Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-06-05 18:41:19    
Barua 0603

cri

Wasikilizaji wapendwa ni watangazaji wenu Chen na Jane Lutaserwa, tunawakaribisha katika kipindi hiki cha sanduku la barua. Leo tunawaletea barua tulizopokea kutoka kwa wasikilizaji wetu.

Msikilizaji wetu Francis Oduko Magio wa S.L.B 4 Mubwayo nchini Kenya, anaanza barua yake kwa kutoa shukurani kwa idhaa ya Kiswahili ya radio China kimataifa kwa kumtumia kalenda pamoja na fomu ya shindano la chemsha bongo, "ama kwa hakika ameamini kuwa China ni nchi inayowazawadia wageni, ana imani kuwa siku moja Mungu atamsaidia kufika nchini China, ndivyo anavyosema bwana Francis Oduko Magio.Vilevile anaomba kama inawezekana jina lake liwekwe katika Jarida la Urafiki na kama jarida la wakati huu lipo basi atumiwe. Anamalizia barua yake kwa kutoa shukurani nyingi na kuwatakia wafanyakazi wote wa idhaa ya Kiswahili Baraka za Mwenyezi Mungu.

Tunamshukuru Bwana Francis Oduko Magio kwa barua yake ya kueleza hisia zake za kirafiki kwetu sisi wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya Radio China Kimataifa, ni matumaini yetu kuwa ataendelea kusikiliza matangazo yetu na kueleza maoni na mapendekezo yake. Kutokana na sababu fulanifulani toleo la mwaka huu la jarida dogo la daraja la urafiki mpaka sasa bado halijachapishwa. Hapa tunaomba radhi , lakini tutafanya juhudi, ili kuchapisha jarida hilo mapema iwezekanavyo. Samahani sana.

Msikilizaji wetu Gabriel Simiyu Wekesa wa kijiji cha Kimalewa, S.L.P 292 Kimilili nchini Kenya, ametuletea barua akisema, pokeeni heri na salamu za mwaka mpya wa 2007, ndivyo anavyoanza barua yake msikilizaji wetu huyu. Anasema, ameyapata maswali ya chemsha bongo ambayo inamalizika mwezi nne mwaka 2007 na anatumaini kuwa atayajibu maswali yote vyema na atapata nafasi maalumu, anaongeza kwa kutoa shukurani kwa zawadi ya maua mazuri.

Vilevile katika barua yake hii anapenda kumshukuru Mutanda Ayub wa Bungoma kwa sababu yeye ndiye alimuonyesha njia ya kuwasiliana na idhaa ya Kiswahili ya radio China Kimataifa.Anaendelea kusema kuwa hivi kimalewa, watu wengi zaidi wanaisikiliza Radio China Kimataifa na wana mpango wa kuanzisha kikundi cha wanasalamu wa Kimalewa, ila anauliza watapataje kadi za salamu? Anaomba watumiwe kadi nyingi.

Anamaliza barua yake kwa kuwatakia watangazaji Chen,Fadhili Mpunji, Han Mei na Anthony Monge, mafanikio katika taaluma ya utangazaji.

Tunamshukuru sana Bwana Gabriel Simiyu Wekesa kwa barua yake ambayo imeonesha amefanya juhudi za kushiriki katika mashindano ya chemsha bongo yaliyoandaliwa na Radio China Kimataifa na kutarajia kupata ushindi. Hapa tunapenda kuwaambia wasikilizaji wetu kuwa, kila mwaka wasikilizaji wetu wengi wanashiriki katika mashindano ya chemsha bongo yanayoandaliwa na Radio China Kimataifa, na wengi kati yao wanatarajia kupata ushindi. Kwa kweli lengo letu ni kuwawezesha wasikilizaji wengi washiriki kwenye vipindi vyetu na kuongeza ujuzi kuhusu China. Radio China Kimataifa kila siku inatangaza kwa lugha 43 zikiwemo lugha 38 za kigeni, hivyo wasikilizaji wa Radio China Kimataifa wanaoshiriki kwenye mashindano ya chemsha bongo huwa ni wengi sana, lakini kila mwaka washindi waliopata nafasi maalumu na kuweza kuja kutembelea China ni wachache, kwa kawaida ni washindi 10 hivi, hivyo si rahisi kuchaguliwa kwa wasikilizaji wa nchi moja au sehemu moja kila mwaka. Ni matumaini yetu kuwa, wasikilizaji wetu wataendelea kusikiliza matangazo yetu na kushiriki mashindano ya chemsha bongo kwa ajili ya kuongeza maelewano na kuzidisha urafiki kati ya China na nchi za Afrika.

Msikilizaji wetu Ali Hamis Kimani wa S.L.B 61 Othoro ,Kadongo nchini Kenya, ametuletea barua akisema pokeeni mkono wangu wa tahania kwa kazi yenu nzuri, ama kwa hakika mmeifanya radio hii kupendwa na wengi, ndivyo anavyoanza barua yake bwana Ali Hamis Kimani wa kule Kadongo nchini Kenya. Ombi lake ni kuwa idhaa ya Kiswahili ya radio China Kimataifa iendelee na moyo huo huo mwaka huu na miaka ijayo.

Aidha, msikilizaji wetu anapenda kumpongeza sana mama Chen huku akiwa na huzuni kuwa aliambiwa mama Chen atastaafu na wataikosa sauti yake tamu, hata hivyo anamtakia maisha mema baada ya kustaafu kwake. Lakini hapa tunapenda kumwambia kuwa, mama Chen bado hajastaafu, ameruhusiwa kuahirishwa muda wa kustaafu kwa mwaka mmoja. Hata akistaafu ataendelea kuwasaidia vijana wa Idhaa ya Kiswahili ya Radio China Kimataifa, anawashukuru sana wasikilizaji wanaompenda.

