Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-06-06 18:49:08    
China kuharakisha shughuli za kutokomezatatizo la ukosefu wa madini joto mwilini kwenye sehemu za magharibu za China

cri

Naibu waziri wa afya wa China Bw. Wang Longde hivi karibuni huko Urumqi, mji ulioko kaskazini magharibi mwa China amesema, maendeleo dhahiri yamepatikana katika kazi ya kutokomezamagonjwa yanayosababishwa na ukosefu wa madini joto mwilini nchini China, lakini magonjwa hayo bado yanawasumbua wakazi wengi wa sehemu ya magharibi ya China. Kutokana na hali hiyo, China imeweka mkazo kwenye sehemu hizo, ili kutimiza lengo la kutokomezatatizo hilo kwenye asilimia 95 ya miji na wilaya nchini China.

Madini joto (Iodine) ni moja ya madini muhimu mwilini mwa binadamu. Ukosefu wa madini joto husababisha magonjwa mengi ukiwemo ugonjwa wa matezi na ukuaji mbaya wa ubongo. China ikiwa ni moja ya nchi zinazoathiriwa vibaya zaidi na tatizo la ukosefu wa madini joto mwilini duniani, mikoa mingi ya China iliwahi kuathiriwa na tatizo hilo. Tangu miaka ya 80 ya karne iliyopita, Idara husika ikiwemo wizara ya afya ya China, zimechukua hatua mbalimbali na maendeleo dhahiri yameshapatikana.

Katikati ya mwezi Mei, wizara ya afya ya China, kamati ya maendeleo na mageuzi ya China na kampuni kuu ya uzalishaji wa chumvi ya China zilifanya kongamano kuhusu mikakati ya kazi ya kudhibiti tatizo la ukosefu wa madini joto huko Urumqi. Naibu waziri wa afya wa China Bw. Wang Longde alisema:

"matokeo ya uchunguzi na upimaji wa miaka miwili mfululizo yameonesha kuwa, kwa jumla wastani wa madini joto katika mwili wa binadamu nchini China uko kwenye kiwango cha kawaida, kiasi cha matumizi ya chumvi yenye madini joto na idadi ya watoto waliopatwa ugonjwa wa matezi kwa jumla zinatimiza vigezo vya kimataifa kuhusu kutokomezamagonjwa yaliyosababishwa na ukosefu wa madini joto. Hali hiyo imeonesha kazi ya kutokomezatatizo la ukosefu wa madini joto imeingia kwenye nafasi za mbele duniani."

Bw. Wang Longde alisema, katika miaka ya hivi karibuni, China imetekeleza hatua za udhibiti wa jumla, yaani kueneza matumizi ya chumvi yenye madini joto kwenye sehemu zilizoathiriwa vibaya na tatizo hilo. China pia imeweka sheria ya kuagiza utaratibu wa uuzaji wa chumvi chenye madini, na kufanya shughuli kubwa za kueneza ufahamu kuhusu tatizo hilo ili kuinua mtizamo wa wananchi kutumia kwa hiari chumvi chenye madini. Juhudi hizo zimeleta maendeleo halisi.

Naibu mkurugenzi wa shirikisho linashughulikia magonjwa ya kisehemu la China Bw. Chen Jixiang alisema, kuanzia mwaka 1994, baraza la serikali ya China lilitekeleza kanuni za usimamizi wa kutokomezatatizo la ukosefu wa madini joto na kueneza matumizi ya chumvi yenye madini joto kote nchini China. Hatua hizo zimepata maendeleo dhahiri. Bw. Chen Jixiang alisema:

"China ilieneza matumizi ya chumvi yenye madini joto kuanzia mwaka 1995, wakati huo asilimia 30 hivi tu ya watu wa China walitumia chumvi chenye madini, na hivi sasa idadi hiyo imeongezeka na kufikia zaidi ya asilimia 90."

Pamoja na maendeleo yaliyopatikana katika kutokomezamagonjwa yanayosababishwa na ukosefu wa madini joto mwilini, masuala mengine bado yanakuwepo. Naibu waziri wa afya wa China Bw. Wang Longde alisisitiza kuwa, suala la kutopatikana kwa chumvi yenye madini joto kwenye sehemu za milimani na za makabila madogomadogo linapaswa kutiliwa maanani, hasa kwenye mikoa 7 ya magharibi ya China, ikiwemo Gansu, Qinghai na Xinjiang, wilaya 400 zinakabiliwa na ukosefu wa chumvi yenye madini joto. Bw. Wang Longde alisema:

"sehemu nyingi za magharibi ya China zina ukoseu mkubwa wa madini joto kwenye mazingira ya kimaumbile, lakini kutokana na bei kubwa zaidi ya chumvi ya aina hiyo na matatizo yaliyokuwepo katika utaratibu wa usambazaji wa bidhaa kwenye sehemu hizo, baadhi ya wakazi hawawezi kupata au hawamudu chumvi yenye madini joto, badala yake wanachimba wenyewe au kununua chumvi isiyotiwa madini joto, kutokana na masuala hayo, hali ya ukosefu wa madini joto halikuboreka katika muda mrefu uliopita. Hivyo China inapaswa kutoa kipaumbele na kuweka mkazo katika sehemu hizo."

Mwezi Agosti mwaka jana, wizara ya afya ya China iliwatumia wataalamu kufanya uchunguzi kuhusu hali ya ukosefu ya madini joto mkoani Xinjiang. Uchunguzi huo umeonesha kuwa, hivi sasa zaidi ya nusu ya wakulima na wafugaji wanaoishi mkoani huo bado wanatumia chumvi isiyokuwa na madini joto.

Idara ya afya ya sehemu inayojiendesha ya waUyghur mkoani Xinjiang Bw. Mamatimin Yasen alisema, mwaka huu serikali ya sehemu hiyo imefanya utafiti kuhusu kazi ya kinga na tiba za magonwa yanayosababishwa na ukosefu wa madini joto na kuchukua hatua mbalimbali kuhimiza matumizi ya chumvi yenye madini joto, kueneza ufahamu kuhusu tatizo hilo na kutoa dawa za kuongeza madini hiyo mwilini. Bw. Mamatimin Yasen alisema:

"serikali ya sehemu hiyo imethibitisha majukumu na wajibu wa serikali katika ngazi mbalimbali na idara husika katika kazi ya kutokomezatatizo la ukosefu wa madini joto. Serikali pia imeamua kutenga yuan milioni 18 kwa ajili ya utoaji wa chumvi yenye madini joto kwa wakulimu wa sehemu hiyo. Hatua hizo zimeweka msingi imara wa kisera kwa kutimiza lengo la kutokomezakikamilifu tatizo la ukosefu wa madini joto ifikapo mwaka 2010."

Naibu mwaziri wa afya wa China Bw. Wang Longde alisema, ili kuhakikisha zaidi ya asilimia 95 ya miji na wilaya za China zinaweza kutimiza lengo hilo, idara za huduma za afya katika ngazi mbalimbali zinapaswa kuimarisha uongozi wa kazi za kusimamia na kutoa tahadhari kuhusu magonjwa yanayosababishwa na ukosefu wa madini joto, kupanua eneo lilioko chini ya usimamizi, na kuweka utaratibu wa kukabiliana na hali za dharura. Idara husika pia zinapaswa kuandaa kundi la wataalamu na kuinua mtizamo wa umma wa kinga dhidi ya magonjwa.