nje, walizungumzia na kusuluhisha misimamo kuhusu masuala ya kikanda na ya dunia, na walibadilishana maoni kuhusu kusukuma mbele mazungumzo ya kisiasa, kiuchumi na ya kiutamaduni. Hii imeonesha pande mbili, Asia na Ulaya, zinataka kuimarisha zaidi ushirikiano wao?" Bw. Yang Jiechi alisema, kutetea kuwepo kwa ncha nyingi duniani na kuimarisha maendeleo ya pamoja ni kitu muhimu sana kwa nchi wanachama wa Asia na Ulaya.
Katika siku za mkutano huo mawaziri waliohudhuria mkutano huo, walijadili kwa kina na kuafikiana kimaoni kuhusu suala la nyuklia la Iran, suala la Iraq, hali ya Mashariki ya Kati na Afghanistan, suala la kutoeneza silaha za nyuklia, mabadiliko ya hali ya hewa duniani, usalama wa nishati na mapambano dhidi ya ugaidi. Zaidi ya hayo mawaziri hao, pia walijadili na kushauriana kuhusu namna ya kufungua soko, na kupanua ushirikiano wa kibiashara. Mjumbe wa Kamati ya Umoja wa Ulaya anayeshughulikia mambo ya nje Bi. Waldner alisema,
"Kamati ya Umoja wa Ulaya itatoa misaada ya kifedha kwa nchi wanachama wa Asia. Katika muda wa miaka minne ijayo, itatoa misaada ya kifedha, inayofikia Euro milioni 775, licha ya misaada ya kiserikali, ili kuimarisha mazungumzo, kati ya Asia na Ulaya, ikiwa ni pamoja na maingiliano na mazungumzo katika mambo ya elimu, hifadhi ya mazingira, sera za nishati, utamaduni na dini."
Idhaa ya kiswahili 2007-05-30
|