Bwana Kimani anaikumbusha idhaa ya Kiswahili ya Radio China Kimataifa, kutilia maanani maoni ya wasikilizaji mara kwa mara, kwa mfano anasema alitoa ombi kuwa ingekuwa busara kutangaza majibu sahihi ya chemsha bongo na ikiwezekana kutumwa kwa kila msikilizaji aliyeshiriki kabla kuanzisha shindano jingine. Jambo hilo halijatekelezwa.

Pia anatoa shukurani kwa zawadi anazotumiwa zikiwemo picha za ndege, wanyama pamoja wadudu.Na anaomba atumiwe kalenda ya mwaka huu na jarida la urafiki.Ni matumaini yake kuwa msimu huu bahati itakuwa yake katika chemsha bongo .

Msikilizaji wetu Ali Hamis Kimani anasema katika barua yake nyingine kuwa akiwa na matumaini kuwa tumekuwa tukizipokea barua zake kwa njia ya posta na barua pepe. Hamu yake hasa kujua kama idhaa ya Kiswahili ya CRI, ilipata barua iliyokuwa inaonyesha kwamba amebadilisha anuani .

Bwana Kimani amejawa na furaha tele kutokana na zawadi ya fulana(T-shirt) kutokana na ushindi wa nafasi ya tatu katika chemsha bongo ya mwaka 2006, pia hati ya ushindi ikiwa ni uthibitisho wa ushindi wa nafasi hiyo ya tatu.Pamoja na zawadi hizo, alipata pia kadi za salamu,picha za wanyama, wadudu na ndege, wanaopatikana nchini China na mwisho bahasha zilizolipiwa. Hayo yote yamemtia moyo na kumpa changamoto ya kushiriki na kusikiliza matangazo na vipindi vya idhaa ya Kiswahili ya radio china kimataifa.

Anamalizia barua yake akiwa na matumaini makubwa kuwa siku moja atapata nafasi ya ushindi maalumu katika chemsha Bongo ili aweze kuitembelea nchi ya China na kuwaona watangazaji wa Radio China kimataifa.

Tunamshukuru Bwana Ali Hamis Kimani kwa barua zake za kueleza maoni yake juu ya usikivu wa matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya Radio China Kimataifa, maelezo yake yameonesha juhudi zake za kufuatilia matangazo yetu, pia yametutia moyo sana, kwani tunaona juhudi zetu za kuandaa vipindi zimefanyika na kusifiwa na wasikilizaji wetu, tutaendelea kuchapa kazi ili kuwafurahisha wasikilizaji wetu. Kuhusu ombi lake la kutangaza majibu sahihi ya chemsha bongo na kutumwa kwa kila msikilizaji aliyeshiriki kabla ya kuanzishwa kwa shindano jingine, tutajitahidi kulitekeleza. Asante sana.

Msikilizaji wetu Dominic Ndukis Muholo wa S.L.P 397 Kakamega nchini Kenya, anaanza barua yake kwa kutoa salamu nyingi kutoka kwake mjini Kakamega, akitarajia kuwa wafanyakazi wote wa idhaa ya Kiswahili ni wazima wa afya kwa uwezo wake Mwenyezi Mungu.

Bwana Dominic anashukuru sana kwa kutumiwa fulana pamoja na hati, inayoonyesha kuwa amekuwa mshindi wa nafasi ya tatu, katika shindano la chemsha bongo lililomalizika mwaka 2006.

"Hakika nilikuwa mwenye furaha tele, nilipoenda moja kwa moja kupokea kifurushi cha zawadi zangu, kutoka Radio China Kimataifa" ndivyo anavyosema msikilizaji wetu huyu. Anaendelea kusema kuwa hayo ni maendeleo mazuri, na hatua kubwa ambayo, radio China kimataifa imechukua kuwahudumia wasikilizaji wake.

Bwana Dominic Ndukis Muholo anaendelea kusema, Radio China Kimataifa, inawajali sana wasikilizaji wake wote kwa kuwapa aina mbalimbali za zawadi, kama vile kadi za salamu na bahasha zilizolipiwa stempu tofauti za radio zingine za kimataifa.

Zaidi ya hayo, anawashauri wasikilizaji wote wa Radio China Kimataifa, pamoja na mashabiki, kuzingatia usikivu wa vipindi vyote, na hiyo itachangia ushindi wa nafasi yoyote katika chemsha Bongo. Ni matumaini yake kupata matokeo bora yatakayomwezesha kupata ushindi maalumu katika chemsha bongo ya mwaka huu 2007.

Anamalizia barua yake kwa kuwatakia wafanyakazi wote wa idhaa ya Kiswahili ya radio China Kimataifa heri na Baraka tele, anabakia mwenye furaha tele, huku akiendelea kuisikiliza radio China Kimataifa.

Tunamshukuru Bwana Dominic Ndukis Muholo kwa barua yake ya kueleza maoni yake kuhusu namna ya kusikiliza na kufuatilia matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya Radio China Kimataifa, hii inawasaidia wasikilizaji wengine. Ni matumaini yetu kuwa ataendelea kusikiliza matangazo yetu, na mawasiliano na urafiki kati yake na Radio China kimataifa utaongezwa na kuimarishwa siku hadi siku.