Tarehe 5 Juni ni maadhimisho ya mwaka wa 36 wa "siku ya mazingira safi duniani". Miaka ya karibuni, kutokana na matatizo ya mazingira yanavyozidi kuzingatiwa, nchi zinazoendelea zinachukua hatua mbalimbali za kuboresha mazingira duniani.
Nchini Thailand, hifadhi ya mazingira katika sehemu ya utalii imekuwa kazi muhimu katika juhudi za kuhifadhi mazingira safi nchini humo. Shirika la Utalii la Taifa la Thailand limetunga sheria kwamba ni marufuku kupiga michezo ya filamu katika sehemu za utalii na ni marufuku kuvua samaki na kuchuma marijani baharini.
Kadhalika, Thailand inawashauri watu watumie vipodozi vilivyotengenezwa kwa mimea, na kupunguza kodi kwa wauzaji wa vipodozi hivyo. Katika idara nyingi za serikali na makampuni viyoyozi huzimwa kwa muda wa saa moja kabla ya muda wa kazi kumalizika na kutumia zaidi taa zinazookoa umeme.
Nchini India idara husika imetangaza kuwa mabadiliko ya joto duniani yameiletea India maafa mengi ya kimaumbile. Ukweli ni kwamba India imekuwa ikifanya juhudi nyingi katika kutunga sheria, kufanya harakati za hifadhi ya mazingira. Katika jimbo la kaskazini ambapo kuna watu wengi zaidi, mwishoni mwa mwezi Mei serikali ilitangaza kuwa tarehe 31 Julai itakuwa ni sikuya kupanda miti milioni 10.
Aidha, katika nchi hiyo kuna idara nyingi zisizo za serikali zinashughulikia hifadhi ya mazingira. Moja ya idara hizo inaitwa "fikra za kuhifadhi mazingira ziko shuleni", nia ya idara hiyo ni kuwahamasisha wanafunzi wahifadhi mazingira ya kimaumbile kwa vitendo, na mara kwa mara shule hiyo inawaalika wataalamu wafanye mihadhara, fikra za kuhifadhi mazingira zinakaa akilini mwa wanafunzi hata baada ya wao kupata kazi.
Nchini Kenya kuna maliasili nyingi za utalii, miaka ya karibuni uchafuzi wa mifuko ya plastiki umeathiri vibaya utalii wa nchi hiyo. Wanyama pori wanakufa kutokana na kula mifuko hiyo, na pia maisha ya raia yanaathirika vibaya.
Hivi sasa serikali ya Kenya imekuwa ikitekeleza mpango wa muda mrefu na mfupi wa kutatua tatizo hilo. Kwa mujibu wa mpango huo, serikali imepiga marufuku kutumia mifuko ya plastiki yenye unene wa micron 20 na baada ya miaka miwili mifuko ya plastiki yenye unene wa micron 30 itapigwa marufuku. Zaidi ya hayo serikali inaunga mkono kifedha shughuli za kurudisha mifuko ya plastiki, na kwa sera ya kupunguza kodi inavutia viwanda na maduka ya kuuzia vitu vya plastiki vishiriki kwenye harakati za kupunguza uzalishaji na mauzo.
Nchini Mexico, tatizo la hewa iliyotolewa na magari ni kubwa. Serikali ya nchi hiyo imeanzisha "mpango wa kupambana na uchafuzi" kwa njia ya kuongeza ubora wa mafuta ya magari, kudhibiti utoaji hewa chafu kwa viwanda na kufanya uchunguzi wa hewa. Mjini Mexico kuna mtandao wa kuchunguza hewa na kutangaza ubora wa hewa kila siku kwa nchi nzima. Serikali imeamua kwamba magari yote lazima yachunguzwe hewa kila baada ya nusu mwaka. Kadhalika, kuanzia mwezi Mei mwaka huu imetangaza wito kwa wananchi wajitahidi kutumia baiskeli.
Ili kuboresha ubora wa mafuta ya magari, serikali ya Mexico imetumia dola za Kimarekani bilioni mbili kufanya utafiti na kutengeneza mafuta yaliyo safi zaidi, hivi sasa kampuni ya taifa ya mafuta ya Mexico imekuwa na teknolojia ya kutengeneza mafuta yenye kiasi kidogo cha uchafuzi.
Idhaa ya Kiswahili 2007-06-05
|