Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-05-31 21:36:03    
China yachukua hatua kuwalinda watoto wa wakulima vijijini ambao wazazi wao wanafanya kazi za vibarua mijini

cri

Kutokana na maendeleo ya uchumi na jamii nchini China, wakulima wengi wa vijijini wanamiminikia mijini kutafuta kazi za vibarua, na kuwaacha watoto wao nyumbani. Takwimu zinaonesha kuwa, hivi sasa nchini China kuna wakulima zaidi ya milioni 100 wanaofanya kazi za vibarua mijini, na idadi ya watoto hao wanaobaki nyumbani imefikia milioni 20. Kutokana na kukosa elimu ya nyumbani, upendo wa wazazi na kutokuwa na usimamizi mzuri, watoto wa wakulima hao wanaoishi vijijini wanakabiliwa na matatizo ya aina mbalimbali, kama vile kuwa na mienendo mibaya, kujisikia upweke na kutopenda kwenda shule.

Naibu mkurugenzi wa kamati ya mambo yanayohusu wanawake na watoto ya baraza la serikali ya China Bi. Huang Qingyi alisema, hali ya wakulima wanaofanya kazi za vibarua mijini kwa upande mmoja imeboresha maisha ya watoto wao wanaoishi kwenye maskani yao, lakini kwa upande mwingine watoto hao pia wanakabiliwa na matatizo ya aina mbalimbali.

Serikali ya China inafuatilia sana suala la watoto hao, kwenye mkutano wa mwaka huu wa baraza la mashauriano ya kisiasa la China rais Hu Jintao aliiagiza jamii kuwatilia maanani watoto wa wakulima vibarua wanaoishi vijijini. Waziri mkuu wa China Bwana Wen Jiabao alipotoa ripoti yake kuhusu kazi za serikali alisisitiza kwa mara nyingine kushughulikia vizuri suala la elimu kwa watoto wa wakulima wanaoishi mijini au vijijini ambao wazazi wao wanafanya kazi za vibarua mijini.

Katika miaka ya hivi karibuni, China imekuwa ikichukua hatua mbalimbali kuimarisha kazi za kuwalinda na kuwaelimisha watoto hao. Kwa mfano baraza la serikali ya China limetoa mapendekezo kuhusu utatuzi wa suala la wakulima vibarua, na kuunda kikundi maalum kitakachoelekeza sehemu mbalimbali kuwashughulikia watoto hao. China imeharakisha ujenzi wa shule za bweni vijijini, ili kutatua matatizo ya elimu na maisha kwa baadhi ya watoto hao, na imeanzisha utaratibu wa uungaji mkono unaozishirikisha serikali, shule, familia na mitaa katika ngazi mbalimbali, na kufanya juhudi kuanzisha utaratibu wenye ufanisi wa kudumu wa kushughulikia mambo yanayowahusu watoto hao. Pia China imekuwa inaimarisha kazi ya kutoa maelekezo na huduma kwa elimu ya nyumbani, na kuwaelekeza na kuwaandaa wasimamizi wa watoto hao.

Mkoa wa Hunan ni moja ya mikoa ambayo wakulima wengi wanafanya kazi za vibarua kwenye mikoa mingine. Takwimu zinaonesha kuwa mkoani Hunan kuna wakulima vibarua zaidi ya milioni 12, na watoto milioni 1.6 wa wakulima hao wanaoishi vijijini. Ili kuwawezesha watoto hao kufurahia maisha ya utotoni na kupata afya nzuri kama ilivyo kwa watoto wengine, kamati zinazoshughulikia mambo ya vijana na watoto za mkoa huo zimeanzisha kwa pamoja mfuko wa kuwafuatilia watoto wa wakulima wanaoishi vijijini ambao wazazi wao wanafanya kazi za vibarua mijini, kuitaka jamii kuwafuatilia watoto hao.

Fedha zitakazochangishwa na mfuko huo zitatumiwa kwa ajili ya vifaa vya mafunzo kwa watoto hao wanaoishi vijijini, kujenga vituo vya kufanya shughuli mbalimbali kwa watoto hao, nyumba za kusomea kwa watoto hao, vyumba vya majarida vya watoto hao, kuanzisha namba maalum za simu kwa ajili ya kuwahudumia watoto hao, na kuwaandaa walimu wanaojitolea kuwafundisha watoto hao .