Tarehe 31 Mei waziri mkuu wa Uingereza Bw. Tony Blair alifika mji wa Johannesburg nchini Afrika Kusini ambapo ni kituo chake cha mwisho katika ziara yake barani Afrika na pia ni ziara yake ya mwisho katika nchi za nje. Vyombo vya habari vinasema hii ni "safari ya kuaga", na wachambuzi wanaona sababu ya Bw. Blair kuchagua Afrika kufanya ziara yake ya kuaga ni kutaka kutukuza sera zake kuhusu Afrika baada ya sera zake kuhusu Iraq kushindwa.
Kwanza, lengo la ziara yake hiyo ni kutaka kuonesha mafanikio ya sera zake barani Afrika. Mwaka 2003, kwa kushawishiwa na Tony Blair, rais wa Libya Bw. Gaddafi aliacha mpango wake wa kutengeneza silaha kali na kuahidi kupambana na ugaidi, wakati ambapo watu wa Uingereza walikuwa wakimlalamikia Tony Blair kuhusu sera zake za Iraq, ufanisi wake huo nchini Libya ulimsaidia sana kunawiri, na zaidi ya hayo amekuwa kama mfano wa kutatua masuala ya silaha za nyuklia ya Korea ya Kaskazini na Iran. Ziara ya Tony Blair nchini Libya ikiwa ni kituo cha kwanza barani Afrika ilifanywa kwa makusudi. Tarehe 29 Bw. Tony Blair alipokutana na Bw. Gaddafi alisema, "katika miaka mitatu iliyopita, uhusiano kati ya Uingereza na Libya umebadilika kabisa, na maingiliano ya kibiashara kati ya nchi hizo mbili yamekuwa mengi zaidi."
Maingiliano mazuri ya kibiashara kati ya nchi hizo mbili yameonesha kwamba Uingereza imepata faida kubwa. Mwanzoni mwa mwaka 2004, wakati ambapo muda mfupi baada ya Libya kutangaza kuacha mpango wa kutengeneza silaha kali, kampuni ya mafuta ya Shell iliyomilikiwa na Uingereza na Uholanzi ilianza mradi wa kuchimba gesi nchini Libya. Katika siku hiyo ya tarehe 29 Bw. Blair alipokutana na Bw. Gaddafi kampuni ya mafuta ya Uingereza ilitangaza kuwa kampuni hiyo imetia saini makubaliano yenye thamani ya dola za Kimarekani milioni 900 na kampuni ya mafuta ya serikali ya Libya kutafuta mafuta na gesi nchini Libya. Lakini watu wengi wa Libya wanasema, baada ya kuacha mpango wa kutengeneza silaha kali uwekezaji waliopata kutoka Magharibi umewakatisha tamaa.
Pili, Pengine Bw. Tony Blair atafanya juhudi za mwisho kuhimiza kundi la nchi nane tajiri kuisaidia Afrika kuondoa umaskini. Bw. Tony Blair kwa mafanikio alisukuma mbele jumuyia ya kimataifa, hasa nchi nane tajiri, zitupie macho umaskini barani Afrika. Mwaka 2005 kwa kutumia fursa ya Uingereza kuwa ni mwenyekiti wa zamu wa kundi la nchi nane tajiri Bw. Tony Blair alifanikisha kundi la nchi nane tajiri kutia saini mpango wa utekekezaji wa kuisaidia Afrika kuondokana na umaskini, na kuahidi kuwa hadi kufikia mwaka 2010 fedha za mpango huo zitaongezeka mara mbili yaani dola za Kimarekani bilioni 50 na kusamehe madeni ya nchi 14 zilizo maskini kabisa barani humo. Tarehe 31 Mei Bw. Tony Blair kwa mara nyingine tena alitoa hotuba kuhusu mpango huo, akisema kama nchi za magharibi hazitahakikisha misaada ya kifedha kwa Afrika, basi mchakato wa demokrasia na ustawi barani humo utakuwa hatarini, alitumaini wiki ijayo kundi la nchi nane tajiri lifanye mkutano na kwenye mkutano huo suala la Afrika lizungumzwe zaidi.
Ingawa Chansela Angela Markel wa Ujerumani, nchi ambayo kwa sasa ni mwenyekiti wa kundi la nchi nane alisema atawahimiza viongozi watimize ahadi kwa Afrika, lakini vyombo vya habari vinamtilia shaka. Kutokana maoni tofauti kati ya nchi nane tajiri pamoja na sababu za nchi za Afrika yenyewe, baadhi ya watu wanafananisha suala la kuondoa umaskini barani Afrika na "safari ndefu ya marathon, na sio mbio za mita mia moja". Ikiwa mrithi wa Blair akirudi nyuma mbele ya matatizo, basi mafanikio ya Bw. Tony Blair ya kuisaidia Afrika yatakuwa bure.
Hivi sasa ni jambo la bayana kwamba waziri wa fedha wa Uingereza atakuwa waziri mkuu baada ya Tony Blair kuondoka madarakani. Wachambuzi wanaona kuwa baada ya kushika madaraka mrithi huyo hatabadilisha sana sera za Uingereza kuhusu Afrika.
Idhaa ya kiswahili 2007-06-01
|