Wafanyakazi wa Idhaa ya Kiswahili ya CRI
China Radio International
China
Dunia
(GMT+08:00) 2007-06-07 18:56:18    
Maisha ya watoto 20 wa kabila la Wa-uygur wa Xinjiang wanaosoma mjini Beijing

cri

Mwaka 2005, watoto 20 wenye umri wa miaka 14 hivi wa kabila la Wa-uygur kutoka sehemu ya Hetian iliyoko nyuma kimaendeleo ya mkoa unaojiendesha wa kabila la Wa-uygur, kaskazini magharibi mwa China walijiunga na shule ya kazi za sanaa na tamaduni za kikabila ya Beijing kujifunza ustadi wa sanaa, utamaduni na ujuzi mwingine.

Mkuu wa shule ya kazi ya sanaa na utamaduni ya kikabila ya Beijing Bwana Xue Baoxiang alifahamisha kuwa, watoto hao licha ya kujifunza ujuzi wa utamaduni kama wanafunzi wengine, pia wanatakiwa kujifunza kitaalamu uimbaji nyimbo na uchezaji ngoma:

"Watu wa kabila la Wa-uygur ni hodari kuimba nyimbo na kucheza ngoma, hivyo tunashughulikia kuendeleza uhodari wa kisanii wa watoto hao, na kuwawezesha wapate kazi mjini Beijing."

Bw. Xue alisema, hii ni mara ya kwanza kwa watoto hao kuondoka nyumbani, hivyo mwanzoni watoto wengi hawakuweza kuzoea maisha ya Beijing, ili kuwasaidia watoto hao kuondoa upweke walipewa kadi ya simu kuwapigia simu wazazi wao mara kwa mara. Watu wa kabila la Wa-uygur wanazoea kula nyama na vyakula vya unga wa ngano, hawapendi kula wali na vitoweo kama wanafunzi wa kabila la Wa-han. Hivyo kila ifikapo sikukuu au likizo, shule hiyo inawapikia kwa umaalum chakula wanachopenda ili wapate upendo wa kifamilia.

Bw. Xue alisema, ili kuwasaidia watoto hao wajue mambo mengi zaidi ya kijamii, shule hiyo imewapeleka nje kutembelea mara kwa mara kama vile kupanda mlima, ukuta mkuu, kwenda uwanja wa Tian'anmen kuona upandishaji bendera, na kutembelea kasri la wafalme, kasri la mapumziko ya majira ya joto (Summer palace) na bustani ya Beihai.

Msimamizi wa darasa la watoto hao Bi. Yang Pei alisema, walimu wote wa shule hiyo wanawatunza vizuri kama watoto wao weneywe. Katika miaka miwili iliyopita, watoto hao wamezoea maisha ya Beijing hatua kwa hatua, na kila mmoja wao amepata maendeleo yake. Mkuu wa darasa Alijan alisema, amepata maendeleo makubwa katika kucheza ngoma. Alisema:

"Kabla ya kuja Beijing mimi sikuwahi kucheza ngoma, lakini nilichagua somo la kucheza ngoma, na nimepata maendeleo makubwa."

Mambo yanayowafurahisha zaidi watoto hao ni kushiriki katika maonesho na mashindano ya aina mbalimbali ya kuimba nyimbo na kucheza ngoma. Kila shule hiyo inapotembelewa na wageni wa nchi za nje, watoto hao huonesha michezo ya sanaa, na katika tamasha la mashindano ya michezo ya sanaa ya Beijing lililofanyika mwezi Aprili mwaka huu ngoma yao ya kabila la Wa-uygur ilishika nafasi ya kwanza. Jambo hilo limewatia moyo sana.

Hivi sasa watoto hao 20 wa kabila la Wa-uygur wamekuwa na ndoto na malengo mbalimbali kwa siku zijazo. Baadhi yao wanatarajia kubaki Beijing kuendelea na masomo ili kujifunza ujuzi mwingi zaidi, halafu kurudi nyumbani na kuwafundisha wanafunzi wengi zaidi ili kustawisha uchumi wa nyumbani kwao, wengine wanataka kubaki mjini Beijing kuingia kwenye vyuo vikuu kuendelea na masomo na kuwa waimbaji maarufu.

Iko siku watoto hao watatimiza ndoto zao, na walimu waliowahi kuwafundisha watoto hao watafurahia maendeleo yao na kuona fahari kwa ajili yao.