Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-06-01 16:53:55    
Mwalimu wa China barani Afrika

cri

Baada ya miezi miwili tangu afike nchini Zimbabwe, Bw. Xu Benyu amezoea hatua kwa hatua maisha ya huko. Bw. Xu Benyu ni kijana anayejitolea kutoka nchini China, na hivi sasa anaishi katika kituo cha ngazi ya juu cha mafunzo ya menejimenti, kilomita 20 kutoka Harare, mji mkuu wa Zimbabwe. Bw. Xu Benyu na kijana mwingine anayejitolea Bw. Hao Dongzhi wanaishi pamoja, katika nyumba yao kuna choo, ukumbi, na televisheni. Mazingira kama hayo ni mazuri kuliko shule za vijijini mkoani Guizhou.

Mwaka 2003 Bw. Xu Benyu alichaguliwa na chuo kikuu cha kilimo cha Huazhong kuwa mwanafunzi mzamili, lakini aliacha nafasi hiyo ya kujifunza zaidi katika chuo kikuu, na kwenda mkoani Guizhou kutoa msaada wa mafunzo. Baadaye wenzake waliokwenda mkoani Guizhou kutoa msaada wa mafunzo pamoja naye waliondoka kutoka mkoani Guizhou, lakini Bw. Xu Benyu alibaki huko na kushikilia jukumu la kutoa msaada wa mafunzo. Hadithi yake iliwagusa moyo watu wengi, pia iliihimiza jamii yote itilie maanani kazi ya mafunzo ya sehemu zilizo nyuma kiuchumi. Bw. Xu Benyu alichaguliwa na kituo cha CCTV kuwa "mtu aliyewagusa moyo wachina mwaka 2004."

Bw. Xu Benyu na vijana 14 wengine ni kundi la kwanza la wachina wanaojitolea nchini Zimbabwe. Katika mkutano wa wakuu wa Baraza la ushirikiano kati ya China na Afrika uliofanyika mwaka jana hapa Beijing, China iliahidi kutuma vijana 300 wanaojitolea barani Afrika. Bw. Xu Benyu aliyekuwa mwanafunzi mzamili alichaguliwa na kamati ya Umoja wa vijana wa China, na kuanza kushughulikia huduma ya kujitolea kwa mara nyingine.

Jukumu muhimu la Bw. Xu Benyu ni kuwafundisha watu wanaopenda kujifunza lugha ya kichina katika kituo cha ngazi ya juu cha mafunzo ya menejimenti. Wengi wa wanafunzi wake wana kazi zao, katika kituo hicho watapata mafunzo ya kichina kwa muda wa wiki tatu. Kabla ya mafunzo kuanzishwa rasmi, mkurugeni wa kituo hicho aliwaita wafanyakazi wote wa kituo hicho kujifunza lugha ya kichina kwa Bw. Xu Benyu. Tangu wakati huo, wafanyakazi wa kituo hicho, wanapenda kuzungumza na Bw.Xu Benyu kwa kichina.

Tarehe 16 mwezi Machi, mwalimu Xu Benyu alianza rasmi kutoa mafunzo ya lugha ya kichina. Wanafunzi wake walitoka sekta mbalimbali. Kuna vijana waliopata digrii hivi karibuni na hawajapata kazi, meneja anayeshughulikia ujenzi pamoja na wachina, na pia kuna watu wanaopanga kutalii na kufanya biashara hivi karibuni nchini China. Kati ya wanafunzi hao, kuna mwanafunzi mwenye umri wa miaka 65, yeye ni mjumbe wa utendaji wa shirika la urafiki kati ya Msumbiji na Zimbabwe. Aliwahi kuja nchini China mwaka jana, na alipata kumbukumbu nyingi juu ya vyakula vya kichina.

Wanafunzi hao wana sifa za pamoja, yaani wote wanapenda sana kujifunza kichina. Wanafunzi hao hupiga simu kwa Bw. Xu Benyu mara kwa mara, ili kufanya mazoezi ya kuongea kwa kichina.

Lakini si rahisi katika wiki tatu tu, kuwafanya wanafunzi hao wapate maendeleo makubwa kwa njia ya kawaida ya kuwafundisha kichina, hivyo Bw. Xu Benyu aliamua kutafuta njia nyingine. Alipanga mazungumzo kadhaa kwa kutumia maneno ya kichina yanayotumika mara kwa mara katika maisha, kama kubadilisha pesa, kununua bidhaa, kutalii, kujitambulisha, na kupiga simu.

Bw. Xu Benyu aliona kuwa kwa waafrika hao waliojifunza lugha ya kichina hivi karibuni, uwezo wa kusoma lugha ya kichina ni muhimu kuliko kuandika. Hivi sasa Bw. Xu Benyu anafundisha wanafunzi wa kipindi cha kwanza cha darasa la mwanzoni, katika kipindi cha pili, wanafunzi watatakiwa kujifunza kuandika kichina, pia kufanya mazungumzo ya kichina yanayotumika mara kwa mara kwenye maisha ya kawaida.

Wazimbabwe ni hodari wa kujifunza lugha. Baada ya kujifunza masomo kwa wiki mbili, wanafunzi wengi wameweza kusema "mwalimu Xu, nina maswali", "jina lake ni nani", "naipenda China", "bei gani kwa kilo moja ya nyanya?", "una kamusi?" "una pasipoti?" "wapi unakotoka", ingawa maneno yao si sanifu sana, lakini bw. Xu Benyu alifurahi sana kwa kusikia wanafunzi wake wakisema lugha ya kichina.

Kufika nchini Zimbabwe kwa vijana wa China wanaojitolea kumewafanya wazimbabwe waone ajabu kwa vitu vyote vya China, hali hiyo pia inamfurahisha Bw. Xu Benyu. Wakati alipokula kwenye bweni, aliwafundisha wafanyakazi wa bweni lugha ya kichina. Mfanyakazi mmoja aliandika maneno yote ya kichina aliyojifunza kwenye kitabu, na kuyaeleza kwa lugha ya huko. Hata wafanyakazi wa super-market walipokutana na vijana wa China, walitaka kujifunza maneno ya kichina. Juhuzi za kujifunza lugha ya kichina zilimfurahisha sana.

Alipozungumzia tofauti kati ya kutoa msaada wa mafunzo mkoani Guizhou na kuwafundisha waafrika lugha ya kichina nchini Zimbabwe, Bw. Xu Benyu alisema, ingawa moyo wa watu wanaojitolea ni wa pamoja duniani, lakini wakiwa vijana wanaojitolea katika nchi za nje, wanaonesha sura ya vijana wote wanaojitolea wa China. Vijana wanaojitolea kwa kueneza lugha ya kichina ni kama mabalozi wanaoeneza utamaduni wa China, jukumu lao si kama tu ni kuwafanya wakazi wa huko waelewe maneno ya kichina, bali ni kuwafahamisha China kupitia mafunzo ya lugha ya kichina, ili kuzidisha urafiki kati ya China na Zimbabwe.

Ingawa Bw. Xu Benyu anafundisha barani Afrika, lakini anawakumbuka sana watoto wa sehemu ya milima ya mkoani Guizhou. Mara kwa mara anawasiliana na wenzake wanaotaka kutoa misaada kwenye sehemu zilizonyuma kiuchumi kwa barua pepe, na kuna barua pepe zaidi ya 100 zinazohitaji kujibiwa. Bw. Xu Benyu alisema barua hizo zote zinaonesha moyo wa kuwasaidia watoto milimani.

Idhaa ya kiswahili 2007-06-01