Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-06-04 18:36:20    
Bush atakabiliwa na masuala mbalimbali katika ziara barani Ulaya

cri

Rais George W. Bush wa Marekani tarehe 4 Juni atakwenda Ulaya kufanya ziara ya siku 8, ambapo pamoja na kuhudhuria mkutano wa wakuu wa kundi la nchi 8 za viwanda utakaofanyika nchini Ujerumani, pia atazizuru nchi tano za Czech, Poland, Italia, Albania na Bulgaria.

Kabla ya kufunga safari rais Bush alipohojiwa na vyombo vya habari vya nchi za Ulaya, alisema anataka kuwaoneshea watu wa Ulaya sura ya Marekani yenye uchangamfu na moyo mwema. Kuhusu maneno yake hayo, vyombo vya habari vya Ulaya vinachambua kuwa, lengo la ziara hiyo ya rais wa Marekani ni kuboresha uhusiano na nchi za Ulaya, kutafuta uungaji mkono wa nchi hizo ili kuhakikisha hadhi ya uongozi ya Marekani katika masuala makubwa ya kimataifa. Kabla ya ziara hiyo, rais Bush alitangaza mkakati mpya wa kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa duniani, akipendekeza kuwa kabla ya mwishoni mwa mwaka 2008, Marekani ikishirikiana na nchi nyingine 15 zinazotoa kwa wingi hewa zinazoleta kuongezaka kwa joto duniani zitaweka malengo mapya ya kupunguza utoaji wa hewa hizo katika muda mrefu. Vile vile alihimiza bunge la Marekani liongeze kwa miaka mingine mitano muda wa mradi wa kuisadiai Afrika kupambana na ukimwi ambao utamalizika mwakani, na kuongeza mfuko huo kutoka dola bilioni 15 za kimarekani kwa hivi sasa hadi dola bilioni 30.

Wachambuzi wanaona, rais Bush atapata maendeleo katika suala la kuboresha uhusiano kati ya Marekani na nchi za Ulaya, hususan baada ya nchi mbili muhimu za Ulaya, Ujerumani na Ufaransa kupata viongozi wapya. Kansela wa sasa wa Ujerumani Bibi Angela Merkel na rais mpya wa Ufaransa Bw. Nicolas Sarkozy wanachukuliwa ni watu wanaotetea uhusiano wa karibu kati ya Ulaya na Marekani. Kwa hiyo rais Bush atajikuta kuwa suala la Iraq lililoathiri uhusiano kati ya Ulaya na Marekani halitakuwemo kwenye ajenda ya mkutano wa kundi la nchi 8 za viwanda wa mwaka huu.

Lakini rais Bush atakabiliwa na changamoto kuhusu suala la kuweka mfumo wa kupambana na makombora katika kanda ya Ulaya ya Mashariki. Russia imeeleza msimamo wake kwamba, hatua hiyo ya Marekani inatishia usalama wa Russia. Viongozi na maofisa waandamizi wa Russia, akiwemo rais Vladimir Putin wameipinga hatua hiyo. Zaidi ya hayo, Russia imechukua hatua za kujizatiti kwa nguvu za kijeshi ili kukabiliana na Marekani. Aidha nchi hizo mbili pia zinapingana katika suala la Kosovo. Hayo yote yanazifanya nchi za Ulaya ziwe na wasiwasi kuwa, huenda Russia na Marekani zitarudi katika hali ya vita baridi, na kufanya mashindano ya kutengeneza silaha. Baadhi ya nchi za Ulaya hazikubaliani na Marekani kuhusu suala la kuweka mfumo wa kupambana na makombora katika Ulaya ya Mashariki. Ndiyo maana katika ziara hiyo, rais Bush atajikuta kuwa, pamoja na kutuliza hasira za rais Putin wa Russia, pia atabeba jukumu la kutafuta uungaji mkono wa washirika wa Marekani barani Ulaya.

Kuhusu suala la mabadiliko ya hali ya hewa, ingawa rais Bush amelegeza msimamo wake kwa kiasi, lakini anashikilia nchi mbalimbali zenyewe ziamue kiasi cha kupunguza utoaji wa hewa zinazosababisha kuongezeka kwa joto duniani. Kauli hizo zimekosolewa na mwenyekiti wa kamati ya Umoja wa Ulaya Bw. Durao Barroso na serikali ya Ujerumani. Bw. Barroso alisema, Marekani ikiwa ni nchi inayotoa kwa wingi hewa zinazosababisha kuongezeka kwa joto duniani, ni lazima ichukue wajibu mkubwa zaidi.